Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pamoja na wasaidizi wake wote. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mbalimbali iliyoelekezwa sana kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la SGR liliongelewa sana, napenda tu kutoa taarifa kwamba mpaka sasa hivi kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro tumekwishafikia asilimia 48. Kazi kubwa ya kujenga tuta kuanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro imekamilika kwa asilimia 98. Imebakia kulaza reli na kuweka miundombinu ya umeme kusubiri uanzaji wa safari ambapo mwezi Novemba tuna hakika safari za kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa njia ya SGR zitakuwa zimeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba transfer of knowledge tunaifanya kwa umakini wa hali ya juu sana. Kuna vijana wetu wengi sana ambao tumewa-attach kwenye mradi mzima lakini kuna wengine ambao tunawapeleka nje ya nchi kuwasomesha kwa awamu. Kwa hiyo, watakapoondoka hawa wakandarasi tutakuwa na timu nzuri kabisa ya kuweza kuendeleza mradi wetu kwa mapana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi waliongelea sana kuhusu meli kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika. Nitoe tu taarifa kwamba tayari tumekwishasaini mkataba wa kutengeneza meli moja Ziwa Victoria lakini tunakarabati meli ya MV Victoria na MV Butiama kwenye Ziwa Victoria. Vilevile tumeshaingia mkataba wa kutengeneza meli moja mpya kwenye Ziwa Tanganyika pamoja na kukarabati MV Liemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi walizotupatia kwa uanzaji na kuimarisha Shirika letu la Ndege la ATCL. Michango yao mingi tumeipokea na tumeendelea kurekebisha hata ratiba ambapo sasa tunaweza ku-move sehemu mbalimbali kurahisisha usafiri wa Watanzania.

Sasa hivi kwa Dodoma siku nne tunasafiri asubuhi na jioni na tunaendelea kuimarisha na tutakwenda na ratiba nyingine mpya huku tukiendelea kukaribisha hata wawekezaji wengine kwa ajili ya kurahisisha usafiri wa anga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imeendelea kuimarisha viwanja vyetu vya ndege sehemu mbalimbali. Mpaka sasa kuna viwanja 11 ambavyo wakandarasi wako katika hatua mbalimbali ya kuvipanua kwa ajili ya kuweza kuhudumia ndege zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuelezea masuala ya mawasiliano, Serikali yetu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kupeleka mawasiliano maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Mpaka sasa hivi nchi yetu tunawasiliana kwa asilimia 94 na hizo asilimia 6 zilizobakia tunaendelea kuzifanyia kazi kwa sababu nyingine ziko kwenye maeneo ambayo jiografia yake ni ngumu kidogo kupeleka mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, barabara za Mikoa zinaendelea kuunganishwa. Tunaamini hivi karibuni nchi yetu mikoa yote itakuwa imeshaunganishwa kwa lami, hasa kwa ile mikoa michache iliyobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)