Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ziwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, anafanya vizuri, lakini Katibu Mkuu, mzee Iyombe, ni miongoni mwa watu mahiri ambao wanalazimu watambulike katika utumishi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na e-Government, Wakala wa Serikali Mtandao (eGA). Kabla ya kusema chochote napendekeza moja kwa moja kwamba Serikali ituletee Muswada wa sheria hapa Bungeni tuibadilishe eGA kuwa mamlaka. Nayasema hayo kwa sababu kama wakala hana uwezo wa ku-enforce, yeye kazi yake ni kushauri, hawezi kudhibiti wala hawezi kufanya kitu chochote ambacho hata mlaji anapokataa kufuata zile regulations na ile miongozo; kama wakala hana uwezo wa ku-enforce sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali ilete Muswada wa sheria hapa tubadilishe. Kwa sababu gani; kwa sababu katika dunia ya sasa ukitazama research iliyofanywa na cyberspace, inavyofika 2025, internet users watakuwa 4.7 billion, wanafunzi waliohitimu kwenye hisabati, sayansi, engineering, technology, watafika milioni kumi na sita kwa mwaka. Ongezeko hilo linahitaji uwepo wa chombo ambacho kitaweza kukabiliana na mabadiliko hayo (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eGA ikiendelea kubaki kuwa wakala haiwezi kabisa kukabiliana na mwendelezo huo mkubwa wa teknolojia. Kwa hiyo, niiombe Serikali ilete hapa Muswada na kama Serikali hawakujibu hili jambo tunaweza kupambana. Kadri teknolojia inavyoongezea ndivyo uhalifu unavyoongezeka. Idadi ya watu inavyoongezeka na uhalifu wa mtandao unaongezeka, hatujui sasa eGA wametengewa kiasi gani cha kuwawezesha kukabiliana na hali ya teknolojia inavyobadilika; hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya ambapo tunawazidi kwa idadi ya watu ambao wanakwenda kwenye milioni 50 sasa hivi watumiaji wa intaneti ni asilimia 85, wana about watu milioni ishirini na tisa. Uganda ingawa wana watu milioni arobaini lakini wanakwenda kwenye asilimia 42, Tanzania bado tumebaki kwenye asilimia 38, jambo ambalo linatufanya; kwanza eGA yenyewe ipo kwenye Serikali, haipo mahali popote, haipo nationwide. Kwa hiyo, hiyo ni sababu ya kwamba kama hatukuwekeza mapema, kama hatukuwekeza leo, tutajuta kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimalize hili nije kwenye Usalama wa Taifa; na hapa ndipo ambapo mara zote huwa nalisemea suala la Usalama wa Taifa. Usalama wa Taifa nafikiri hawana Kitengo cha Economic Intelligence Unit. Mheshimiwa Rais anasema katika mkutano na wafanyabiashara kwamba kuna kiwanda cha sukari hewa kilichokuwa kikiagiza sukari, Usalama wa Taifa hawajui. Baada ya kiwanda kuagiza na kuleta ndipo habari zinapatikana, kabla hawajaleta Usalama wa Taifa haukuiarifu Serikali kwamba jambo hili halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaingia mikataba ambayo inaumiza nchi, why Usalama wa Taifa hauiambii Serikali? Au, je, kitengo hiki kwanza kipo na kama kipo kina uwezo gani? Je, teknolojia ipi ambayo inatumia? Mtuambie. Kama ni hivyo kimetengewa kiasi gani kwa ajili ya kuokoa uchumi wa nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapa mfano; kwenye tenda hizi za Serikali, mfano flow meter Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda kule kwenye flow meter bandarini, akasema kwamba hii flow meter itafanya kazi baada ya wiki mbili, flow meter haijafanya kazi hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais akasema flow meter hii lazima ifanye kazi, flow meter haikufanya kazi. Tenda ya kwanza imepelekwa, mtu mmoja kapeleka kampuni sita, kampuni sita zikawa saba wakati wa submission akaondoa kampuni zote tano ikabakia moja; Serikali haijui. Wafanyabiashara wale wa mafuta wanachezea, tenda ikafutwa ikawekwa tenda nyingine, consultant akapewa bilioni mbili tenda ikaenda ikafutwa, Usalama wa Taifa sasa hivi wao ndio wameichukua tenda ili wafanye wao, haiwezekani. Haiwezekani hivyo, lazima tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Usalama wa Taifa, Mheshimiwa Waziri, nishauri kwamba hiki kitengo kisishughulike na haya mambo madogo madogo huyu kaandika nini yule kaandika nini, mambo madogo, wasimamie maslahi mapana ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize na Usalama wa Taifa nije kwenye hoja yangu ya tatu ambayo ni Shirika la Elimu Kibaha. Shirika hili liliingia mikataba mitatu na ndiyo maana nasema Usalama wa Taifa wana matatizo. Katika mkataba wa kwanza ulikuwa na hekta 310 ambazo Serikali imepangisha Shirika la Elimu Kibaha kwenye ile ardhi kwa miaka 66 kwa shilingi milioni 120. Sasa ardhi inapangishwa kwa miaka 66 kwa milioni 120, kweli jamani? Hizo pia zilipwe cash ili dola isije ikapanda kwa sababu iko in terms of dollars. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkataba wa pili wa Kisarawe, kwa Mheshimiwa Waziri Jafo, pamoja na Kibamba, kuna hekta 110 umeingiwa pale na huyu Mkurugenzi kachukuliwa hatua kaondolewa tu; pamoja na yote haya aliyoyafanya lakini kachukuliwa kaondolewa kawekwa pembeni, hakuna hatua yoyote iliyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Usalama wa Taifa sasa itabidi tusaidie sisi; pale Tanzania Internal Logistics Center, Kurasini, pale Serikali imelipa fidia hela nyingi, nasahau kichwani kidogo, lakini baada ya kuwekeza hayo makubaliano na China mwisho wamewekwa kiwanda cha misumari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imelipa bilioni sitini, niziache, lakini sasa logic yangu ni hii kwamba why unawekeza kiwanda cha misumari badala ya kuwekeza ile hub ambayo Mheshimiwa Mwijage alituambia Afrika Mashariki ndiyo itakuwa hub kubwa; kwa sababu Usalama wa Taifa hawajui kwamba hizo pesa zilizotolewa na Serikali bilioni mia moja kwamba zinafanya kazi anapewa nani. Zilikwenda kwenye mifuko ya watu na sasa kwa taarifa nilizonazo wamewekeza kiwanda misumari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme kuhusu hili ambalo tunalizungumza, juu ya vijana wetu wa Pemba waliochukuliwa. Tuiombe Serikali ya Muungano, sisi ni wenzenu, tukae pamoja tuone hili jambo, ni jambo dogo sana, hakuna sababu ya jambo kama hili tukapiga kelele kila wakati kuwaambia jamani hivi na hivi, hebu tukae pamoja tuone tunalitatuaje; kwanza ni kupatikana hawa watoto.