Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika aya ya 33, ukurasa wa 15 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge amezungumzia kuhusu marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na utekelezaji wake ambao umeanza. Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu haijazungumzia hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni kufuatia marekebisho hayo ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni nyeti na tete, kwa kuwa wakati Muswada wa marekebisho ya sheria hiyo ulipotoka, Msajili wa Vyama vya Siasa aliwasilisha pia rasimu ya kanuni kabla hata ya sheria kutungwa. Baada ya kubaini kasoro hiyo, rasimu hiyo ilichukuliwa na Msajili. Hata hivyo, rasimu ya Kanuni hiyo ilionesha kwamba masharti mengi yaliyo kinyume na Katiba ya Nchi na ziada ya mambo yaliyokuwa katika Muswada na sheria yanakusudiwa kupenyezwa kupitia kanuni. Katika muktadha huo Waziri mwenye dhamana pamoja na Ofisi ya Msajili hawapaswi kujifungia na kuandaa rasimu, bali mchakato mzima wa marekebisho ya kanuni zinazohusu Sheria ya Vyama vya Siasa unapaswa kuwa shirikishi na vyama vya siasa viitwe kwa ajili ya majadiliano kuhusu suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika aya ya 36, ukurasa wa 17, Serikali imeeleza kuwa imekamilisha maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hii ni katika hotuba ya tarehe 4 Aprili, 2019 wakati ambapo tarehe 1 na 2 Aprili, 2019 nimeshiriki mkutano baina ya Wizara ya TAMISEMI na Vyama vya Siasa ambapo wadau tulitoa maoni ya marekebisho kwenye vifungu na vipengele vingi vya rasimu ya kanuni zilizowasilishwa. Aidha, tarehe 3 Aprili, 2019 Wizara ya TAMISEMI, ilikutana na Asasi za Kiraia na wadau wengine kwa ajili ya kupokea maoni yao katika kikao ambacho kiliisha jioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo inawezekanaje tarehe 4 Aprili, 2019 isemwe Bungeni kuwa maandalizi ya kanuni za uchaguzi huo yamekamilika? Hotuba hii ya Waziri Mkuu sio ushahidi wa kwamba vikao vya wadau vimeitwa kwa kujikosha wakati ambapo tayari Serikali imeshafanya maandalizi ya kanuni za uchaguzi huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inajitokeza pia katika aya ya 37 ambapo Waziri Mkuu ameeleza kuwa kanuni za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura zimeandaliwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na. 792 na 793 ya tarehe 28 Desemba, 2018. Kanuni hizo ziliandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kutangazwa bila kwanza wadau kupewa rasimu na kutoa maoni. Mwezi Machi, 2019 ndipo NEC ilikutana na vyama kupata maoni wakati tayari kanuni zilishatangazwa. Waziri Mkuu awasiliane na NEC kutoa majibu Bungeni ni lini marekebisho ya kanuni hizo yatafanyika kabla zoezi la uboreshaji haujafanyika nchi nzima. Aidha, naomba kupewa nakala ya Kanuni iliyotangazwa 28 Disemba, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Aya ya 92, ukurasa wa 44 wa hotuba ya Waziri Mkuu, Serikali imezungumzia kuhusu kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Naunga mkono upanuzi wa barabara ya Kimara Mwisho – Kiluvya kilometa 19.2 kutoka njia mbili kuwa nane na ni vyema kiwango cha fedha katika bajeti kikaongezwa na kutolewa kwa wakati ili ujenzi ukamilike mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na ujenzi huo kuendelea, bado nasisitiza haja ya Serikali kuwalipa fidia wananchi waliobomolewa kupisha ujenzi wa barabara hiyo. Ombi hili la wananchi niliwasilisha mbele ya Rais tarehe 19, Desemba, 2018, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo. Rais alikataa ombi hilo kwa maelezo kwamba kesi ilishaamuliwa na Mahakama Kuu. Naomba Waziri Mkuu na Mawaziri wengine wenye dhamana wamkumbushe Rais kuwa kesi anayoirejea wananchi waliohusika ni wa Kimara pekee waliofungua kesi haikuhusu eneo lote linalohusika na ujenzi hivi sasa na haihusu substantive grounds bali wananchi walishindwa kwa technicalities.

Mheshimiwa Spika, baadaye wananchi wa Mbezi walifungua kesi nyingine mwaka 2005 kupitia shauri Na. 80 katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi na hukumu ilitolewa tarehe 31 Mei, 2013 ambapo wananchi walishinda. Pamoja na mambo mengine, mahakama ilitamka kuwa the Highway Ordinance Cap 167, Government Notice No. 161 ya tarehe 5 Mei, 1967 ambayo hutumiwa na TANROADS kutwaa ardhi za wananchi bila fidia ni batili kwa kutofautiana na vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Rais alisema kuwa upana wa barabara wa toka mwaka 1932 uliingizwa kwenye Sheria ya Barabara mwaka 2007. Hata hivyo, ukipitia Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 haina kifungu kinachotaja upana wa Barabara ya Morogoro. Upana unaolalamikiwa sasa uko kwenye Kanuni ya Barabara za mwaka 2009 ambazo zinakinzana na Sheria ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na sheria nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hayo, naomba Rais abadili uamuzi na kuwezesha wananchi hao kulipwa fidia. Kama Serikali haiwezi kulipa fidia kamili basi ifuate misingi ya haki na kuwalipa wananchi hao ex gratia kwa kuzingatia kuwa Serikali yenyewe ndiyo iliyoweka wananchi katika maeneo hayo toka wakati wa operesheni ya vijiji ambapo sasa imewaondoa bila ya kuwalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine naamini Serikali imeona faida ya barabara za mlisho/ mizunguko/pete katika kupunguza foleni kupitia Barabara ya Mbezi – Goba, Temboni – Msingwa – Msigani – Malamba Mawili mpaka Kinyerezi. Kwa umuhimu huohuo, naomba Serikali itenge fedha kwa barabara za Mbezi – Mpiji Magohe, Kibamba – kibwegere, Malamba Mawili – Kwembe na zingine zilizoko kwenye mpango wa barabara za mlisho (feeder), mzunguko (ring) ambazo zitaisadia barabara ya Morogoro inayojengwa zikiunganisha Wilaya ya Ubungo na Wilaya za Kinondoni na Ilala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika aya ya 115 ya hotuba ya Waziri, ukurasa wa 55 ameeleza kwamba hadi Februari, 2019 upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine yanayohudumiwa na DAWASA imefikia asilimia 85. Kiwango cha asilimia 85 hakina ukweli ukilinganisha na hali halisi ya matatizo ya maji ilivyo. Hivyo, katika majumuisho Mheshimiwa Waziri Mkuu aeleze ni vigezo gani vimetumika kupata takwimu hizo kwa kulinganisha baina ya idadi ya kaya na watu katika Jiji la Dar es Salaam na hali halisi ya upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa Jimbo la Kibamba lenye kata sita ili Ofisi ya Waziri Mkuu ishirikiane na Wizara ya Maji na DAWASA kutoa majibu ya takwimu halisi na kuchukua hatua za kuongeza kwa haraka kiwango cha upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mosi, katika Kata ya Goba, Mitaa ya Matosa Goba, Tegeta A na Kulangwa, maji hayatoki na uwekaji wa mabomba ya maji unakwenda kwa kusuasua. Hata katika maeneo ambayo wananchi walijitolea kuchimba mitaro na mabomba kuwepo, lakini maji hayatoki. Kwa hali hiyo upatikanaji wa maji Kata ya Goba hauwezi kuwa umefikia asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Kata ya Msigani, Mitaa ya Malamba Mawili, Kwa Yusufu na mitaa mingine mambomba ya maji hayatoi maji kwa kuwa hayajaunganishwa na bomba lenye maji kwa madai kuwa hakuna vifaa. Mradi uko chini ya kampuni ya India ambayo nayo imeipa kazi kampuni ya kutoka China. Kampuni hizi mbili zinatupiana mpira kuhusu ukamilishaji wa kazi. Aidha, baadhi ya vifaa vinasubiriwa mpaka vitoke India, hali inayofanya mashimo yaliyochimba kuweka mabomba mengine kuanza kujaa mchanga/ udongo. Hivyo, kata hii nayo haijafikiwa kwa asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Kata ya Mbezi Luis, Mtaa wa Makabe, mabomba ya inchi nane yamechimbwa ardhini toka 2017, lakini maji hayatoki na kuwa mtandao na mabomba kwenda barabara za ndani kwenda kuwafikiwa wananchi. Pia kuna ujenzi wa tanki ambao umesimama kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mtaa wa Msakuzi hakuna mtandao wa mabomba. Mtaa wa Luis wameunganishwa walioko kwenye mita 50 kwa mkopo lakini maji hayatoki katika bomba kubwa. Pia maeneo manne katika mtaa huo hayajaunganishwa na Bomba Kuu. Kata hiyo nayo maji hayatoki kwa asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, Kata ya Kwembe, Mtaa wa King’azi B wanamaliza kufunga vizimba lakini maji hayatoki hata kwa walio pembezoni ya bomba. Hali iko hivyo maeneo mengi ya Mtaa wa Mji Mpya. Hivyo, kata hii nayo haina maji kwa asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, Kata ya Kibamba Mitaa ya Hondogo, Kibwegere na mingine hakuna maji. Kibwegere waliahidiwa toka 2016 kupelekewa bomba la inchi nane mpaka Daraja la Mpiji Magohe toka 2016 lakini kazi hiyo haijafanyika. Hivyo, napo haiwezi kuwa asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Kata ya Saranga, Mtaa wa Saranga mabomba ndiyo kwanza yanatandazwa kwa kusuasua. Mtaa wa Kimara B, maji yakitoka ni mara moja kwa mwezi. Kwa ufupi kwa wastani huo haiwezekani Jimbo la Kibamba kama sehemu ya Dar es Salaam kuwa imefikiwa kwa asilimia 85. Hatua gani zitachukuliwa ili kufikia lengo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu pia inapaswa kumshauri Rais kuweka kipaumbele maalum kwenye maendeleo ya vijana na kuongeza fursa za ajira kwa vijana. Tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana lisipodhibitiwa kwa haraka litaleta madhara makubwa kwa nchi. Katika aya ya 138, ukurasa wa 65, programu ya kuendeleza vijana imewezesha vikundi 755 tu ambavyo vimepatiwa shilingi bilioni 4.2 pekee.

Mheshmiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kiwango cha fedha katika mfuko wa maendeleo ya vijana kinapaswa kuongezwa. Katika kutumia mfuko huo, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu itoe mikopo pia kwa vikundi vya vijana katika Jimbo la Kibamba. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali inatarajia kuwezesha vijana kupata mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa vijana 46,950. Mpango huo wa mafunzo utekelezwe. Pia katika Jimbo la Kibamba na Ofisi ya Mbunge na Manispaa ya Ubungo tuko tayari kutoa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ya fursa za ajira, kiwango cha kutengeneza fursa hizo hakilingani na kiwango cha nguvu kazi ya vijana kinachoingia kwenye soko la ajira kwa mwaka. Aidha, kitendo cha jumla ya ajira 221,807 kuwa zimezalishwa kufikia Februari, 2019 huku ajira kwa sekta binafsi zikiwa 75,393, sawa na asilimia 34, kinadhihirisha kwamba programu ya kutengeneza ajira siyo endelevu. Mkakati endelevu wa kuibua fursa za ajira kwa vijana hauwezi kutegemea zaidi utekelezaji wa miradi ya Umma bali kutoa fursa kwa sekta binafsi hutengeneza ajira kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika hotuba yote ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hakuna mahali ambapo amezungumzia kuhusu Baraza la Vijana la Taifa kama nyenzo ya kuwaunganisha vijana kuanzia ngazi ya chini mpaka ya Taifa katika masuala ya maendeleo ya vijana. Sheria ya Baraza la Vijana ilipitishwa mwaka 2015, lakini mpaka sasa miaka mitatu imepita bila baraza kuundwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali kisingizio kilikuwa kutokamilika kwa kanuni jambo ambalo haliwezi kuwa sababu tena kwa kuwa kanuni zilishachapishwa kwenye gazeti la Serikali. Hivyo, katika majumuisho Serikali ieleze mchakato na ratiba ya kukamilisha uundwaji wa Baraza la Vijana katika ngazi zote zilizojatwa katika sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine, kanuni zimeweka utaratibu wa Asasi za Kiraia na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayolenga vijana kuwasilisha maombi ya kufanya kazi kwa baraza. Haya ni mashirika ambayo yamepitia mchakato wa makubaliano (compliance) kwa sheria nyingine zinazotawala mashirika yasiyo ya kiserikali. Kwa uwezo mdogo wa taasisi za vijana, kutakiwa kulipa gharama za usajili/kujiandikisha kwa mamlaka zaidi ya moja ni mzigo mkubwa. Hivyo ni vyema kanuni zirekebishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu ina wajibu, pamoja na mambo mengine wa kushughulikia masuala ya Bunge na Wabunge kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge. Katika masuala hayo ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Wabunge. Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge zitoe maelezo Bungeni ni kwanini Ofisi za Wabunge hazijengwi katika Majimbo mbalimbali ambayo hayana Ofisi za Wabunge mpaka sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Wabunge kupewa Ofisi kwenye majengo ya Wakuu wa Wilaya, kimefanya Wabunge kutokuwa kwa huru juu ya matumizi ya Ofisi hizo. Pia kupewa nafasi ndogo ya chumba kimoja ya Mbunge na Watendaji wake wote na hivyo kukosekana faragha ya kuwahudumia wananchi. Aidha, wapo Wakuu wa Wilaya ambao wamewanyang’anya Wabunge Ofisi kwa maelezo kwamba zinahitajika na Watendaji wengine walio chini ya Mkuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo la Kibamba, lipo katika Wilaya mpya ya Ubungo ambapo kumekuwa na mchakato wa kutenga viwanja/maeneo kwa ajili ya Makao Makuu ya Halmashauri na Mkuu wa Wilaya. Baadhi ya viwanja hivyo vimepatikana kutoka ardhi iliyokuwa chini ya National Housing Corporation (NHC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka kadhaa, nimeiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iratibu mambo nyingine kuwezesha kiwanja/eneo kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mbunge. Hata hivyo, mpaka sasa sijapatiwa majibu stahili. Hivyo katika majumuisho, Ofisi ya Waziri Mkuu inipe majibu, ni eneo gani hasa limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mbunge? Hata kama hakuna fedha za ujenzi kwa sasa, kiwanja kipatikane wakati huu kabla ardhi iliyo wazi haijaendelezwa kwa matumizi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kutaka pia uratibu ufanyike kuwezesha kutengwa kwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama jirani na panapojengwa Makao Makuu mapya ya Wilaya ya Ubungo.