Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza naomba kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wote kwa jinsi wanavyofanya vizuri. Naomba pia kumpa pongezi Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kuiona hii sekta ya madini ni muhimu sana na jinsi anavyoiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niongelee Mkoa wangu wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro una madini mbalimbali. Kwa mfano, Wilaya ya Morogoro Vijijini kule Mkuyuni pamoja na Matombo kuna madini ya dhahabu. Madini haya ya dhahabu yanachimbwa na wachimbaji wadogo wadogo. Hawa wachimbaji wadogo wadogo hawana elimu na mara kwa mara wanachimba na kusafishia kwenye mto mkubwa uliopo hapo hapo Mkuyuni na wanatumia zebaki ambayo wakati mwingine si nzuri kwa binadamu. Kwenye kitabu cha Wizara sikuona vizuri kama Mkuyuni na Matombo imeonekana kuwa tuna dhahabu na wanachimba sana na ipo miaka mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ulanga kuna rubi nayo ni ya muda mrefu, miaka nenda rudi. Kwa hiyo, naomba itambuliwe kuwa Ulanga kuna rubi na inachimbwa na wachimbaji wadogo na inaonekana hawana elimu na soko. Naomba sana hawa wachimbaji wadogo waweze kupatiwa teknolojia nzuri ya uchimbaji wa madini na kupatiwa soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Afisa Madini wa Mkoa, naamini mikoa mingi au kila mkoa kuna Afisa Madini, lakini nilivyosikia na navyojua hakuna Maafisa Madini wa kutosha kwenye wilaya zetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba hilo aliangalie kwa sababu hawa Maafisa Madini ndiyo wanapaswa watoe elimu kwa wale wachimbaji wadogo ili waweze kuelewa wachimbeje madini hayo na wauze wapi. Kwa sababu hawana elimu wanajichimbia wenyewe, hawana vifaa, wakiona jiwe hawaelewi kuwa ni kitu gani wanaendelea wenyewe bila ya kuelewa. Kwa hiyo, naomba hawa Maafisa Madini waweze kupelekwa mpaka huko wilayani ambako madini yanachimbwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kilosa, kuna madini mengi hata mengine siyajui, ni majina ya watu kama Felista nilikuwa sijui kuna madini yanaitwa Felista. Felista ni jina la mama yangu, sasa nakuta kuwa kuna madini yanaitwa Felista. Pia kuna madini ya rubi, red garnet, moonstone lakini sikusikia kama yametajwa, naomba Mheshimiwa Waziri ayafanyie kazi. Mkoa wa Morogoro ni tajiri kwa madini naomba wauangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nimeona kwenye kitabu Mheshimiwa Waziri amesema kwamba utafiti wa awali umefanyika kwenye Mkoa wa Morogoro ila sikuona kama haya madini yametajwa kuwa yanatoka kwenye Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, naomba iangaliwe kuwa tunatoa madini na tuweze kupata wawekezaji kusudi tuweze kuwa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo hawana elimu, wapewe elimu na ruzuku ili kusudi waendelee vizuri na uchimbaji wao na waweze kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa unafahamu kuna Chama cha Wanawake Wachimbaji naomba nao waweze kupatiwa elimu kusudi waweze kuchimba. Unajua ukimuendeleza mwanamke hasa kwenye machimbo na sasa hivi tumesema kazi yoyote hakuna mwanaume hakuna mwanamke yeyote yule anaweza akafanya kazi hii, naomba Mheshimiwa Waziri awaangalie hawa wachimbaji wanawake waweze kuendeleza nchi yetu na kujiletea mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Morogoro kuna wawekezaji wamekuja, kuna mazungumzo yanaendelea hasa Ulanga. Naomba sana waangaliwe kwa sababu hawa wawekezaji tunaomba wawekeze lakini wasiwasumbue wachimbaji wadogo wadogo. Wachimbaji wadogo wapate nafasi yao na hawa wawekezaji waweze kupata nafasi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna graphite, sijui kama Mheshimiwa Waziri anajua kuwa Ulanga kuna graphite. Kwa hiyo, naomba Waziri aangalie na Ulanga ili iweze kuendelea na kunufaika na madini yanayopatikana huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa ukuta wa Mererani. Kwa kweli amefanya jambo zuri katika kudhibiti utoroshaji wa tanzanite ambayo ilikuwa inatoroshwa inaunzwa nje na haifahamiki kuwa imetoka Tanzania inafahamika imetoka mahali popote pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ninalokazia sana ni kuhusu soko la madini hapa nchini. Nashauri Waziri ahakikishe soko la madini linakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tin kule Cherwa ambayo tangu nazaliwa naisikia kule lakini mpaka sasa hivi hakuna kitu chochote kimefanyika kuhusu madini haya.

Mheshimiwa Waziri anafahamu madini ya tin, naomba sana nayo yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi, ahsante sana.