Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kulinda rasilimali zetu yakiwemo madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nielekeze mchango wangu moja kwa moja katika Mkoa wa Manyara, Mererani. Naipongeza sana Serikali na Wizara na Jeshi la Ulinzi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kujenga ukuta wa Mererani. Kwa kweli, vijana wale walikuwa wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mkuu wa Majeshi kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kumaliza ule ukuta wa Mererani kwa wakati. Ingawa Mheshimiwa Rais aliposema kuwa ule ukuta ujengwe, watu walibeza sana kuwa hautaisha, lakini Jenerali Mabeyo alijitahidi wakamaliza kwa wakati. Naomba niwapongeze sana. Kweli nchi yetu ina watu wazalendo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu tu alipoamua kujenga ukuta wa Mererani alitaka madini yetu tuyauze wenyewe na yatufaidishe Watanzania wenyewe ili tulipe kodi na hizi kodi zinufaishe nchi yetu katija sekta mbalimbali. Kwangu mimi ukuta ni ishara tu ya ngome ya ukuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ukuta huu uwe kumbukumbu, mali zetu ni lazima zitufaidishe sisi wenyewe na sasa mali zetu imetosha kuwanufaisha wageni na Watanzania wachache. Madini yetu yanatakiwa yatunufaishe Watanzania na vizazi vijavyo. Mheshimiwa Rais wetu ana nia hiyo na Watanzania tunamuunga mkono Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa uzalendo huu mkubwa aliouonesha kwa nchi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuta huu wa Mererani unatakiwa uwe kielelezo cha dhuluma iliyodumu tangu mwaka 1967 ambapo madini haya ya tanzanite yaligundulika. Mheshimiwa Rais wetu tumeona alivyoonesha uzalendo kuzungushia ukuta na kuwa mkali na rasilimali hii ya madini hasa haya ya tanzanite. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa ya Mheshimiwa Rais wetu pamoja na Wizara, lakini nataka kusema hivi, madini bado yanatoroshwa. Madini ya tanzanite bado yanatoroshwa, yanaenda nchi za nje, wanapitia njia mbalimbali. Naamini sana vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi. Kama tu mimi Mbunge najua kuwa madini ya tanzanite bado yanatoroshwa, nina uhakika kwamba wenyewe wakifuatilia hili watagundua na wawe makini sana na mipaka yetu. Madini ya Tanzanite bado yanapita mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa hii kazi kubwa, Wizara inavyohangaika na Mheshimiwa Rais wetu, watakaokamatwa wanatorosha madini yetu, naomba wachukuliwe hatua kali sana. Hawawezi wakachezea rasilimali zetu ambazo tumekuwa tunahangaika nazo kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niko Mererani. Tumeona wale Wanaapolo wakiwa wanachimba madini na tunaona wale wamiliki wa migodi wakiwa wanahudumia madini. Hii migodi ya Mererani ni kama bahati nasibu. Mtu anaweza akachimba hata miaka 10 au 20 asipate. Kuna kitu kimoja tulikisikia hata kwenye Kamati yangu nilibisha sana kuwa hawa wamiliki wa migodi wawe wanawalipa mshahara hawa wachimbaji kila mwezi. Kwa kweli, tusijidanganye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara wanatakiwa wafanye uhakika wa hiki kitu, wakiangalie kwa umakini, ni ngumu sana. Kwa sababu hawa wachimbaji unakuta wakati mwingine mpaka wanakopa tu ili kulisha migodi yao ili iweze kutoa mawe na unakuta inakaa hata miaka 20 haijatoa. Nasi tangu tunakua tunaonana na Wanaapolo tunaishi nao mitaani, haijawahi kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tu Wizara iangalie mkakati mzuri wa kuweka ili hata watakapopata waangalie hawa wachimbaji ambao tumezoea kuwaita Wanaapolo wapate malipo yao, kwa sababu, kwa kusema hili la kulipwa kila mwezi tusijidanganye, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja katika Mkoa wangu wa Arusha, Wilaya ya Longido, Kijiji cha Mundarara. Kijiji kile kina wachimbaji wa madini ya aina ya rubi. Wachimbaji hawa wamekuwa wakihangaika muda mrefu sana kujitafutia kipato chao kihalali kabisa, lakini wachimbaji hawa wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ambapo wana imani kubwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba itatatua kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa waliyonayo ni madini haya mara wanapopata wanataka yakatwe na madini haya yakishakatwa thamani yake inapungua. Sasa tunakuwa tunafanya nini? Tunataka tuwasaidie wananchi wetu au tunawaumiza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai kunaweza kukawa kuna sheria, lakini Wizara lazima ikae tuangalie hii sheria, kama inawaumiza wananchi wetu, ibadilishwe, tutunge sheria ambayo inawafaidisha. Kwa sababu tunasema madini yanatakiwa yanufaishe Watanzania na wananchi wetu wote kwa ujumla. Sasa kama haya madini yakikatwa yanaumiza wananchi wetu, yanawaumiza hawa wachimbaji, kwa nini tusiangalie sheria ambayo itawasaidia wachimbaji hawa wa Mundarara ili na wenyewe waweze kuchimba kwa amani na waweze kupata thamani na madini yao ili malengo yao waliyokusudia yatimie? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri, dada yangu Mheshimiwa Angellah Kairuki, kaka yangu Mheshimiwa Doto na Mheshimiwa Nyongo nawaamini, najua kwenye hili mtawatendea haki watu wa Mundarara. Nawaombeni sana mnapokuja, mje na jibu la uhakika ili watu wa Mundarara wajue hatima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba sana watakapotoa vitalu katika maeneo haya waangalie wazawa ambao ni wananchi wa Longido. Wasije wakawapa wageni tukawasahau wananchi wazawa ambao ndio wapo katika maeneo hayo kila siku. Naomba sana Mheshimiwa Waziri hili suala aliangalie kwa makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nakushukuru sana, siku ambayo niliuliza swali kuhusu Longido, Mundarara hapa, nashukuru Mawaziri wangu ni wasikivu. Mheshimiwa Nyongo alienda mpaka Mundarara baada tu ya kuuliza lile swali na akakutana na wananchi wa Mundarara. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wako kwa kuwa wasikivu kwa wananchi na Wabunge kwa ushauri wetu. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niendelee kuipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi kubwa inayofanya tangu kuanzishwa kwake. Tumeona maduhuli yanazidi kuongezeka. Kwa mfano, mwaka 2017/2018, Wizara ilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 194.66 lakini hadi tarehe 31/03/2018 ilikusanya shilingi bilioni 225 sawa na 115.59%. Mafanikio haya yamechangiwa na juhudi mbalimbali ikiwemo kurekebisha Sheria ya Madini ya Mwaka 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze sana Serikali, naomba nimpongeze dada yangu ambaye ni Waziri wa Madini wa kwanza, Mheshimiwa Dada Angellah Kairuki, unafanya kazi sana mwanamke mwenzetu. Naomba tukutie moyo na wanawake wenzako tunaendelea kukutia moyo, piga kazi tuko na wewe na tunakukubali sana. Huna majivuno, unatusikiliza na uko tayari kushaurika na kukosolewa. Piga kazi dada yangu, tuko na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niwapongeze Manaibu wako Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Doto. Vilevile jamani Wizara hii ina viongozi wenye busara sana, wamekuwa pamoja nasi, tunawasumbua muda mwingi na wamekuwa wakitusikiliza na kutatua kero mbalimbali. Kwa kweli, Mheshimiwa Rais hakufanya makosa kuwapa hiyo Wizara, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu, aendelee kufanya kazi. Alivyoongea kuhusu ukuta, alivyokuwa anaongea kuhusu madini kuna watu walimdhihaki humu humu ndani, lakini wameshindwa, Watanzania wanamkubali Rais wetu na Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kutekelezwa, tupo na wewe Rais wetu. Piga kazi, sasa hivi matokeo wanayaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.