Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie bajeti hii ya Wizara ya Biashara. Naomba nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwa hivi nilivyo leo. Kipekee niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Msalala kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa wananchi hawa wa Jimbo langu la Msalala wamenipa nafasi kwa mara nyingine ya kuja kuwawakilisha hapa Bungeni, wamenipa heshima kubwa, naamini nitaitumia vizuri …
Kwa ajili ya maslahi na maendeleo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na timu yake ambayo kwa kweli dhahiri kazi inayofanyika kila Mtanzania anaikubali.
Mimi naamini kampeni nzuri inafanywa na Serikali yetu kupitia matendo ambayo yanafanywa na kwa maana hiyo wana-CCM wenzangu wala tusipate hofu mwaka 2020 kama siyo robo basi watakuwa wamebaki theluthi au watakuwa wamepungua zaidi kwa sababu kazi inafanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa rafiki yangu sana Waziri wa Viwanda. Hotuba yake imesheheni matumaini makubwa sana. Kwa kweli naamini, endapo nia ya Waziri itatekelezwa kama ambavyo mwenyewe anatamani tutafika kwenye nchi ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimsaidie Mheshimiwa Waziri baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kumsaidia sana. Cha kwanza naomba ufahamu kwamba Wizara yake ni kiungo. Serikali kwa miaka mingi ilishajitoa kwenye uzalishaji na kwenye biashara moja kwa moja. Serikali haijengi viwanda, haina mashamba, haifanyi chochote zaidi ya kuweka mazingira mazuri kwa biashara kufanyika. Ili biashara ziweze kufanyika cha kwanza ni muhimu kuangalia mazingira yanayoweza yakaruhusu biashara hizi kushamiri. Ili tuweze kufika huko, nikuombe Mheshimiwa Waziri rejea kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais alipolihutubia Bunge tarehe 20 Novemba, 2015, alituwekea dira kwamba anapenda ndani ya miaka mitano hii asilimia 40 ya ajira zitokane na viwanda. Ni suala kubwa ambalo nilitegemea kwenye hotuba yako kwa kiasi fulani ungeweza kuwa umeligusia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nini kinachopaswa kufanyika kwenye eneo hili ambacho sijakisikia, ninachosikia tu ni kwamba tutakuwa na viwanda na kadhalika.
Nilipenda kupitia kauli hiyo ya Mheshimiwa Rais Waziri atufanyie study na atuletee ili nasi tuweze kuwa tunafuatilia na kumshauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, ni vizuri angeweza kutupa baseline data kwamba hivi sasa ajira zilizopo ni kiasi gani na zinazalishwa ngapi kwa mwaka. Kati ya hizo ajira kiasi gani au asilimia ngapi inatokana na viwanda. Akishapata hiyo takwimu atuambie mwaka 2020, 40% ya ajira zote zitatokana na viwanda maana yake tutakuwa na ajira ngapi zitakazotokana na viwanda. Ili kufika huko aende mbele zaidi ajaribu kuangalia ni sekta zipi zinaweza zikampa hizo ajira zinazohitajika na kuzitazama hizo sekta ni vizuri pia akaangali ni vitu gani vya kufanya katika sekta hizo. Eneo mojawapo la muhimu la kuliangalia ni mazingira ya kodi, upatikanaji wa malighafi pia aina na upatikanaji wa wafanyakazi watakaofanya kazi kwenye hivyo viwanda na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la malighafi ambalo mimi naliona ni muhimu sana hakuna eneo litakalotoa malighafi nyingi za ku-feed viwanda vyetu zaidi ya eneo ambalo rafiki yako na rafiki yangu na mdogo wangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba analisimamia, Wizara ya Kilimo. Wizara hii ya Kilimo ni Wizara pacha na Wizara hii, naomba mfanye kazi kwa pamoja. Sekta hii Mheshimiwa Waziri itakupa 95% ya malighafi zote unazohitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wa eneo moja, malighafi moja muhimu na kubwa inayoweza ikasaidia viwanda ni inayotokana na zao la pamba. Pamba inatoa nyuzi, nguo, mafuta, mashudu yanayotumika kulishia mifugo na vitu vingi ambavyo vyote vinakwenda kutumika kwenye viwanda. Angalia hali ya zao hili ambalo ndiyo malighafi muhimu kwa viwanda unavyohitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1995 pamba tuliyozalisha nchini ilikuwa zaidi ya tani 600,000. Kwa takwimu za Mheshimwia Mwigulu ambazo alizisoma hapa juzi mwaka 2014/2015 tumezalisha pamba tani 245,000 na tunategemea mwaka 2016 tutazalisha pamba tani 145,000 ina maana uzalishaji wa pamba umeshuka kutoka tani 600,000 miaka mitano iliyopita au kama siyo mitano ni kumi hadi wastani wa tani 150,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini uzalishaji wa zao la pamba umeanguka? Kama uzalishaji wa pamba unaendelea kuanguka maana yake hautapata malighafi na bila malighafi maana yake hautapata viwanda na usipopata viwanda, ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kufikia 40% ya ajira zitokane na viwanda haitatimia. Kuna nini kwenye pamba? Yapo matatizo mengi, kaeni na Mheshimiwa Mwigulu mshirikiane kupata majibu ya msingi ya matatizo ya eneo hili. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, matatizo wanayokabiliana nayo wakulima wa pamba moja ni bei inayoratibiwa na soko la dunia. Ni lazima tutafute namna ya kupambana na tatizo la bei. Tuliwahi kupendekeza hapa kwamba ni vizuri tukaanzisha mfuko wa ku-stabilize bei ya pamba (price stabilization fund) ya pamba ili pale bei inapoanguka kwenye soko la duni mkulima aweze kupata fidia. Ni wapi suala hili limefikia? Kaeni na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo mpate namna ya kutatua tatizo hili. (Makofi)
Mhehimiwa Naibu Spika, tatizo la pili linalojitokeza ni suala la dawa. Mwaka huu tumeletewa dawa inaitwa “ninja” haiuwi wadudu. Kimsingi kilichofanyika ni wizi, ni uhujumu uchumi. Mheshimiwa Mwigulu nakufahamu, nakuamini, naomba ufahamu kwamba mwaka huu pamba uzalishaji utakuwa chini ya nusu ya ile uliyotarajia kwa sababu dawa iliyoletwa hii inayoitwa “ninja” haiuwi kabisa wadudu badala yake wadudu wanafurahia kuwa kwenye maji maji ya ile dawa kwa sababu yanawapunguzia joto. Wanakula vizuri zaidi yale matunda ya pamba na pamba haikomai. Kwa hiyo, suala la dawa ya “ninja” naomba tupate taarifa ni nani aliye-supply na kwa nini haiui na hatua gani zinachukuliwa kwenye jambo hili ambalo ni uhujumu uchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la mizani kwenye pamba. Kwa kawaida ninavyojua mimi ni kwamba unapoenda kuuza kitu anayemiliki mizani ni yule muuzaji. Ukienda kwa mtu anayeuza sukari mzani utaukuta kwa muuza sukari, ukienda kwa mtu anayeuza kitu kingine chochote hata petrol station mzani au pump iko kwa muuzaji. Kwa zao la pamba pump au mizani anayo mnunuzi au wakala wake, jambo hili si sawa. Katika mazingira hayo, wanachezea mizani, tulianza na ile mizani ya ruler ikawa haitumiki, sasa hivi wanatumia mizani ya digital ndiyo wanaharibu kabisa wanawaibia wakulima wa pamba. Naomba shirikianeni hizi Wizara mbili mpate ufumbuzi wa tatizo la mizani ya pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine kwenye suala hili la pamba ni kodi kwenye mafuta ambayo yanatokana na pamba hasa VAT ambayo inawanyima nafasi ya kushindana na mafuta yanayotoka nje lakini kubwa na mafuta yanayozalishwa na viwanda vingine. Kwa mfano, pale Shinyanga kuna kiwanda cha Mchina ambacho kimewekwa kwenye mazingira ya uwekezaji ya EPZ, amesamehewa kodi nyingi, wakulima wa kawaida na wenye viwanda vidogo vidogo vingine vya ukamuaji wa mafuta ya pamba hawana misamaha hiyo, kwa hiyo mafuta wanayozalisha wanashindwa kushindana naye. Niombe eneo hili nalo mlirekebishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine hata yale mashudu wanayozalisha kutoka kwenye makapi yanayotokana na matunda ya pamba nayo yanatozwa VAT. Mimi navyojua mali zote au vitu vyote vinavyotumika kwa ajili ya kuendeleza mifugo vinapaswa kusamehewa kodi. Mashudu yanayotokana na pamba yanatozwa VAT matokeo yake wafugaji wanashindwa kuyanunua na kunenepesha mifugo yao. Niombe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Waziri Viwanda na Biashara shirikianeni kupata ufumbuzi, hizi kodi ambazo kimsingi wala hazina maana yoyote zaidi ya kuleta bugudha kwa wakulima na wafugaji ziweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuomba sana, Mheshimiwa Waziri kaa na wafanyabiashara, watakusaidia sana. Kwa kuwa wewe huwezi ukajenga viwanda basi ukae nao watakueleza wana matatizo makubwa ya jinsi kodi zinavyokokotolewa, wana matatizo makubwa jinsi wanavyopata malighafi, wana matatizo makubwa jinsi wafanyakazi wanaoajiriwa kwenye viwanda vyao wanavyo-behave. Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini kwa kiasi kikubwa inajenga mazingira ya wafanyakazi kutofanya vizuri kama ambavyo wawekezaji wanapenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naomba kusema kwamba naunga mkono sana hoja hii, namshauri Mheshimiwa Waziri aondoe vikwazo kwenye upatikanaji wa malighafi. Ahsante sana.