Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Naomba niseme mambo machache kwenye Wizara hii ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina madini mengi sana na pengine Tanzania ingekuwa Korea ya Kusini ingekuwa ni nchi tajiri sana. Nahisi kuna kitu ambacho kama nchi hatujakiona. Tunapambana kuwekeza kwenye vitu ambavyo havina faida, tunaacha kuwekeza kwenye madini ambayo nchi kama Tanzania tungekuwa ni miongoni mwa nchi tajiri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila kona ya nchi kuna madini, leo nikimuliza Mheshimiwa Waziri ana-enroll wanafunzi wangapi wanaoenda kusomea madini? Chuo cha Madini kipo hapa Dodoma kina-enroll wanafunzi 70 kwa mwaka kwa ajili ya diploma, mpo hapa Mawaziri watatu kina-enroll wanafunzi 70. Kwa hiyo, hatujawekeza vya kutosha kwenye madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali kwamba nchi hii kama kuna sehemu tunaweza tukawekeza na tukatoka haraka ni kwenye madini na tuanze na elimu, Watanzania wengi hawajui madini. Hata humu ukiuliza Wabunge wengi dhahabu inafananaje inawezekana physically hawajawahi kuona dhahabu ikoje. Wanaona tu kwenye mikufu labda na kwenye Siwa hapo lakini yenyewe kama yenyewe hawajawahi kuiona lakini dhahabu iko kila kona. Kwa hiyo, niiombe Wizara hebu wekeni fedha za kutosha kwenye elimu inayohusu madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nchi kama Afrika ya Kusini imeendelea sana kwa sababu waliokuwa wanachimba dhahabu Afrika ya Kusini, wale Makaburi ni wa palepale. Faida yote waliyokuwa wanaipata walikuwa hawapeleki Uingereza walikuwa wanawekeza Afrika ya Kusini. Sisi kama Taifa tumewasaidiaje wazawa kumiliki migodi mikubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna wachimbaji wadogowadogo ukiangalia namna wanavyochimba yaani ni aibu. Kama Taifa tunahangaika kwenda kuwekeza billions of money kwenye bombardier, lakini fedha hizo tungepeleka tukawasaidia wachimbaji wadogowadogo wakawa na migodi mikubwa, wakawa kama Acacia, wakawa kama GGM, Taifa tungeondokana na umaskini tulionao. Kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Waziri anapokuja kujibu, hebu watusaidie kama Serikali wanawasaidiaje wachimbaji wadogo ili waweze kufikia kiwango cha kuwa wachimbaji wenye migodi mikubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo pia nataka mje mnipe majibu. Tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano iingie madarakani imevuruga soko la madini hususan gemstone. Wale mnaofahamu pale Arusha wanunuzi wakubwa walikuwa wanakuja kununua gemstone pale Arusha, baada ya hii purukushani ya Serikali ya Awamu ya Tano wamekimbilia Nairobi. Sasa hivi wachimbaji wadogo wanavyochimba hizi gemstone wanaenda kuuza Nairobi, kama Taifa tunakosa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akija atuambie wana mpango au mkakati gani kwa sababu tangu mlivyoingia madarakani mwaka wa kwanza 2016 mpaka leo soko la gemstone halieleweki, soko la madini halieleweki? Leo gemstone za kwetu zinawanufaisha watu wa Kenya, kama Taifa hatulioni hili? Ni miaka mingapi mmesema mnaandaa soko la pamoja pale Arusha ili wanunuzi wanunue hapo, utekelezaji mpaka lini au mpaka Yesu arudi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nipate majibu, tuliambiwa kwamba tunaibiwa sana na ikaundwa Tume ikakuta kwamba tumeibiwa shilingi trilioni 424, hivi ziko wapi? Baadaye nikaona wale Wazungu wamekuja, tukaambiwa eeh, tutawapa shilingi bilioni 700, ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu haya makinikia, Mungu anajua hata kama mkijifanya hamjui, mimi najua haya makinikia ndiyo yalisababisha Mheshimiwa Tundu Lissu kupigwa risasi. Watu walijaa jazba wakasema Mheshimiwa Tundu Lissu ni kibaraka cha Wazungu, kesho yake tunaona Wazungu hao hao mmekaa nao Ikulu. Sasa nataka mtuambie hizi fedha mlisema tunaibiwa na mkatoka kwenye vyombo vya habari pale, ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetengeneza sheria ni kweli na ni sahihi kulinda rasilimali zetu za madini, lakini mmekwishakaa na haya makampuni makubwa ya uchimbaji wa madini tuliyonayo hapa Tanzania mkasikia changamoto zao? Mmeshakaa nao? Maana huko pembeni ukipitia wako hapo, mimi nimejaribu kupita nawasikilizia, wanalia, wanalalamika, sasa kwa nini msikae nao? Kaeni nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri nikuombe Mheshimiwa Waziri hawa watu wenye haya makampuni na pengine wana chama chao, waje watupe elimu nasi angalau tujue. Hivi unadhani Wabunge wanajua nini hapa, wengi hawajui, sehemu kubwa ya sisi Wabunge hatujui haya mambo ya madini. Kwa hiyo, ni vizuri mkatafuta hata semina kwa Wabunge wote wakajua kuhusu mambo ya madini, lakini mkikaa ninyi wenyewe, tunatunga Sheria ya Madini, madini yenyewe hatuyajui, utatungaje sheria hata hujui unachokitunga? Unatunga Sheria ya Madini, madini yenyewe huyajui, utaratibu wa kuchimba madini huujui. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri mkawa- empower Wabunge ili wawe na elimu wajue undani kuhusu haya madini, ili wanavyotunga sheria wanajua wanachotunga. Bila hivyo watatunga sheria ya kukomoa, mwisho wa siku utadhani unawakomoa hawa Wazungu kumbe unawakomoa na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.