Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba hizi mbili za Katiba na Sheria na Kamati yangu ya Sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo napenda kuongea mambo machache. Kwanza, napenda kuongelea misingi miwili ya Utawala Bora katika nchi yoyote inayoendeshwa Kidemokrasia. Misingi miwili nitakayoiongelea, wa kwanza ni mgawanyo wa madaraka, kwa maana ya separation of power na wa pili ni uwajibikaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote inayotambua misingi hii miwili ya Utawala Bora, ni lazima, siyo tu itekeleza misingi hii, lakini pia ionekane kwamba inatekeleza kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, hasa kwenye upande wa mgawanyo wa madaraka, Tanzania katika uendeshaji wa shughuli za Serikali, tunayomihili mitatu, kwa maana ya Mahakama, Serikali na Bunge. Juzi tulikuwa na Siku Maalum ya Sheria hapa Tanzania. Katika siku hiyo Maalum, iliyofanyika karibu nchi nzima, kitu kinachotarajiwa kwenye siku ile, viongozi wa Judiciary wanategemewa kuitumia siku hiyo kama siku maalum kujadili changamoto na namna bora ya uendeshaji wa Mahakama katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa ambacho nilikishuhudia kinaendelea, ni namna ambavyo Judiciary wanawapa nafasi watu wa Executive (Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa) kwenda kutangaza yale ambayo wanayafanya kwenye Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko forum mbalimbali ambazo tunaweza kuzitumia kutangaza haya tunayotangaza, lakini siku ya Wanasheria Duniani Watanzania wangependa kusikia ni namna gani Judiciary wamejielekeza kupunguza mlundikano wa kesi zisizokwisha Mahakamani, ni namna gani wanapunguza mahabusu waliolundikana Magerezani, ni namna gani wanaongeza Mahakama, ni namna gani wanaongeza Mahakimu na Majaji, katika nchi hii, ili siyo tu haki itendeke, bali ionekane imetendeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaona Majaji na ilitokea Iringa kule, picha moja inazunguka kwenye mitandao. Jaji na Mkuu wa Mkoa, Jaji ki-hierarchy ni mtu mkubwa sana. Sijui kama wamejawa na hofu, sielewi. Jaji anatembea pembeni, kwenye Red Carpet anatembea Mkuu wa Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali itekeleze mambo yake ya Executive na iiache mhimili wa Mahakama uweze kufanya kazi kwa uhuru, ufanye kazi kwa weledi na utashi. Kwa sababu pamoja na kuhubiri maeneo mbalimbali kwamba haki inatendeka, haipaswi...

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka niishauri Serikali, iliwekwa misingi ya Utawala Bora, iliwekwa misingi ya Uwajibikaji, yote hiyo ni kutoa sintofahamu na kutoa ombwe kubwa ambalo lilikuwepo la kuonekana mihimili hii inaingiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa wale wanaosoma, Wanazuoni, huu mjadala ni mkubwa sana. Nawaomba sana, Serikali, Mahakama na Bunge, kuepusha maneno yanayojitokeza ya kuonyesha kwamba mihimili hii inatawaliwa na mhimili wa Executive. Hebu tuoneshe kwa vitendo kwamba tunaweza kujisimamia, kwamba tunaweza kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Katiba na Sheria na Katiba inatulinda kufanya hivyo.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye hoja ya pili kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi, ni lazima kila mtu awajibike kwenye eneo lake. Leo Mheshimiwa Selasini ameeleza vizuri kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Waziri wakati anajaribu kujibu, anasema jambo hili linafanyika kwa uwazi. Sisi ni Wabunge, ni Wawakilishi wa Wananchi, tunasimama hapa kutoa maoni na mapendekezo yetu ya namna bora ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nafikiri Mawaziri wangetumia fursa hii kusikiliza maoni yetu, kuyasimamia, kuyatekeleza kwa mustakabali wa Taifa hili kuliko kusimama kuwa defensive, kwa sababu haimsaidia mtu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Chaguzi kwenye nchi hii ni moja kati ya kitu ambacho kinaweza kutuletea matatizo ambayo yanaweza kuvunja amani. Tusipoandaa uchaguzi huu kwa kufuata taratibu za ushirikishwaji wa wadau…

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sisi Wabunge, moja kati ya jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunaisaidia nchi hii kuwapa uelewa mzuri wa yale tunayoyatunga humu ndani wananchi wetu, kuwasaidia kuwafikishia taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakuja kukutana hapa Bungeni tena mwezi wa Nne, tukitoka hapa ni mwezi wa Saba. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aweke uwazi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili tunapotoka hapa, moja kati ya majukumu yetu iwe ni kwenda kuwaelimisha wananchi na kuwapa taarifa juu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, anasema hiyo kazi inafanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ndicho kinachofanya leo na kesho sisi Wabunge tutukanwe na kuonekana hatuna maana. Tunatoa ushauri, Serikali inaelewa kuliko sisi tunaowakilisha wananchi. Mwisho wa siku, ndiyo kauli zinapozuka mtaani, unazisikia zile; kama ile aliyosema CAG, sijui ameshaomba radhi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais alipohutubia Bunge hili kwa mara ya kwanza. Moja kati ya kitu Mheshimiwa Rais alisema, ni lazima tufute tozo za kero kwa wananchi kwa sababu zinapunguza ufanisi na zinazuia wananchi kufanya shughuli za maendeleo. Juzi Mheshimiwa Rais ameanzisha kitu kinaitwa Vitambulisho kwa Wajasiriamali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)