Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru sana kwa kupata nafasi hii kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kusifu sana juhudi ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezifanya katika kipindi cha miaka mitatu. Imefanya mambo mengi ambayo yatakuwa ni historia. Napenda sana kusifu hasa miradi mikubwa ambayo imeanzishwa na ambayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa mwaka 2017, kuna mambo mengi ambayo ni ya msingi ambayo yameachwa hayakuorodheshwa kwenye Mpango wa mwaka huu na mapendekezo hayo Kamati ya Bajeti imeorodhesha vizuri sana katika page namba 13. Pamoja na mapendekezo hayo, napenda kujikita zaidi kwenye mambo mawili ambayo naona ni ya msingi sana na napenda kujua kwa nini yameachwa kwenye mapendekezo ya mpango wa mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni barabara ya Chalinze Express Way. Barabara hii naona imeachwa na sijui kwa nini imeachwa. Cha msingi tunaona ni muhimu kwenye mapendekezo haya barabara hii ikaingizwa kwa sababu mapato mengi sana yanategemewa kwenye mambo ya road toll.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikizungumza suala la road toll tangu mwaka 2017 lakini naona bado Mheshimiwa Waziri hajaona umuhimu wake, lakini road toll ni muhimu sana kwa sababu Mataifa mengi duniani sasa hivi unapoenda unakuta kwamba kuna mageti ambayo yanakusanya mapato na mapato yanaweza kupatikana kwa urahisi zaidi. Najua inawezekana sababu mojawapo ni uanzishwaji wa SGR, lakini SGR ni kitu kingine na mambo ya barabara ni kitu kingine kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la Bandari ya Bagamoyo. Bandari ya Bagamoyo imeachwa kabisa na sijui ni kwa nini imeachwa. Bandari hii imeshughulikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Nakumbuka mpaka MoUs ambazo tumewahi kuzisaini kati ya Serikali yetu na Serikali ya Oman pamoja na Serikali ya China tulifanya sherehe kubwa sana kule kwenye Ubalozi wetu Oman kusherehekea mradi huu, lakini sasa hivi naona kama mradi huu haupewi umuhimu ambao unatakiwa. Nashauri kwamba mradi huu na wenyewe uweze kuingizwa kwenye mapendekezo ya mipango ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kiwanda pia cha kuchakachua au kusafisha madini sijaona mpango huo kwenye Mapendekezo ya Mpango huu ya Mheshimiwa Waziri. Ningefurahi sana kama na suala hilo pia lingeweza kuingizwa kwenye mpango huu wa 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uchimbaji wa gesi asilia. Suala hili naona pia limesahauliwa na sijui ni kwa nini, lakini utakumbuka kwamba gesi yetu asilia tulikuwa na wawekezaji wengi sana kule Mtwara na Lindi, lakini wawekezaji wale wameondoka na sasa hivi wamehamia kwenye nchi jirani tu pale, lakini suala hili halijapewa umuhimu wa kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikisoma kwenye mitandao taarifa fulani nikaona kwamba wawekezaji ambao walikuwa wawekeze kule, moja ni Kampuni ya Shell sasa hivi imeenda kuwekeza kule na imejenga mitambo ile ya LNG Canada kule British Columbia kwa gharama kubwa sana. Sasa tunaona tunampoteza mwekezaji mkubwa kama yule na ilikadiriwa kwamba mitambo hii ambayo ingewekwa hapa nchini, kwa mwaka tungeweza kupata zaidi ya trilioni 10 na kuendelea. Ni vizuri hayo mazungumzo ambayo yamekwamisha wawekezaji kuweza kuendelea kuwekeza kwenye suala hili yakapewa umuhimu ili yaweze kufanyika na kufikia muafaka mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo Kamati ya Bajeti imependekeza ni suala la magofu kwenye shule, maabara na zahanati. Kuna magofu mengi sana na mwaka jana kwenye bajeti tulipendekeza kwamba hela nyingi ziwekwe kwa ajili ya kukamilisha magofu haya, lakini naona kwenye mapendekezo ya mwaka huu hayapo. Ni vizuri aka- take note ya mambo hayo ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni miradi ya mikakati. Suala hili ni zuri sana kwa sababu najua miradi ya mikakati ambayo ilipitishwa kwenye mwaka wa fedha 2017/2018 ni 17 tu, lakini ni vizuri miradi hii ikasambazwa kwenye kila Halmashauri, kwa sababu najua ni source kubwa sana ambayo ingeweza kuleta mapato mengi kwa Serikali kama miradi hiyo itaweza kuwekwa kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ni vizuri ikagawiwa kwa usawa kwa sababu utakuta ile miradi 17 ambayo imegawiwa, mikoa mingine imepata miradi miwili, mitatu wakati mikoa mingine haijapata mradi hata mmoja. Ni vizuri iangaliwe ili tuweze kupata usawa katika ugawaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo linatakiwa liongezewe fedha. Kwa kweli Wajumbe wengi wameongea hapa na ni muhimu likaangaliwa. Fedha ambazo zinatengwa kwenye sekta ya kilimo ni ndogo sana na ni vizuri fedha hizo zikaongezwa ili tuweze kusonga mbele kwa sababu kazi kubwa ya Watanzania wengi iko kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji pia ni vizuri liangaliwe. Sasa hivi tumefanya vizuri sana kwenye mambo ya miundombinu, lakini suala la maji bado ni tatizo kubwa, linaleta matatizo mengi sana kwa wapiga kura wetu na wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi huu mpango wa certificate, tumepeleka certificates kule, wakandarasi wamefanya kazi, certificates zimekwama kule karibu miezi sita. Sasa Wizara ya Maji sijui inatuambia nini kwa sababu linakwamisha na jinsi unavyomkwamisha mkandarasi anaongeza interest kwenye ule mradi kufuatana na mkataba ambao upo. Ni vizuri suala hilo likaangaliwa kwa undani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REA pia ni vizuri likaangaliwa kwa sababu wakandarasi wapo na kila siku kule wanakwambia kwamba tunasubiri vifaa. Mheshimiwa Dkt. Kalemani amefika Muheza na ameona hali ya kule, mkandarasi yule uwezo wake ni mdogo kabisa, ameweka vijiji viwili tu mpaka sasa hivi. Tangu Mheshimiwa Waziri amekuja kuzindua, hajaendelea tena, ukimwuliza anakwambia bado vifaa vinakuja, hivyo vifaa vitakuja lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la motisha kwa watumishi wa Serikali. Kwenye Mpango huu sijaona kuongezwa mishahara ya watumishi. Mishahara ya watumishi ni kitu cha muhimu sana, hatuwezi kukaa na watumishi miaka mitatu hatujawaongeza mishahara, pamoja na mambo mengine, lakini hawawezi kuelewa. Kwa hiyo, naomba kabisa kwenye Mapendekezo ya Mpango huu kwenye bajeti ijayo mishahara iweze kuongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.