Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika wizara hizi mbili, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Utawala Bora. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi pia kwa kunipa afya njema nami niweze kuchangia kwa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwenye elimu, elimu bila malipo ni suala zuri katika Serikali yetu, lakini wakati inaanzisha elimu bure bila malipo Serikali haikufanya utafiti wa kina. Watu walihamasika sana kuwapeleka watoto wao kujiandikisha, lakini ukatokea upungufu wa madarasa, ofisi za Walimu, vyoo na maabara. Naishauri Serikali hususani mijini maeneo ni madogo ya shule zetu ijenge madarasa kwa style ya ghorofa ili iweze kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi kuliko sasa wanafunzi wanaingia kwa session, wengine wanakuja asubuhi wengine jioni na inapelekea wale wanaokuja jioni hususan katika Jiji la Dar es Salaam kuchelewa kurudi majumbani na wakati mwingine mpaka nyakati za usiku unakuta watoto wako barabarani wanasubiri usafiri wa kurudi nyumbani. Naishauri Serikali sasa itenge fungu maalum ambalo litafika kwa wakati ili liweze kujenga madarasa ya kutosha, vyumba vya Walimu, vyoo pamoja na maabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika barabara zetu hizi za mijini na vijijini Serikali imejitahidi sana hususani katika wilaya yangu ninayotoka ya Temeke imejenga barabara za kiwango cha lami, lakini bado kuna changamoto kubwa sana katika barabara za lami hizo hakuna alama za barabarani hususani katika maeneo yetu, hupeleka magari makubwa ambayo kwa mfano Dar es Salaam kuna barabara ya Mandela, kipindi cha jioni kunakuwa na foleni kubwa sana katika daraja la Mfugale kupelekea magari makubwa kupita katika barabara za mitaani ambazo hazina alama za kuonyesha ni tani gani ya kiasi gani cha gari inatakiwa kupita kwenye eneo hilo. Kwa hiyo nashauri Serikali iweze kuweka alama za barabarani kwenye barabara zetu ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Pia iongeze fungu kwa TARURA kama walivyosema wenzangu kwa sababu kila mtu anahitaji barabara ya lami, lakini kutokana na uchache wa fungu hilo ndio maana kuna maeneo mengi wanajenga barabara za changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu hospitali zetu za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Naishauri Serikali ipeleke vifaa tiba vya kutosha katika hospitali hizo kwa sababu tunaona kuna msongamano mkubwa katika hospitali za rufaa, endapo Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha Madaktari Bingwa wakawepo pia na wauguzi wa kutosha katika vituo vyetu vya afya na hospitali za wilaya hakutakuwa na msongamano mkubwa katika hospitali ya rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano, sasa hivi Hospitali ya Temeke imekuwa hospitali ya rufaa, lakini kunakuwa na msongamano kutokana na hospitali hiyo inahudumua Wilaya ya Kigamboni, pia inahudumia wagonjwa kutoka Wilaya ya Mkuranga na vituo vingine vya jirani. Kwa hiyo naishauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kupeleka miundombinu ikiwepo vifaa tiba vya kutosha katika vituo vya afya kuondoa msongamano katika hospitali zetu za rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hospitali hizo siyo wote wanaoenda kutibiwa wana uwezo wa kulipa gharama ya bili, wengi wanalipia kwa cash na pia hupelekea kutibiwa ugonjwa wao kwa gharama kubwa sana na wakati mwingine wagonjwa hao hupoteza maisha. Naishauri Serikali kupitia TAMISEMI iondoe ile tozo ya maiti kwa sababu ni kero kwa Watanzania, ni kero kwa walipa kodi. Ikumbukwe kwamba marehemu huyo pia alikuwa analipa kodi kwenye Serikali wakati akiwa ananunua bidhaa mbalimbali, hivyo basi katika tozo zote tunashauri Serikali iondoe tozo katika huduma ya kuhifadhi maiti, imekuwa ni kero kwa sababu tunaona maeneo mengi ndugu zetu walioondokewa na ndugu zao huchelewa kuchukua miiili yao kwenye mortuary kutokana na kiwango kikubwa cha kulipia. Naishauri Serikali katika bajeti yao iangalie suala hili ni muhimu sana na ni kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia katika eneo la watumishi. Mheshimiwa Waziri hapa amesema kwamba watumishi lazima wapewe elimu na watumishi hawa wamesema baada ya kuajiriwa wanatakiwa walipe. Naongezea kwa kusema kwamba, sio tu wale ambao wameajiriwa pia wateuliwa wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, wapate elimu ya kutosha ya kujua mamlaka yao ni mwisho wapi kuongoza, kwa sababu tunaona kabisa kuna maeneo mengi ambapo wanatumia mihemko ya kisiasa. Wewe kama kiongozi wa
nchi, kama kingozi wa eneo, kama kiongozi wa mkoa, wilaya unapaswa kufuata maadili au ethic za uongozi, hata kama una itikadi ya chama, lakini hupaswi kuionesha hadharani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia hivi karibuni kuna Mkuu wa Mkoa anatoa tamko kwamba nitahakikisha kwamba Serikali za Mitaa zote, majimbo yote yatakuwa chini ya CCM. Kwa kweli jambo hilo kama ni kiongozi na umesomea uongozi kabisa huwezi kutamka hivyo. Kwa hiyo tunaomba wapatiwe elimu jinsi ya kuongoza kwa sababu hata Rais wetu anaongoza watu tofauti na huduma anatoa na kama ni maendeleo ni maeneo yote bila kujali itikadi. Kwa hiyo elimu si kwa wale ambao wameajiriwa tu pia kwa wateule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia eneo moja la watumishi. Kuna watumishi ambao ni kina mama ambao hupata ujauzito na kujifungua, siyo wote ambao wanajifungua kwa njia ya kawaida, wengine hujifungua watoto wa chini ya umri, watoto njiti (pre-mature) lakini wanapewa likizo sawasawa na yule aliyejifungua kwa kawaida na likizo hiyo ni ya miezi mitatu tu. Ikiwa mwanamke amejifungua mtoto wa miezi mitano, anahitajika kukaa hospitali kwa miezi minne, unakuta likizo ya uzazi inaishia pale pale hospitalini. Mwingine mashallah Mwenyezi Mungu amemjalia akapata watoto wawili, watatu mpaka wanne lakini likizo ni ile ile ya miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali watumishi wa Serikali wanaotakiwa kukaa likizo ya uzazi, kwa wale wenye mahitaji maalum kama hao, waipitie sheria ile na kuweza kuongeza angalau wapewe muda maalum wa kuweza kukaa na kuwahudumia wale watoto, kwa sababu muda mwingi unakuta wako pamoja hospitalini na wengine wamezaa watoto zaidi ya mmoja tofauti na mwanamke mwingine. Kwa hiyo, naishauri Serikali ione haja sasa ya kupitia sheria na kuongeza muda kwa akina mama ambao wamejifungua watoto njiti au mtoto zaidi ya mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la kukaimishwa, sehemu nyingi wafanyakazi wamekaimu. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kwa sababu kuna shortage ya wafanyakazi na watu wako competent mmeshawakaimisha mnajua kabisa wana uwezo wa kufanya hizo kazi, iwaajiri moja kwa moja kwenye nafasi zao na siyo kuwakaimisha kwa muda mrefu. Huwezi kuwa kwenye nafasi ya kukaimu zaidi ya miaka miwili, mitatu. Kwa hiyo, naishauri Serikali, sioni haja ya kuendelea kuwa na makaimu wakati uwezo wa kazi wanao, naomba wawaajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni hali ngumu ya maisha kwa wananchi wetu, kila kukicha afadhali ya jana. Naishauri Serikali ione haja sasa ya kuongeza kipato cha mwananchi wa kawaida hasa mfanyakazi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)