Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja hii ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza masuala muhimu kwa kuipongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara yake yote ya Fedha na Mipango. Nami sitabaki nyuma, naomba nichukue nafasi kuipongeza sana Wizara hii na Waziri mwenyewe kwa kazi kubwa kwa mpango huu waliotuletea hapa mbele. Ni mpango unaoonekana kabisa unaenda kutuvusha maana tuna lengo la kuivusha Tanzania toka hapa tulipo kuipeleka kuwa Tanzania ya viwanda ili tuingie katika uchumi wa kati mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba nijikite katika masuala matatu hivi katika kitabu hiki tulichopewa cha Mapendekezo ya Mpango, kwanza nizungumzie suala la elimu. Suala la elimu kama ilivyoorodheshwa katika kipengele namba 4.5.1.1(b), kuboresha mazingira ya utoaji elimu katika ngazi za shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari ikijumlisha ujenzi wa madarasa, mabweni na maabara, hili ni jambo zuri sana. Tunapozungumza kutaka kulivusha Taifa kutoka hapa kuingia katika uchumi wa kati elimu ni kitu cha msingi sana. Elimu yetu ni lazima ianzie huko chini awali, msingi, sekondari baadaye ndiyo tunakuja kupata elimu za ujuzi na stadi mbalimbali pamoja na elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa wananchi wa Tanzania wamekuwa wakijitolea sana kufanya shughuli za maendeleo kuunga mkono Serikali yao katika sekta hii ya elimu. Wamezungumza baadhi ya wasemaji waliopita kwamba wananchi wamejitolea wamejenga shule yamebaki maboma, wamejenga zahanati yamebaki maboma, wamefanya kazi nyingi sana lakini yamebaki maboma, Serikali ina mpango gani juu ya hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napenda kabisa niungane na wazungumzaji waliopita nikim-cite ndugu yangu Mheshimiwa Kanyasu kwamba Serikali ina haja ya kufikiria sasa inafanya nini na maboma haya yanayobaki kila wakati. Halmashauri zetu hazina uwezo, haziwezi hata dakika moja, maboma ni mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hilo halitoshi kuna suala zima la watu kujikusuru, wamejenga madarasa mawili kwa uchache ili tusiendelee kuweka maboma mengi, unajenga madarasa mawili mnaezeka mnayaweka sawa. Mkitaka kuanzisha shule, tumesikia shule zina wanafunzi wengi sana wa kuzidi kabisa haifai shule kuwa na wanafunzi 7,000 lakini wananchi wetu wanajitolea wamejenga madarasa mawili wanataka kuisajili shule haiwezekani, sasa tunafanya nini? Siyo tunawavunja nguvu kweli, tunawavunja moyo badala ya kuwatia moyo kwa kuzisajili hizi shule labda na kuwaambia tunaomba kila baada ya mwaka basi muongeze madarasa mawili mengine mzisajili shule ziweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shule nyingi ambazo zimekamilika lakini madarasa mawili haijasajiliwa. Kwa hili kwa kweli ningeshauri Serikali hebu iliangalie kwa kina shule zote ambazo zimekamilika zikiwa na madarasa hayajafika hayo sita zisajiliwe ili wanafunzi waanze kusoma. Tuambizane tu kwamba kila mwaka tujitahidi tuweze kuongeza madarasa mengine pamoja na nyumba za walimu ili tuweze kusonga mbele. Hilo ni kwa upande wa shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la pili la maji na afya. Maji ni muhimu sana ili wananchi wetu wawe na afya bora. Wananchi wetu wakiwa na afya bora wataweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na katika kuisukuma nchi kuivusha kutoka hali hii ya uchumi tuliyonayo hadi uchumi wa kati lakini maji safi na salama ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikishangaa ukiangalia kwa kiasi kikubwa sana vyanzo vya maji na salama ama vinatokana na mito ama vinatokana na mabwawa yaliyojengwa kama hivi tunaona kuna mabwawa ya Farkwa yanatakiwa kujengwa huo lakini wewe ni shahidi Kanda yetu ya Kati, Dodoma maji chini ya ardhi ni mengi sana. Mji wa Dodoma kwa wasiojua unapata maji siyo ya bwawa, siyo ya mto, maji yanatoka kwenye visima kule Mzakwe kwa Mji wote wa Dodoma. Hii ni kudhihirisha kwamba chini ya ardhi Dodoma kuna maji mengi. Sasa inashangaza, nenda vijijini kwetu watu wana shida ya maji kwa nini Serikali isiweke nguvu ya makusudi kuchimba visima vya uhakika kila kijiji ili watu wapate maji safi, wawe na afya bora na washiriki katika kuleta maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maji na kilimo. Tunazungumzia kuivusha nchi hii kwenda kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda vinavyotegemea kilimo. Kama kilimo chetu tutategemea mvua nadhani hapo tumepotea njia. Kilimo chetu lazima kiwe kilimo cha uhakika. Kilimo cha uhakika ni kilimo cha umwagiliaji ama utatumia mabwawa lakini kwa Dodoma kama tunavyoendelea kusema Dodoma maji chini ni mengi Serikali ifanye juhudi ya makusudi maeneo fulani fulani ichimbe visima kwa ajili ya vijana kufanya shughuli za umwagiliaji na uzalishaji ambao utalisha viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee suala zima la umeme. Tunapozungumzia Tanzania ya viwanda maana yake tunazungumzia umeme lakini umeme bado ni tatizo sehemu kubwa sana vijijini yaani tunataka kusema kwamba maendeleo yaje mjini vijijini hapana. Naipongeza sana Serikali kwa mpango mzima wa REA ambao unakwenda kwa kasi vijijini naomba kasi yake iongezwe ili hivi viwanda ambavyo vimeshamiri mijini pia vikapatikane huko vijijini na mambo mengine ya uzalishaji yapatikane vijini badala ya kila jambo kuja mjini. Mazao yazalishwe vijijini yaje mjini kuchakatwa, kwa nini yasichakatwe huko huko, mjini zije ama semi-finished product au finished products kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, mchango wangu ni huo, maoni yangu ni hayo Mheshimiwa Waziri kama akiyachukua akiyafanyia kazi nitashukuru sana. Ahsante sana.