Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa, naomba niunge mkono Azimio la Bunge Kuridhia Ubadilishaji wa Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika-Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa. Naunga mkono Azimio hili kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, katika mapori haya kwa kweli hali ya kiusalama kwa wananchi wakati wanasafiri kutoka eneo moja hadi lingine ilikuwa si yenye mazingira rafiki. Watu wakisafiri ilikuwa ni lazima kuwe na wasindikizaji kwenye maeneo hayo. Kwa kuipandisha hadhi ina maana hali ya usalama itakuwa imeboreka zaidi na ni jambo zuri kwa maeneo yale na ni jambo zuri kwa wananchi wetu wa Taifa letu la Tanzania kwani kila mtu anahitaji usalama, anahitaji kuishi na anahitaji ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kwenye mapori haya ambayo yamepandishwa hadhi majirani zetu au watu wa maeneo mbalimbali waliweza kuyavamia na kuyamiliki kuwa ya kwao. Kwa muktadha huu sasa hivi hawataweza kuyavamia tena kwa sababu yako chini ya TANAPA watayaangalia katika mazingira bora zaidi. Sambamba na hilo, maeneo haya ni muhimu sana katika uchumi wa Taifa letu na maeneo yale yanayozunguka. Maeneo haya ni mazuri kiutalii kwa sababu ndani yake kuna maziwa, Uwanda wa Savana na vyanzo vya maji ambavyo ni muhimu sana katika mazingira ya kiutalii na wananchi ambao wapo katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukizungumzia Geita kama Geita kuna Uwanja wa Ndege mkubwa ambao unajengwa. Uwanja huu kwa maeneo haya kupandishwa hadhi hautakuwa tena uwanja ule ambao unaitwa white sleeping giant au shite sleeping elephant matokeo yake watalii kutoka maeneo mbalimbali watautumia uwanja ule na utaweza kuleta tija kwa Taifa letu. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa maeneo haya kupandishwa hadhi ili kuweza kuleta mazingira bora na rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku za nyuma kuliwekwa maazimio ya maeneo ya Kusini kuwa ni maeneo ya kiutalii, wakati tunazungumzia maeneo haya tusiyaache yale maeneo ya Kusini kwa sababu Kusini kama Kusini iliachwa nyuma kwa muda mrefu. Kwa hiyo, nachoshauri ni lazima yale maeneo ya Kusini yapewe kipaumbele, wakati huku tunatoa kipaumbele na kule kutolewe kipaumbele kwani Tanzania ni moja na sote ni wamoja.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kurudia tena kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)

Whoops, looks like something went wrong.