Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya tatu asubuhi ya leo, mbele ya ma-sterling. Lakini nashukuru leo nachangia mpango wakati Waziri Mkuu yumo humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema mara nyingi na tumekuwa tukiishauri Serikali mara nyingi juu ya nchi yetu twende vipi, lakini Waheshimiwa kabla sijachangia nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba tunailaumu Serikali hii na zaidi Serikali ya Awamu ya Tano lakini mimi naona wa kulaumiwa ni sisi Wabunge, je, Wabunge tunatimiza wajibu wetu? Kazi yetu sisi Wabunge kwa mujibu wa sheria kwa mujibu wa Katiba ni kuisimamia Serikali, je, tunaisimamia Serikali hii? (Makofi)

Kwa hiyo Bunge hili limeshindwa kutekeleza wajibu wake na ndio maana Serikali ikayumba hiyo, hiyo Serikali kama inayumba haifanyi vizuri ni kwa sababu sisi Wabunge tumeshindwa, kwa hiyo, Bunge hili limepoteza nguvu yake, limepoteza hadhi yake, tunashindwa kuisimamia Serikali na ndio maana Serikali inafanya itakavyo. Haiwezekani Bunge hili tupitishe bajeti, sisi sheria inasema, Katiba inasema kwamba tukishapitisha bajeti tuisimamie Serikali, Serikali haifanyi halafu tunaiachia tu hiyo Serikali. Wabunge hatujiamini, tumegawanyika, hatujui wajibu wetu na sidhani kama tunafaa kuwa katika Bunge hili wote humu ndani. Haiwezekani huo ndio wajibu wetu sisi kuisimamia hii Serikali na hatuisimamii, kwa hiyo, Serikali inafanya itakavyo kwa sababu msimamizi ambao ni sisi Wabunge hatufanyi kazi yetu. Tujitathmini sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mpango mimi nakushauri tena, na naiambia tena Serikali na Waziri Mkuu yupo, ubaguzi huu tunaokwenda nao kwenye nchi hii kubaguana, kutoshirikiana hatuwezi kufikia maendeleo kamwe na kama nchi. Ni lazima tukae kama nchi, tuwe na mpango angalau wa miaka 50 tutakaokubaliana kwamba huu ndio Mpango wa Taifa, hii ndio vision ya Taifa, Rais yeyote, Waziri yeyote, Mkuu wa Mkoa yeyote, kiongozi yeyote anaekuja aende hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa natoa mifano mara zote, Serikali ya awamu ya nne tulikopa fedha nje ya nchi kwa sababu ya gesi. Leo kaja Rais ana interest nyingine gesi tumeacha Deni la Taifa, hatuwezi kwenda na huwa nasema huwezi kupima maendeleo ya nchi kwa miaka miwili, mitatu, mitano au kumi ni lazima tuwe na mpango ambao kwa muda wa miaka 50 Rais yeyote anayekuja, Waziri yeyote anayekuja, kiongozi yeyote anayekuja ataenda hapo. Sasa kama hatuko hivyo sisi tunaendelea kubaguana tu hapa, tunaendelea kuwawinda wapinzani, tunaendelea kusema huyu mbaya, huyu hivi, hatuwezi kufikia maendeleo, ni lazima tuache tofauti zetu kama Watanzania tunataka maendeleo tukae kitu kimoja tuweke vision tunataka nini ndani ya nchi yetu. Ubaguzi huu unaoendelea hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikwambie kama kitabu hiki cha Bunge maana yake ushauri wa Kamati ya Bunge ndio Bunge lenyewe kama huu tutaufuata haya yaliyomo humu tu basi nchi yetu itaondoka hapa ilipo na kupiga hatua mbele. Lakini niulize vitabu kama hivi vimeandikwa vingapi na kipi kimetekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nikuombe pamoja na kwamba nazungumza hunisikilizi, nikuombe Bunge hili tukitoka tuseme kwamba hili Bunge limeiagiza Serikali moja, mbili, tatu. Tukija Bunge la Januari hapa katika Mkutano wa Kumi na Nne kama Serikali, turudie kwanza yatokanayo na Bunge la Kumi la Tatu je, Serikali tulitaka mfanye hivi mmefanyaje? Kama Serikali haikufanya basi sisi tuchukue hatua kama Bunge kama tunataka maendeleo. Hatuwezi hivyo Waheshimiwa hii ni mark timer tunadanganyana. Ukisoma hiki kitabu cha Kamati watu wamekaa, wameandika vitu vizuri, vitu vya maana, vitu ambavyo vitatupeleka kwenye maendeleo ya kweli ya nchi yetu, lakini hakuna hata kimoja kinachofanyika.

Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, hebu kaeni, hebu Waziri Mkuu tuondoeni hizi tofauti zetu za kisiasa tulizonazo tukae kama Taifa moja tupange mipango ya nchi yetu tujueni tunakwenda vipi, anayekuja kiongozi yeyote aende hapo isiwe kila mtu anakuja na interest zake hatuwezi kufika. Huwa siku zote naisema na nakuomba hebu tuweke majaribio tu Bunge hili tuliagize Serikali halafu Bunge lijalo tuiulize Serikali kama itakuwa imefanya. Kwa hiyo, hatuwezi kwenda katika mfumo huo tukapata maendeleo kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiyumkiniki nchi zina miaka 48 ya Uhuru wao wana chumi 2 wana mafuta na dhahabu, lakini wametupita mara 5930 sisi tuna miaka 57 ya Uhuru bado tunapiga mark time eti leo Tanzania asilimia 16 ya ardhi ya Tanzania maji, lakini Mbunge anasimama hapa anaomba maji kwa Waziri wa Maji si aibu hiyo? Nchi hii kuna mikoa inalalamika njaa wakati asilimia 53 ya nchi hii ni ardhi ambayo ni productive land.

Kwa hiyo, hatujajipanga sisi wenyewe na tunakaa sisi wenyewe na kutegemea labda misaada, mikopo na ufadhili lakini sisi wenyewe kama nchi hatujajipanga na hatuwezi kufikia hapo kwa mfumo huu wa kubaguana, kwa mfumo huu wa kunyoosheana vidole lazima tukae kama Taifa Waheshimiwa mimi naomba tujiulize tuna laana gani kwenye nchi hii kila kitu tunacho kila kitu tunacho labda tunapitwa na kwa Afrika tunapitwa na DRC tu, labda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nchi nyingine zote tena kwa item moja moja tu lakini vitu vyote tunavyo tuna misitu ya kutosha, tuna maji ya kutosha, tuna ardhi ya kutosha ya kilimo hasa nini tunakuwa hivi ni kwa sababu Serikali hamjaamua sasa na kwa sababu sisi Wabunge tupo hivi labda tuiombe Serikali sasa tuwapigie tena magoti muamue kukaa chini ebu mje tuweke Mpango wa Taifa ambao utatupeleka.

Narudia atamaliza miaka kumi Rais Magufuli pamoja na nguvu yote anayoitumia ataacha hivi hivi katika lawama, lakini ebu tujeni akiondoka Rais Magufuli kama ameazisha hiyo reli ya kati atakayekuja aendeleze asije akaiacha hapa Dodoma kama itakuwa imefika ili tufikie sasa ile lengo, lakini hivi tunavyokwenda hatuwezi kwenda. Mimi napenda kumshauri Waziri katika mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pato letu dogo kama nchi mahitaji makubwa mahitaji ni makubwa, kwa nini tunaenda kwenye miradi mikubwa ambayo inagharimu pesa nyingi na itachukua pesa nyingi na itachukuwa muda mrefu kuanza kuzalisha tusiende katika miradi midogo ambayo itazalisha kwa muda mfupi? Nilisema hapa kwa mfano kama tutajenga mahoteli 100 katika ukanda ule wa bahari Dar es Salaam au Mtwara mpaka Tanga tukajenga mahoteli 100 hali yanachukua mwaka moja kuyajenga baada ya mwaka tunaanza kuzalisha tunaanza kupata fedha ambazo tutazipeleka kwenye Stiegler’s Gorge, tutazipeleka kwenye reli na mambo mengine. Leo tunaanza kufanya miradi ambayo inachukua labda miaka mitano, miaka 10 haijamaliza inakula fedha halafu hatuna njia nyingine ya kupata fedha kwa nini tunaunga kimo kwa kwa kinu? Mheshimiwa hebu twendeni kwenye miradi midogo midogo ili tupate tija kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.