Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa yale aliyotujalia.
Pili, nikupongeze wewe Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nakuomba unifikishie salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Spika pamoja na Wenyeviti ambao tumewachagua hivi karibuni kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutuongoza. Naungana na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ambayo kwa kweli, mimi nailinganisha na tangazo la vita, kwa namna ambavyo ilipangiliwa, lakini kwa namna ambavyo imetoa taswira ya kero za Watanzania na mikakati iliyopo ya namna ya kuzitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wenzangu wamesema mengi, lakini kama ninavyosema hili ni tangazo la vita kuhusu maadui zetu wale ambao walianza kutajwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ujinga, umasikini, maradhi, lakini sasa yakaongezeka pia ufisadi, rushwa, uzembe na mambo ambayo yanakwaza maendeleo yetu, sina budi na mimi kupita katika baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya kurasa 36 aliyoyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana kwa dhamira yake aliyoionesha na tayari ameshaanza kutenda kwa matendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili ni tangazo la vita kwa sababu Mheshimiwa Rais baada ya hotuba yake na hata kabla hajaunda Baraza la Mawaziri na kwa nafasi hii pia nawapongeza sana wateule Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wengine ambao wameteuliwa kumsaidia Mheshimiwa Rais; tayari Mheshimiwa Rais aliingia vitani, alishaanza kufanya kazi na akaanza kutumbua majipu kwa lugha ambayo imezoeleka sasa kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana, lakini kubwa tunazungumzia uwezeshaji wa huduma kwa Watanzania ambao sisi ni mojawapo ya wadau wakubwa sana katika kuwezesha hilo. Lakini tunapozungumzia kuimarisha huduma za Watanzania tunazungumzia uwezo wa makusanyo ya Serikali na matumizi mazuri ya fedha inayopatikana kutoka kwenye makusanyo yanayofanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya na sisi Watanzania wote, tukiwemo sisi Wabunge, ni dhahiri na jambo la msingi kumuunga mkono na kumpongeza ni hili la kuongeza mapato. Kwa muda mfupi tu ambao amekuwepo Ikulu, kama Kiongozi wetu Mkuu wa Taifa, Mheshimiwa Rais amefanikisha kuongeza mapato ya Serikali yanayokusanywa kwa mwezi kwa kiwango ambacho kimetangaziwa Watanzania, kwa mwezi uliopita tuliambiwa makusanyo yalikuwa shilingi trilioni 1.4! Si jambo dogo!
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba kwa mwendo huu dira ambayo inaonekana sasa, tunajenga uwezo wenyewe wa Taifa kwenda kusimamia kwa kiwango kikubwa sana kuwezesha utekelezaji wa huduma mbalimbali na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais pamoja na mambo mengine, ametuambia na Watanzania tunakiri kwa matendo anayoyafanya kwamba, anataka kuiona Tanzania ya Viwanda katika kipindi chake cha utumishi wa takribani miaka 10 ijayo, tunaamini itakuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda tunazungumzia mambo mengi, lakini mimi hapa ni mwakilishi wa Jimbo la Sengerema ambako ninawashukuru sana wananchi hawa walionituma, nikiunganisha nguvu na wawakilishi wa Majimbo mengine kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, tunapozungumzia viwanda kwa vyovyote vile tutashuka chini kuzungumzia viwanda vinavyotuhusu katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuungana na wenzangu ambao wamekuwa wakizungumzia umuhimu wa kuwa na viwanda katika Taifa letu na kwa Kanda ya Ziwa na hasa Mkoani Mwanza, Jimbo la Sengerema, viwanda ambavyo navizungumzia hapa ni vile ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza sana, viwanda vya pamba. Nazungumza hapa nikiwa namuona Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini nawaona pia, baadhi ya Mawaziri ambao wanahusika na mambo ambayo yanabeba uchumi wa Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nijielekeze zaidi kwenye maeneo haya, zao la pamba. Ninafahamu, Mheshimiwa Rais kwenye kampeni zake amelisisitiza sana, kufufua viwanda vya kuchambua pamba, lakini na viwanda vingine ambavyo vinategemea mazao ambayo tunayalima katika Kanda ile. Sisisitizi hili katika mtazamo wa Kikanda, nazungumzia yale ambayo wananchi wa Jimbo la Sengerema na Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanatarajia kuyaona yaki-reflect ile dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kujenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika eneo la viwanda, si pamba tu! La pili, ni hasa mazao ambayo yanatokana na samaki, mazao yanayotokana na mifugo na mazao yanayotokana na kilimo kwa ujumla. Katika hili, naungana na Mheshimiwa Rais, juzi alipokuwa Arusha alisema na mimi nawaomba Waheshimiwa Wabunge eneo hili tumsaidie sana Mheshimiwa Rais pengine kwa kutolea maelekezo au kupitia Azimio kwa kadri itakavyokuwa ama kupitia taratibu za Kamati zetu mbalimbali za Bunge, hili la kulishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kuendesha na kusimamia baadhi ya viwanda ambavyo tunaviona vinaweza kutumia rasilimali ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo la kuachia lipite hivi hivi, kwa sababu tunaliweza, tunaweza kulifanya, malighafi iliyopo hapa hapa nchini, nikadhani kwamba ni jambo la msingi Bunge lako Tukufu tujipange tuone namna ambavyo tunaweza kum-support Mheshimiwa Rais kutekeleza hiyo azma ya kuweza kuwa na viwanda ambavyo Wanajeshi kwa ujumla wao wanashiriki katika kusukuma hili eneo la viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuzungumzia linahusu sekta ya afya. Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, pale Sengerema tuna hospitali ya mission ambayo imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya, na kwa utaratibu wa sera ya afya hiyo hospitali ina hadhi ya Hospitali ya Rufaa ya Kimkoa. Hospitali ile tumekuwa na matatizo ya muda mrefu, nimeyazungumzia sana, lakini kikubwa ambacho ninakizungumzia sasa hivi ni kwamba, ruzuku inayopatikana kwenye hospitali ile haitoshelezi na miaka kadhaa tumekuwa tukiomba na hatujafanikiwa sana katika ombi letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahesabu ya ruzuku yanatokana na vitanda 150 vilivyokuwa vinatajwa kipindi kile wakati Mkataba wa Serikali na wa-missionary wenye hospitali hii ulivyofungwa, leo hii ina vitanda zaidi ya 300. Ninachoomba Mheshimiwa Waziri wa Afya, ombi letu liko Wizarani pale, ninakuomba sana ombi letu ulizingatie la kuongezewa ruzuku kutokana na vitanda ambavyo viko pale vinavyohudumia wananchi wa Jimbo na Kanda ile ya Sengerema.
Mheshimiwa Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais inayoshughulika na masuala ya TAMISEMI, Mji wa Sengerema mnaufahamu Jimbo la Sengerema, Wilaya ya Sengerema mnaifahamu, Mji wa Sengerema una hadhi ya Mji Mdogo, lakini kwa miaka minne iliyopita tulileta ombi letu na tulikidhi vigezo wa kuubadili ule mji ufikie Halmashauri ya Mji. Nafahamu Serikali imekuwa ikishughulikia jambo hili, nina wajibu wa kukumbushia hili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, kwamba tunamba ombi letu la kufanya Mamlaka Mji Mdogo wa Sengerema ifikie hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Simbachawene kuna lingine tuliongea na wewe la madawati, ombi langu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, sisi tulikuwa na Kikao cha RCC kule Mkoani, tumezungumza tukasema Wakuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya wamepewa malengo na Serikali ya kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi na sekondari, inakuwa na madawati ya kutosha. Sasa sisi Wilaya ya Sengerema tumebahatika kuwa na msitu wa Serikali shamba la miti linafahamika liko Jimbo la Buchosa na kwa sababu Wakuu wa Wilaya na Mkoa wamepewa mamlaka ya kuomba ridhaa ama kupata vibali kutoka Mkoani, nilikuwa naomba sana tusaidiane pamoja na Mheshimiwa Profesa Maghembe tupate hivyo vibali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aelezwe na Wakuu wa Wilaya ili sisi tutengeneze madawati kwa ajili ya kusaidia vijana wetu wanaosoma katika shule za sekondari na sule za msingi kwa Wilaya na Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Bunge hili linahitaji kutengeza action plan, namna ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kuitekeleza hotuba hii ina mambo mengi. Sisemi hili kwa maana ya kwamba hatuiamini Serikali yetu, lakini sisi kama wadau muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo, na naamini unalifahamu na mkakati naamini wa Kamati ya Uongozi upo, sisi ni muhimu sana tutengeneze action plan kwa masuala yanayozungumziwa hapa tuone ni namna gani tunajipanga kumsaidia Mheshimiwa Rais na moja ni hili ambalo tumeshalifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kamati ya Sheria Ndogo imeundwa ni Kamati mpya, mimi ni mmojawapo ya Wajumbe katika Kamati hiyo, ninaamini kwamba tutakuwa na jukumu la kupitia sheria zote ambazo ni kero kwa wananchi na hasa zinawezesha kutoa ushuru ambao ni kero kwa wananchi katika Halmashauri zote za nchi yetu. Lakini tukishakuwa na action plan katika Bunge hili tutaisaidia sana Serikali kuikumbusha kutekeleza yale ambayo yamesemwa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana, nakupongeza sana, naungana na wenzangu kwa mara nyingine tena kuunga mkono hoja, kuunga hotuba hii nzuri ambayo ni tangazo la vita kwa ajili ya kuondoa na kupunguza umasikini wa Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)