Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuja kusimama tena kwenye Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja. Naunga mkono pia miradi yote ya kimkakati ambayo Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wameileta. Naomba nitumie nafasi hii kuipongeza pia Serikali yangu kwa miradi yote ambayo imekuwa ikiendelea nchi nzima. Tumekuwa tukiona mambo mazuri yanaendelea kufanyika katika nchi nzima. Naamini kwamba haya yanayoendelea yanatokana na kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali nzima pamoja na Wizara yenyewe ambayo anaisimamia Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na tatizo dogo ambalo lipo sasa hivi. Wakati tunahamasisha ununuzi wa EFD tulikuwa na makampuni mengi ambayo tumeyapa license ya kufanya kazi hiyo. Ipo kampuni ilikuwa inauza mashine za Prima, hawa walikuwa wanaitwa Boston Solution Ltd, mashine zao zinalalamikiwa kwamba hazifanyi kazi na inasemekana wamevunja mkataba na TRA na sasa wale walio na mashine hizo wanaambiwa wanunue mashine nyingine. Kwa hiyo, nataka kupata ufafanuzi kutoka Mheshimiwa Waziri na pia kuomba suala hili liangaliwe vizuri kwa sababu kama mzabuni amemaliza mkataba halafu mashine zile zinakosa kazi tutakuwa tunawarudisha nyuma wananchi wetu ambao wananunua mashine hizi bei ghali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze TRA kwa makusanyo mazuri ya kodi. Wameendelea kufanya vizuri na kuwa na lugha nzuri kwa wananchi katika maeneo yetu tunayofanya kazi. Nadhani speed ya ku-recruit new tax payers ku-enlarge tax base imekuwa ndogo kwa sababu tunaweza tukaendelea kukusanya hela nyingi kwa walipa kodi walewale na kama tax base haiongezeki basi tatizo letu la kuwa na bajeti finyu litaendelea kuwepo, nadhani hata mwaka jana nilijaribu kusema haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mpango kwenye Wizara ya Kilimo. Tunajenga viwanda na nilisema mwaka jana, lakini watumiaji wa bidhaa za viwanda zaidi watakuwa ni Watanzania ambao zaidi ya asilimia 70 ni wakulima. Tuna bahati mbaya sana kwamba katika nchi yetu jua likiwaka hasara ni ya mkulima, mvua zikizidi hasara ni ya mkulima, mazao yakipungua na yakizidi pia hasara ni ya mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema kuhusu Price Stabilization Fund, bado sioni kama ni solution namba moja hiyo peke yake. Nafikiri Wizara na wahusika wajaribu kufanya market intelligence kwani yapo maeneo ambayo wakati wakulima wanaingia kwenye kilimo unaweza uka-forecast ukaona mwaka huu tutakuwa na mahindi mengi, dengu nyingi na vitu vingi, unajaribu kuwatengenezea wakulima soko mapema kabla ya kwenda kwenye mgogoro huu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye vipaumbele vya kilimo pale, suala la kutafuta masoko kwa maana ya sehemu ya kuuzia mazao haya halimo, lipo suala la kujenga maghala na masoko ya mazao kwenye maeneo ya wakulima. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ikipatikana surplus, Serikali kwa sababu inaweka restrictions za kuuza mazao haya nje, tuwe na uwezekano wa kuchukua ile surplus ili isionekane ni laana tena mkulima anapovuna mazao yake. Inapoonekana kwamba sasa Serikali imetosha kununua yale mazao basi tuwe tayari na information kwamba wanaweza kupeleka wapi hawa wakulima mazao yao. Hivi tunavyozungumza watu wengi wanakimbia kilimo kwa sababu wanaona sehemu zote zina hasara, jua likiwaka na mvua zikinyesha kuna hasara na suala hili lina hatari sana siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye suala la bidhaa za viwanda. Sasa hivi tunapozungumza hasa sisi tunaotoka pembezoni mwa nchi kama Geita bidhaa zote hata zinazozalishwa Tanzania ni bei kubwa sana. Amesema hapa mchangiaji mmoja mimi nikawa nakumbuka bei ya nondo ya milimita 16 imetoka Sh.15,000 kwenda zaidi ya Sh.28,000 mpaka Sh.30,000. Sasa tunajiuliza hizi bidhaa zote zinazalishwa Tanzania, tatizo liko wapi? Ukiangalia bei ya bati imetoka Sh.160,000 mpaka Sh.450,000, tatizo lipo wapi na ni ndani ya miaka mitatu. Watumiaji wakubwa wa bidhaa hizi ni wakulima, kama wataendelea kuona bidhaa hizi zinapanda maana yake ni kwamba wataacha kulima na watahamia mjini. Kwa hiyo, tutaanza kutengeneza mgogoro wa watu kutoa vijijini kwenda mjini kwa sababu kile anachokifanya kijijini hakimlipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wenzangu wamesema inawezekana ni utitiri wa kodi, lakini inawezekana tunahamasisha wawekezaji waje na wakati huo huo hatujaangalia ni kwa namna gani huyu mtumiaji wa mwisho hii product inamfikia. Sasa hivi maeneo yetu yale ni rahisi kuagiza bati za kutoka Uganda na Kenya ukazinunua kwa bei rahisi kuliko kununua bati za Tanzania, sielewi tatizo lipo wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Naipongeza sana Serikali mwaka jana ilitenga pesa kwa ajili ya kukarabati shule kongwe, naipongeza sana. Lipo tatizo naliona kuhusu shule za msingi. Nilikusikia juzi unasema hapa ipo shule ina watoto zaidi ya 5,000, mimi kwangu Geita Mjini nina shule tatu ambazo zina watoto zaidi ya 4,500 kwa shule moja na madarasa yapo 16 au 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mmoja, kama inawezekana tuje na mpango kabambe kwenye mpango huu wa kuboresha miundombinu ya shule za msingi, halmashauri zetu haziwezi. Shule yenye watoto 5,000 maana yake ndani ya 5,000 kuna shule 7, lakini miundombinu iliyopo ni ya shule moja. Watoto wanaingia asubuhi wanatoka saa sita, wengine wanaingia saa sita wanatoka saa nane, mwalimu mmoja anafundisha watoto 400, hakuna uniformity. Huyu mwalimu hata angekuwa genius namna gani watoto hawawezi kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba kama tulivyofanya kwenye vituo vya afya na zile shule maalum, tuje na progamu maalum ya kuboresha hizi shule za msingi. Tuzitoe hizi shule kwenye watoto elfu moja na kitu twende kwenye watoto 800 au 1,200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hapa kwenye shule, lipo tatizo la watoto ambao wanamaliza sasa darasa la saba na hawawezi kuchukuliwa wote kwenda sekondari za Serikali na hata sekondari za Serikali zenyewe zimejaa. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Elimu, unajua zamani ilikuwa watu wote tunafanya mtihani unaambiwa haukuchaguliwa, si kwa sababu walikuwa hawapendi twende shule, walikuwa wanaangalia uwezo wa shule. Sasa siku hizi shule moja ya sekondari form one inapokea watoto 700, miundombinu iliyopo ni ya watoto 120, kwa hiyo, miezi sita ya kwanza yote Halmashauri inahangaika kuwatafutia watoto pa kusoma, hawa watoto watakuja kupimwa na mtihani ule ule wa watoto walioanza Januari, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tu-come up na mfumo, tujue kwamba Halmashauri hii ina nafasi 2,000, watoto watakaochaguliwa ni watoto 2,000 na watakaobaki watafute shule nyingine, ndiyo maana zamani watu walikuwa wanasoma kwa bidii. Hauwezi kuwa na mfumo wa kuchukua watoto wote, haiwezekani kwa sababu itakuwa kila mwaka hakuna halmashauri ambayo imekamilisha miundombinu. Tulikamilisha madawati mwaka juzi, sasa hivi hakuna shule yenye madawati ya kutosha na tulikamilisha madarasa hakuna shule yenye madarasa ya kutosha kwa sababu mfumo tulionao sekondari ni kuzoa watu wote, hauwezi kuwa na mfumo wa namna hiyo. Kwa hiyo, ni lazima tufike mahali tuseme kwamba nafasi tulizonazo ni hizi na kunakuwa na cutting point kwamba hapa tumekata cutting point, kama nafasi zipo ziende sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo pia la watoto sasa ambao inaonekana kwamba wanapomaliza darasa la saba au wanamaliza form four katika shule binafsi wanakwenda chuo kikuu halafu inaonekana kigezo cha kupata mkopo chuo kikuu unatakiwa uwe umesoma kwenye shule ya watu wanyonge, hiki kigezo si sahihi. Tunafahamu kwamba wapo watumishi ambao walikuwa na uwezo wa kusomesha watoto wake wawili kwenye shule nzuri lakini amestaafu, sasa kama kigezo ni hicho maana yake ni kwamba watoto wengi sana watakosa mikopo na ndicho kinachotokea sasa hivi, watoto wote wanamaliza darasa la saba wanakwenda kurundikwa sekondari ya Serikali kwa sababu anahofia mwanaye asikose mkopo chuo kikuu. Mimi nashauri, kama inawezekana mtoto yeyote aliyefaulu kwenda chuo kikuu apatiwe mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uvuvi, tulipiga kelele sana hapa Bunge lililopita kuhusu uvuvi. Tunashukuru kwamba Serikali ililifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Serikali ililifanyia kazi. Hoja yangu hapa ni ndogo, wavuvi wa sangara sasa hivi kwenye Kanda yetu ya Mwanza wanalalamika bei imepungua na kosa lilikuwa ni moja. Wakati sisi tunafanya operesheni kubwa wenzetu Kenya na Uganda walikuwa wanaendelea na kuvua na kuuza Ulaya. Kwa hiyo, matokeo yake walikamata masoko yetu kule na sasa hivi wavuvi wetu Kanda ya Ziwa wanakosa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri sasa Serikali, kwa sababu lipo tatizo la wamiliki wote wa viwanda vya samaki kuwa ni wa aina moja, wanafanya cartel, wanakaa wanapanga. Tutafute uwezekano wa kutafuta mtu wa kukaa katikati pale ili asiwe anakubaliana na lugha moja wanayozungumza wale wenye viwanda vya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.