Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kunipa fursa ya kuchangia machache katika mapendekezo ya mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hii ni mara ya tatu mimi nachangia mapendekezo ya huu mpango. Lakini kwa bahati mbaya, Waziri wa Mipango anapokuja hapa yale yote ambayo tunazungumza naye anakuwa hayazingatii kabisa.

Kwanza nataka niende katika masuala ya miradi ya kiuchumi ambayo jambo la kufurahisha jana yupo Mbunge mmoja alichangia hapa. Tulisema kwamba tokea awali baada ya dhamira ya kuanzisha miradi hii mikubwa kwa mfano, Air Tanzania ni kwa ajili ya uchumi wa nchi na tukasema kwamba tunakubalina kabisa kwamba tunahitaji Shirika la Ndege ili kuweza kunyanyua uchumi wa nchi yetu. Lakini ilikuwa lazima tufanye utafiti wa kutosha, tutafute wataalam watusaidie ili tukianzisha Shirika liweze kuwa la mafanikio. Lakini haraka haraka shirika likaanzishwa, hakuna tatizo, lakini nimwambie Mheshimiwa Waziri Mpango bado hujachelewa, biashara ya ndege ni biashara moja ngumu sana katika dunia, sio Tanzania tu katika dunia biashara ya ndege ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua matatizo ambayo tunayakabili kwa sasa bado shirika letu halijaanza kazi, ni kwamba tulianza na Bombardier lakini baadae tukaja kwenye Boeing, lakini leo Kampuni ya Bombardier kwa zile ndege za JET imenunuliwa na Air Bus, angalia sasa kwamba ndege hizi ambazo zinakuja sasa hivi E220, wanaozuhudumia sio Bombardier tena ni Air Bus kwa sababu hiki kiwanda kwa ndege za JET hiki kimenunuliwa na Air Bus. Lakini pia tuna hiyo Boeing ambayo tuna ndege moja tayari na nyingine inakuja mwaka 2020 na Bombardier tunazo hizi ndege zao za Q400 ambazo Bombardier bado wenyewe wanazihudumia.

Sasa bado hatujachelewa, ndege zimeshanunuliwa sasa ni wakati wa kutafuta watalaam waweze kulisimamia hili shirika ili liweze kuendeshwa kwa faida, vinginevyo shirika hili litakufa. Kwa sababu leo vitabu vyako viwili vinatofautiana hivi, mapendekezo ya mpango ukurasa wa 14 na kitabu chako hiki ambacho cha hotuba yako uliyoisoma ukurasa wa 27 vinatofautiana.

Kwanza kwenye mapendekezo ya mpango umeelezea hapa kwamba ndege jinsi mlivyozinunua na nini, lakini baada ya kununua hizi ndege ndio sasa mnaenda kutafuta soko la hizi ndege. Hichi ni kitabu chako umeandika wewe mwenyewe vyote vitabu hivi viwili umeandika wewe mwenyewe. Kwa maana baada ya kuliimarisha shirika la ndege lakini pia ndio mnaenda kutafuta masoko sasa ya kuweza kufanya hii biashara ya ndege. Lakini huku unasema kwamba kwenye kitabu hiki cha mapendekezo ya mpango ambacho tulipewa kabla inasema kwamba ndege hizi zitaanza kwenda katika miji hii ambayo imetajwa hapa Bombay, Bujumbura, Guangzhou na Entebe. Lakini kitabu hiki ambacho wewe ulichotusomea hapa Bungeni, kinasema kwamba miji ambayo ndege yetu itakwenda ni Mumbay, Bujumbura, Guangzhou na Entebe. Sasa sijui kipi ni sahihi kati ya hivi viwili, kwa hiyo, naomba uangalie zaidi ili uone tujue wapi pana usahihi na wapi hapana usahihi. (Makofi)

Kwa hiyo, hilo ni jambo moja ambalo ninakushauri kwa sababu hili shirika mmetumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kuliimarisha, kwa hiyo, kama mnataka lifanye faida na linyanyue uchumi basi inabidi sasa patafutwe watu ambao ni wataalam, tuwape kazi hii ili watufanyie reform ya shirika letu. Lakini pia utakapokuja hapa utuambie hili shirika baada ya kununua hizi ndege, ni baada ya muda gani litaweza ku- break even ili tujue kwamba tunakokwenda ni wapi. Kwa hiyo, naomba kwamba utakapokuja kuhitimisha hoja yako ile business plan ambayo mnayo mtuambie baada ya miaka mingapi shirika litakuwa limerejesha ule mtaji na lianze kutengeneza faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kwamba katika mpango huu ambao ameuleta Mheshimiwa Waziri, hakuna kipengele hata kimoja kinachoonesha Zanzibar kimo katika mpango huu ili kuiendeleza Zanzibar na mara nyingi tumesema toka tumetaka kuanza bajeti ya mwaka 2015/2016 tumesema kwa nini haitafutwi japo mradi mmoja au miwili au mitatu ambayo inakuja katika mapendekezo ya mpango kwa ajili ya Zanzibar? Kwa nini kuna tatizo gani? Tatizo gani ambalo linatusababishia mpaka leo kila siku tuzungumzie Zanzibar kwenye mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba huu mpango kwa sababu ni mapendekezo ya mpango utakapoleta mpango halisi basi tuone kwamba Zanzibar, kuna mradi gani wa kiuchumi ambao utaweza kuisaidia Zanzibar. Halafu ukiangalia sisi Zanzibar tuna bahari kubwa tu na sasa hivi mwezi huu nafikiria mwishoni mwa mwezi kuna fanyika mkutano wanaita blue economy ambao unafanyika Kenya, ambao unahusisha mazao ya bahari unakwenda kufanyika, sasa kwa nini basi kusifanyike utafiti wataalmu wako, wasifanye utafiti wakaona kwamba kuna eneo hili mahususi la Zanziba likaweza kukuza uchumi wa Zanzibar kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia la mwisho niseme kwamba Mheshimiwa Mpango katika Bunge lililopita baada ya kutoa maelezo ya mwelekeo kuhusu deni la Zanzibar katika masuala ya TANESCO iliposemwa hapa ulitoa maelezo mazuri sana na Mheshimiwa Spika akakubali, na tukakubaliana kwamba Bunge hili likija hii VAT kwenye deni la umeme, iondolewe lakini kwenye miswada hii imekuja hapa halikuondolewa hili suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie Mheshimiwa Mpango najua masuala yote yanapitishwa kwenye cabinet, lakini suala hili ujachukua juhudi za makusudi kuhakikisha ili jambo lina malizika, wewe mwenyewe personally hujachukua juhudi za makusudi kwa sababu sisi tunazungumza na viongozi ambao wa Zanzibar ambao unafanya nao mawasiliano, lakini ujachukua ile juhudi ya makusudi ya kuonesha jambo hili lina malizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtuambie kwamba sisi Zanzibar siyo ndugu zenu, ndugu zenu ni watu wa Rwanda, Kenya huko na Zambia hao ndiyo jamaa zenu sisi hatumo miongoni mwa Taifa hili ili tujuwe haiwezekani kwamba priority anapewa kutoka Rwanda au kutoka Kenya lakini Zanzibar, anaonekana kama ni mtumwa tu analitumikia hili Taifa. Huu ukoloni utaisha lini? Sisi tumeungana hapa kwa nia njema kabisa, lakini leo sasa hivi, mnaanza kutubadilishia maneno mnatufanya kama sisi watumwa wenu tu, wala hamjali tukipiga makelele.

Mimi nawashauri Wazanzibari wenzangu kwamba sasa ni afadhali tutafute njia ya kutafuta umeme sisi wenyewe badala ya kuja kumpigia magoti.