Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa leo nitachangia hoja moja tu na nitaanza kwa kusoma shairi ambalo nimeliita jina la “Dhima”, linasema hivi: “Dhima ipuuzwapo, dhahiri ikawa, husuda ikaongoza, hutia nyoo doa, awaye yeyote kuwa, ajipaye mno madaraka, izara jadidi itamkuta, iwe leo ama kesho. Fundo za majigambo, fitna kwa jamii zitamrudi. Ubinadamu ni ukosefu, ujue sijibereuze.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kuanza na shairi hili kwa sababu naamini, au kwa kiasi kikubwa nitazungumzia juu ya dhima katika lengo la utawala au katika lengo la Taifa. Neno “dhima” nitalielezea huko mbele, lakini linaanzia na kupewa ridhaa ya kuongoza nchi au kukamata dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi Vyama vya Siasa hufikiri kwamba wakipewa ridhaa maana yake ndiyo mwisho wa kila kitu, kwa maana wanaona uchanguzi ndio unamaliza kila kitu. Uchaguzi au kushinda uchaguzi au kupewa kushika dola ni sehemu ndogo sana ya wajibu wa chama ambacho kipo maradakani. Siyo free hander kama wanaweza kufanya chochote, kile lazima kuna maeneo ambayo wanatakiwa wayatazame katika hali nzuri. Huanza kwa kujenga dhana ya kuongoza na siyo kutawala. Kwa ninavyoona mimi, hapa nchini kwetu CCM inatawala na siyo kuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatawala kwa sababu namna wanavyoendesha nchi haikisi human face, haikishi kufungua public space. Nitaelezea huko mbele namna wanavyobana public space. Kwa hiyo, kutawala na kuongoza ni mbingu na ardhi, lakini Kwa CCM tunaona inatawala na siyo kuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaambiwa kuna maendeleo yanafanywa in fact kila mtu anakubali maendeleo ni jambo nzuri; iwe Stiegler’s, Standard gauge, ndege, barabara, madaraja, flyovers na madubwasha mengine yoyote mengine ambayo tunaletewa kama maendeleo. Sehemu ya binadamu ina mbili, ina vitu vya kukamata na ina vitu vipo rohoni. Sasa huwezi kumjazia mtu ukamwambia kwamba kwa kuwa nakuletea ndege, nakujenga daraja, kwa hiyo umnyime haki zake zile ambazo kama binadamu angetaka awe nazo; ku-enjoy public space, lakini pia ku-enjoy vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, studies nyingi zimeonyesha kwamba maendeleo ya vitu siyo maendeleo ya binadamu, lazima kuwa na uhuru wa wananchi kwenye kujikusanya, kwenye maoni, kwenye kujieleza na maeneo mengine. Kwa hiyo, maendeleo bila vitu hivyo, siyo maendeleo kitu. Sasa ili kupewa ridhaa, lazima kuwa na dhima kama chama ambacho kinataka kutawala katika Taifa. Ridhaa ni jambo muhimu sana kwa sababu ndilo ambalo linasimamia vitu vingi. Ni kwamba ukipewa dhima maana yake uendeshe nchi kwa usawa, haki, imani na uadilifu. Bila vitu hivyo basi unakuwa unatawala na huongozi na CCM inatawala, haiongozi, kwa sababu inakosa vitu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuongoza nchi siyo utashi, siyo utakavyo, siyo upendevyo, siyo vyovyote vile, lazima uendeshe nchi kisheria na kikatiba. Hilo kusema kweli linaonekana lina doa katika utawala wa CCM ambao tunakwenda nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, raia wote wanatakiwa wawe na haki sawa wasibaguliwe kidini, kisiasa na kila kitu. Katika hilo tunaliona, raia wa Tanzania hawakuwekwa katika hali sawa. Sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inatakiwa iakisi uendeshaji wa Serikali. Ningetamani Ofisi ya Waziri Mkuu katika bajeti kama hii au katika uendeshaji wa nchi tungeona ina-reflect kwamba inagomba, inakataza, inasimamia kwa wivu kabisa juu ya suala la haki, usawa, imani na uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa CCM inatawala, haingozi, hayo hayaonekani. Nataka nim-quote msanii Idrisa Sultan, aliandika juzi katika twitter, ilikuwa ni suala hili la kutaka suala la CAG, akasema yeye anasaini katika watu 15,000 waliosaini juu suala la CAG kwamba Bunge libatilishe maamuzi yake kwamba akasema nasaini kwa sababu nina wivu na kesho, nataka nione Tanzania ya kesho inatengenezwa. Kwa hiyo, Bunge hili pia au Wizara hii ilipaswa ione kesho yetu sisi kama binadamu, ione kesho ya watoto wetu, ione kesho ya wajukuu zetu na ione kesho ya vitukuu vyetu.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Saleh, kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimwa anayechangia akitaja sana CCM, lakini nilitaka nimwulize kama anapochangia hapo anasimama kama CUF au ACT? Pili, kama ni CUF, anajua kwamba Maalim Seif amekuwa kiongozi Mkuu wa CUF kwa miaka mingapi? Kwa sababu mimi nakumbuka alianza sijui ni enzi ya Mheshimiwa Mwinyi, Mheshimiwa Mkapa, Mheshimiwa Dkt. Kikwete na sasa Mheshimiwa Dkt. Magufuli yupo, sasa anamanisha nini anapozungumzia uongozi na utawala? Ni wapi kuna utawala? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Saleh.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naendelea tu. Nimesema CCM inatawala na haiongozi kwa sababu nina reasons; na reasons zangu siyo za leo, zimekuja kwa muda mwingi sasa. Nitataja mfano, kwa jambo moja tu. CCM katika ilani yake imesema kwamba itakuza vijana ambao wamepata mimba wakati wakiwa shule. Kinyume na Ilani na Sera yake, CCM imebadilika, kwa sababu haina culture ya kuongoza, culture yake ni ya kutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita tu, chama cha CCM kimefanya mkutano wa ndani Sikonge, tumeona mamia ya watu wamekaa, wamefanya mkutano lakini Serikali hiyo haijawazuia kufanya mkutano. Chama hicho cha CCM kimefanya mkutano NIT, wiki hii iliyopita lakini hatuona kuzuiwa. Vyama vingine, iwe CHADEMA, iwe ACT au CUF wakifanya vitu kama hivyo wanazuiliwa. Kwa hiyo, mimi najiuliza, hii Ofisi ya Waziri Mkuu inafanya kitu gani katika kutazama masuala ya kila siku ambapo uhuru wa siasa unaminywa kila siku? Ambapo kila siku uhuru wa kujieleza unazidi kupungua? Ambapo kila siku watu wanapotea, watu wanatekwa, lakini hatukuona uongozi wowote kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiukwaji wa haki za binadamu umekuwa mkubwa nchi hii mpaka juzi Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli akaingilia, mtu ambaye amebambikiziwa makosa na alikuwa ameshakaa kifungoni kwa muda mrefu. Polisi wanazuia vyama vingine kufanya mikutano, tunafika hata maandamano ya amani tunayaogopa. Hivi sasa katika mtandao kuna kikundi kesho kinataka kuandamana kwa ajili ya kueleza hisia zao juu ya kukiukwa Katiba au tishio la kukiuka Katiba uhusiana na CAG, lakini wamezuiliwa wasifanye. Hata maandano ya amani yanakataliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Wapinzani kuporwa Wabunge wao. Pia tunaona kwamba hata suala la Tanzania katika nyanja ya Kimataifa kwenye mikataba ya Kimataifa ya haki za kibidamu ya utawala bora inajitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Bunge haliruhusiwi kuonekana wananchi. Sasa ningetamani Ofisi ya Waziri iakisi katika kuisaidia Serikali kuendesha nchi hii kwa hali ya good faith na public space ili wananchi…

MHE. CHACHA R. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa. Mheshimiwa Ally Saleh unapewa taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHACHA R. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Ally Saleh kwamba jana Tarime Mjini, Mheshimiwa Esther Matiko na Mheshimiwa John Heche walikuwa na Mkutano wa Hadhara. Kwa hiyo, unaposema mikutano inazuiwa, mimi sikuelewi, maana jana walikuwa na mkutano wao na hawazuiliwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Saleh.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Asubuhi Mheshimiwa Gekul alizungumza kwamba alikuwa upande Gaza, naona bado ana Gaza syndrome ndani ya kichwa chake. Hatuzungumzii individual cases na hao ambao wamefanya mkutano baada ya msukosuko. Kwa nini iwe msukosuko wakati ni haki ya kikatiba? Kwa mfano, kufanya mkutano ni haki ya kikatiba, kwa nini uzuiliwe? That is the question, siyo kwamba amepewa mtu mmoja ameonjeshwa ndiyo tuseme kwamba ndiyo general rule, tunataka tuhakikishe…

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka kumpa taarifa mzungumzaji, hivi ninavyoongea sasa hivi, viongozi wa Tarime Jimbo CHADEMA na Mkoa wameshikiliwa na Polisi na wanahojiwa kwa nini walienda kumsindikiza Mbunge wa Chama chao kufanya mkutano jana Tarime? Kwa hiyo, nakupa taarifa. (Makofi)

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa inapokelewa kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kusema kwamba we need to change kama Taifa. Sote…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kaka yangu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba watu wanazuiliwa mikutano na maandamano kwa kutokuwa na nidhamu. Kwa mfano, jana mkkutano wanaozungumza wapo watu ambao wamemsindikiza Mheshimwa Esther Matiko ambao kimsingi sio Wabunge lakini walikuwa wakimtukana Mheshimiwa Rais kwenye mkutano ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Mheshimiwa Esther Matiko mwenyewe kwenye mkutano wake alikuwa anamtuhumu Hakimu aliyeshughulikia kesi kule Mahakamani akamweka ndani na kwamba amepewa dhamana. Sasa katika mazungumzo kama hayo sheria inakataza. Ni lazima Serikali ingalie utaratibu ulivyo. Ukizuiliwa maana yake hukwenda vizuri. Ukiomba mkutano, ukazungumza mambo yanayopaswa, hakuna ugomvi na Serikali wala vyombo vya dola. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya. Mheshimiwa Ally Saleh.

MHE.ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba mambo yanayopaswa siyo mambo ambayo Serikali inayataka, ni yale ambayo kwa uhuru tulionao chini ya Katiba na chini ya Sheria tuna haki ya kusema. Huwezi kumzuia mtu kusema. Kama unamwona ana makosa, mpeleke Mahakamani, siyo umzuilie kusema, siyo utumie utaratibu wa intelijensia kwa vyama vingine lakini vyama vingine unakuwa una madudu kichwani. Lazima tuhakikishe kwamba kama intelejinsia inaonyesha kwamba watu watafanya fujo, basi jukumu la Polisi ni kuwakamata hao ambao wanataka kufanya fujo na siyo kuwazuia wale ambao wana haki ya kukutana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)