Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwa maandishi. Kwanza naipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ya kuhudumia wananchi wenye kipato cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Makamu wetu wa Rais mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu kwa kazi nzuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi nzuri anayoifanya. Jimbo langu la Kibiti lina jumla ya Kata 16, Vijiji 58, Vitongoji 272, Shule za Msingi 74, Sekondari 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, katika Jimbo langu la Kibiti kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa kada hii ya afya kama 320 waliopo ni 120. Tunaomba Serikali yetu sikivu ituangalie kwa jicho la huruma. Pili kuna maeneo ya baadhi za kata zina wingi wa watu, lakini hadi leo hakuna vituo vya afya. Kata hizo ni kama Bungu, Ruaruke, Jaribu Mpakanina Mlanzi. Sambamba na hilo kituo cha afya Kibiti kinafanya kazi kubwa kuhudumia wananchi wa kata zaidi ya moja, naomba tufanyiwe ukarabati mkubwa ili kiweze kutoa huduma yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Wilaya ya Kibiti haina gari la chanjo na wagonjwa, ina upungufu mkubwa wa magari, naomba Serikali yetu ituangalie kwa jicho la huruma. Wilayani Kibiti kuna baadhi za kata zipo Delta kwenye Bahari ya Hindi Visiwani kama Kata ya Mbuchi, Kiongoroni, Msala, Maparoni, Salale sawa na kata tano, vijiji 17, vitongoji 42, vipo Delta. Naomba watumishi wa maeneo haya Serikali iwaangalie kwa jicho la kipekee kutokana na kufanya kazi kwenye mazingira magumu, kama kupewa motisha na kutofanya kazi kwa muda mrefu kwenye kituo kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo hatuna kabisa mafriji ya kuwekea chanjo, boti kwa ajili ya kusafirisha pindi mama mjamzito atakapopata rufaa, upungufu mkubwa wa nyumba za watumishi. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kibiti, tunamshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutusaidia vituo vya afya viwili, ambavyo tunavifanyia ukarabati mkubwa na ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambavyo vyote ujenzi wake unaendelea kwa kasi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, moja ya Ilani ya Uchaguzi ya 2015 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni elimu bila malipo (elimu bure). Kwenye Jimbo langu la Kibiti mwitikio wake ni mkubwa sana. Lakini kila panapo mafanikio hapakosi kuwa na changamoto kama vile upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za Walimu, vyoo bora vya kujisitiri Walimu na wanafunzi, upungufu wa Walimu na Walimu kukaa sehemu moja kwa muda mrefu mpaka Walimu sasa wanakuwa kama wanakijiji na baadhi ya Walimu kudai madai yao ya uhamisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo badhi ya shule kwenye visiwa jumla yake ni 17 ambazo Walimu wake mahitaji yao muhimu kama huduma za kibenki inawalazimu waje Kibiti. Naomba Serikali yangu sikivu ituangalie, hawa wapewe hata posho ya kujikimu kwa mazingira magumu kama motisha. Naomba kushukuru kwa kupata pesa za ujenzi wa mabweni, madarasa machache, pikipiki kwa ajili ya Maafisa Waratibu Elimu Kata na pesa za EPFR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji; hadi leo Kibiti hakuna hata mradi mmoja wa maji ambao unatekelezwa licha la kuchimba visima jumla 12 na kupata maji. Naomba Serikali yangu sikivu tuanze kujenga miundombinu ili zana ya kumtua mama ndoo kichwani iendani na kauli ya hapa kazi tu. Tuna miradi Kibiti takriban mitano inahitaji ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara; nashukuru Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kuunda chombo ambacho kinasimamia shughuli za kurekebisha miundombinu yetu katika majimbo yetu TARURA. Chombo hiki kinafanya kazi nzuri, kwa hiyo kuna kila sababu ya kuongezewa uwezo wa kifedha na watumishi ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Changamoto kubwa kwenye Jimbo langu la Kibiti, moja kuchonga barabara za mitaa za Kibiti, Bungu, Jaribu Mpakani, Nyamisati, pamoja na kujenga mifereji yake barabara ya Muhoro Mbuchi, iangaliwe kwa jicho la huruma kupata tuta la kifusi ili iweze kutoa huduma kipindi chote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kumalizia barabara ya kwenda Makao Makuu ya Wilaya, kilomita mbili zilizobakia kwani ujenzi wa Ofisi hii unakwenda kwa kasi kubwa. Wananchi wa maeneo ya DELTA wanapata shida kubwa kipindi wakiwa wanasafiri, tunaomba ujenzi wa magati katika bandari zetu ndogondogo kama Kiomboni, Mfisini, Mchinga, Salale, Simbaulanga, Ruma, Jafa, Mbwera, Kechuru, Maparoni, kujengewa barabara ya lami kutoka Bungu hadi Nyamisati kwani ujenzi wa gati karibu na unakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme; naomba Kibiti ituangalie kwa jicho la huruma katika maeneo ya DELTA visiwani, hadi leo hakuna hata kisiwa kimoja kimepata umeme wa aina yoyote kama Kata ya Salali, Msala, Mparoni, Kiongoroni, Mbuchi na Vitongoji vyake vyote. Hata kwenye maeneo haya ya nchi kavu kama kama Makima, Zimbwini, Mbumba, Msoro, Nyamwimbe, Manguri na maeneo mengine, tunashukuru kwa kupata Meneja wa TANESCO, kwa hiyo tunaomba sasa tujengewe Ofisi ya TANESCO kwenye Wilaya yetu ya Kibiti.