Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ufafanuzi mbele ya Bunge lako tukufu kuhusu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema ya kuwa hapa kwenye Bunge lako tukufu kujadili bajeti ya Serikali. Aidha, nachukua fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile namshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo wanayoitoa katika kuendeleza na kuboresha uhifadhi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe mwenyewe na Naibu Spika kwa kuliongoza vyema Bunge letu la Kumi na Moja katika Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu.

Aidha, kwa namna ya pekee napenda kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Nape Moses Nnauye na Makamu wake Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota na Waheshimiwa Wajumbe wote kwa namna ambavyo wameendelea kuishauri Wizara yetu ili kuimarisha sekta ya maliasili na utalii ifikie dira na dhima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba kuchukua nafasi hii kuishukuru sana familia yangu na watoto wangu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiniombea, wakinishauri na kunipa faraja katika kipindi chote ambacho nimekuwa nikifanya kazi hii kama Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kukishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi, Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mbozi kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakinisaidia katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Vwawa kwa muda mrefu wamenikosa na wamekuwa hawana muda wa kutosha wa kukaa na mimi, lakini naomba niwaambie kwamba nipo pamoja nao na ninaendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa na wao waendelee kutekeleza majukumu yale mpaka hapo Mungu atakapopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika kuboresha bajeti yetu hii. Kwa kweli niseme Waheshimiwa Wabunge wametoa michango mizuri sana. Michango yao inafaa sana na kwa kweli kama tutaweza kuitumia michango yote hii ni imani yangu kabisa tutaboresha uhifadhi na tutaboresha utalii wetu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda ni kidogo sana, hatutaweza kutoa ufafanuzi wa hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Naomba nichukue nafasi hii kutoa ufafanuzi wa hoja chache ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ufafanuzi mzuri ambao ameutoa juu ya migongano, sheria na kama sheria zilivunjwa na kadhalika. Pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria kwa jinsi ambavyo wamefafanua hoja mbalimbali, kwa kweli tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na sekta ya uwindaji wa kitalii; kumekuwepo na hoja nyingi sana zinazohusu juu ya uwindaji wa kitalii. Wapo Waheshimiwa Wabunge ambao kwa undani kabisa na kwa dhati wamechangia vizuri sana na wengine wakasema hii biashara sasa imedorora ni kwa sababu labda hatua ambazo zimechukuliwa hazikuzingatia sheria. Naomba niseme kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, biashara ya uwindaji wa kitalii inaongozwa na sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo Serikali imeiweka na hiyo ndiyo inayotu-guide namna ya kuendesha uwindaji wa kitalii nchini. Katika Sheria Namba 5 ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2015 zinatoa namna ya uwindaji wa kitalu utakavyoendeshwa kwenye nchi hii, namna vitalu vitakavyogawanywa na vitalu vingapi vitakuwa ni vya wenyeji, labda ni makampuni mangapi ya nje yatakuwepo? Kwa hiyo, sheria ile inafafanua vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na hoja kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2017 Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilibadili utaratibu wa kugawa vitalu kutoka kwenye ule utaratibu wa zamani wa kiutawala (administrative allocation) kuelekea kwenye mfumo mpya wa mnada. Kwa nini wakasema kwamba kumekuwa na ukiukaji wa sheria?

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba kwanza ni kweli kabisa makampuni ya uwindaji yalipewa kibali cha kufanya uwindaji kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2018 mpaka mwaka 2022. Wakati wanapewa hiyo mikataba ya miaka mitano, kwenye barua kulikuwa na maelekezo mazuri kabisa ambayo yalisema kwamba kufuatia mageuzi yanaoendelea ndani ya Wizara katika kuimarisha Sekta ya Uwindaji wa Kitalii, Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii anaweza kubadilisha wakati wowote na imeandikwa na kufafanuliwa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutafakari namna sekta ya utalii ambavyo imekuwa ikiendeshwa nchini, tuliridhika kabisa kwamba bado kuna upungufu ambao upo ambao ni lazima tuurekebishe ili uendane na hali halisi iliyopo kwa sasa. Moja ya sababu iliyowekwa katika ile barua ya mkataba wa awali, ilikuwa ni kwamba kwa sasa hivi vitalu vya uwindaji viko chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), lakini TAWA ndiyo inaanzishwa na kwa sababu ndiyo inaanzishwa, itakuja sasa na utaratibu mpya wa namna ya kusimamia hivyo vitalu, ndiyo maana kulikuwa na hicho kigezo kwenye ile barua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuangalia kile kigezo ndiyo maana tukaamua kwamba sasa hebu tusitishe ili tuje na utaratibu mzuri kabisa ambao utakuwa na manufaa makubwa mawili; kwanza utaongeza mapato ya Serikali kwa sababu sasa tutafanya kwa mnada. Kwa hiyo, badala ya vile vitalu vingine kuuzwa labda dola 5,000, dola 15,000 na dola 30,000; vile vya daraja la kwanza kuuzwa dola 60,000, sasa unaweza ukakuta baadhi ya vitalu vikauzwa mpaka hata dola 300,000. Kwa hiyo, tukaona Serikali itapata mapato makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tukasema sasa lazima hili tulifanyie marekebisho ili liendane na kwanza na tamko ambalo lilikuwepo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba vitalu vya uwindaji vitaendeshwa kwa njia ya uwazi na kwa njia ya mnada ili kusudi kusiwe na milolongo ya rushwa na nini, watu waamue wenyewe na wapange bei wenyewe. Basi tukaona kwamba hili ni la msingi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusitisha, wadau wa uwindaji walitoa malalamiko yao wakatuambia hii sasa mta- frustrate industry, na sisi tukaa tukakubaliana, tukasema kweli kuna hoja. Walipotueleza tukaelewa na ndiyo maana tukasema sasa wakati tunakwenda badala ya kwamba tusitishe mwezi wa kumi ule halafu mwezi wa kwanza tuwe tumetoa, tutashindwa. Ndiyo maana tukaamua kufanya extension ya ule muda wa kwanza, tukaongeza miaka miwili wakati haya mabadiliko sasa yanaendelea kufanyika. Ndiyo maana wamepewa tena wameongezewa miaka miwili. Wameongezewa katika ile baada mitano baada ya kumalizika, wameongezewa miwili. Katika kipindi hiki, Serikali sasa itakuja na utaratibu mpya wa namna ya tutakavyoendeshwa kwa minada.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na hoja kwamba baada ya kutangaza hivi, kuna matatizo yamejitokeza; wakasema vitalu vingi vimerudishwa. Naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sekta ya uwindaji wa kitalii sasa hivi inakabiliwa na changamoto nyingi sana hapa, siyo tu kwa Tanzania bali kwa dunia nzima. Kuna mambo mengi yanaendelea katika hili. Kwanza wawindaji wa kitalii ni kweli kabisa ni wale wale ambao wapo nchi zote, ukiwa-frustrate hapa watahamia kwingine. Kwa hiyo, ni kweli lazima tuwalinde vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna kampeni zinaendelea duniani, kuna watu wanaosema wanalinda haki za wanyamapori. Hawa wamekuwa wakifanya kampeni kila mahali kwamba kuwinda wanyama ni dhambi kubwa. Hizo kampeni za anti-hunting zinaendelea. Makampuni mengi duniani sasa hivi yanafanya kampeni. Kwa hiyo, hiyo kwa kiwango fulani imeathiri kushuka kwa biashara ya uwindaji wa kitalii. Hiyo ni sababu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu ya pili, baadhi ya nchi ambazo ndiyo wadau wakubwa wa uwindaji wa kitalii zimepiga marufuku baadhi ya trophy ambazo zilikuwa zinaenda ikiwemo Marekani na nchi za Ulaya (European Union) zimepiga marufuku na baadhi ya nchi juzi juzi tumesikia hata China wamepiga marufuku. Kupiga marufuku kule kutaathiri moja kwa moja biashara ya uwindaji wa kitalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu ya tatu, sheria yetu ile ilikuwa inasema asilimia 85 lazima ziwe ni kampuni za wazawa na lengo lilikuwa ni kuwasaidia wazawa ili waweze kumiliki hizi kampuni na wapate mapato makubwa kusudi wageni wawe na asilimia 15 tu ya makampuni. Ni kweli ilikuwa ni sheria nzuri na wazawa wengi walichukua, walipata hii, lakini kutokana na changamoto za biashara hii, kampuni nyingi za kizawa zimeshindwa kufanya hii biashara, ndiyo maana zikafikia hatua ya kuanza kuzirudisha.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mpaka sasa hivi ni vitalu 81 vimesharudishwa, vimekosa wawekezaji. Huko nyuma baadhi ya makampuni yalikuwa yanunue hivi vitalu halafu tena yanavikodisha kwa Wazungu. Sasa hivi hiyo biashara haipo. Na sisi tunataka kwamba wale wale wanaokodi, wenyewe wazingatie sheria, sera unaendesha wewe mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo, ndiyo maana sasa kumekuwa na kushuka kwa hii biashara ya wenzetu. Kwa hiyo, ndiyo maana vitalu vingi vimerudishwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulichokifanya, sasa hivi tunaendelea kuuandaa utaratibu, mojawapo, vitalu hivi 81 vilivyorudishwa navyo pia tutaviingiza kwenye huu mnada ambao utakuja ambao tutautumia kusudi watu waweze kufanya hivyo. Pia katika hilo lazima tuendane na sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na hoja kwamba baada ya wale wawekezaji waliokuwa kwenye vile vitalu walipoondoka kuna changamoto zimejitokeza. Watu wakasema vitalu vimebaki bila ulinzi, bila nini.

Mheshimiwa Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba wale wawekezaji wakati wanaendesha au wanamiliki vile vitalu na Serikali pia tulikuwa bado tuna watumishi wetu wanaoshirikiana na zile kampuni za ulinzi. Baada ya wale kuondoka, sasa hivi tunabaki sisi wenyewe tunaendelea kulinda.

Mheshimiwa Spika, pia katika kile kikosi maalum cha Kitaifa ambacho kilianzishwa, yaani kile ambacho tumekuwa tukizunguka nchi nzima, wamekuwa wakipambana na uwindaji haramu, basi kampeni hiyo imefanyika vizuri na ulinzi umefanywa vizuri hasa kwa kutumia intelijensia. Sasa hivi matukio ya ujangili yamepungua kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo, vile vitalu vingi vipo salama na Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inavilinda hivyo vyote ili viwe na manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunadhani hata baadhi ya yale mapori ya akiba, Mheshimiwa Waziri atayasemea, tunafikiria yapandishwe hadhi kama baadhi ya Waheshimiwa walivyosema, yaende kufikiwa kuwa ni Hifadhi za Taifa, yakifika hapo tutakuwa tumefikia hatua nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine kutokana na changamoto hizi ambazo zinaendelea duniani, tunataka tuanze kuipunguza hii biashara ya uwindaji wa kitalii, tuanze kwenda kwenye utalii wa picha zaidi. Utalii wa picha zaidi utaleta manufaa makubwa na utalinda hata hizo haki za wanyamapori kama ambavyo watu wengine wamekuwa wakisema.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana katika baadhi ya maeneo na katika mradi ambao tunakuja nao ule wa kuinua utalii wa Kusini (Regrow) ambao unahusu mbuga ya Selous, Mikumi, Udzungwa na Ruaha ambao tunaanza nao, kwa asilimia kubwa tunataka tuhakikishe hata kule Selous, Kanda ya Kaskazini tulete utalii wa picha badala ya utalii wa uwindaji kusudi tuweze kupata mapato makubwa. Ninaamini kabisa hiyo itasaidia sana katika kuleta hayo manufaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka tu nitoe ufafanuzi huo kwamba yale ambayo tuliyafanya, tuliyafanya kwa mujibu wa sheria na kwa sababu barua, au mkataba wenyewe ulikuwa una-provide ndiyo maana hayo yalifanyika.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo ningependa kutoa ufafanuzi kidogo ni kuhusu sekta ndogo ya misitu. Waheshimiwa Wabunge, wamezungumzia mambo mengi sana kuhusiana na sekta ya misitu na mambo mengi. Kwa kweli nawashukuru sana na niwapongeze. Ni ukweli usiofichika kwamba sekta ya misitu ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi hii. Misitu inachangia asilimia nne.

Mheshimiwa Spika, hebu tuangalie jinsi misitu yetu inavyosimamiwa, kuna Serikali Kuu; Serikali Kuu ina hifadhi 455, lakini kuna nyingine ziko chini ya Halmashauri kama 167; lakini Serikali za Vijiji zina hifadhi 1,200. Sasa unapokuwa na hifadhi ambazo ziko scattered, zina mamlaka tofauti, lazima kuwe na changamoto. Ndiyo maana tukaamua sasa kupitia upya sera ya misitu ili hii sera ikipitiwa upya, ikihuishwa, tulete sasa sheria ambayo itahakikisha kwamba hii sekta ya misitu inatoa mchango mkubwa sana katika uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo basi, ndiyo maana kuna mapendekezo, hata Kamati nafikiri imependekeza kwamba tuwe na mamlaka moja. Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana kwa hiyo hoja. Tuwe na mamlaka ya kusimamia misitu yote Tanzania. Hii itatusaidia sana. Misitu ndiyo uhai, bila misitu hakuna maji, bila misitu hakuna maisha na kwenye sekta hiyo ndiyo tuna nyuki, tuna asali, tuna vitu vingine vingi tu.

Mheshimiwa Spika, naomba niliambie Bunge, sasa hivi kwenye sekta ya nyuki hatujaiendeleza, lakini tunaamini tutaiendeleza vizuri sana. Mkitupa fedha tutaiendeleza sekta hii vizuri. Kwa sababu kwenye nyuki pale, najua hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawajui, nyuki wanatoa maziwa ambayo ni mazuri sana. Pia kwenye nyuki pale tutapata nta, asali na mambo mengi sana, soko ni kubwa. Uzalishaji wa asali ukiongezeka, nta ikiongezeka, maziwa yakiongezeka na baadhi ya kemikali ambazo zinatokana na mazao haya, kutasaidia sana katika kuleta fedha kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine lililojitokeza katika upande wa misitu ni matumizi ya mkaa. Waheshimiwa Wabunge wengi wamelalamika kwamba kweli sijui kuna sehemu wanakamatwa, mikaa inazuiwa, mikaa imefanya nini; naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sisi tulichokifanya, hatujazuia matumizi ya mkaa. Tunasema kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia mkaa, basi lazima tuwe na utaratibu mzuri wa maeneo ya upatikanaji wa mkaa. Tukiruhusu kila mahali kila mtu anauza mkaa, kila mtu anavuna, basi hiyo inakuwa ni changamoto katika uhifadhi wa misitu yetu.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa tunasema kwamba tunataka wananchi wapewe elimu, wawe na meko yanayotumia mkaa kidogo. Pia tuwe na centres ambazo zina vibali wamelipia tozo zinazostahili, tuwe tunajua kwamba wanauza mkaa. Tatu, tuje na elimu. Sasa hivi tumefanya utafiti tumegundua kuna baadhi ya miti ambayo tutahamasisha ipandwe kila mahali ambayo inachukua kati ya miaka mitatu na minne, inafaa sana kwenye kuni na inafaa sana katika uzalishaji wa mikaa. Kwa hiyo, hiyo misitu nayo tutaisambaza, elimu hiyo tutaitoa ili wananchi wa nchi hii wahamasishwe namna ya matumizi bora ya hizo kuni na mikaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala ambalo limejitokeza kwamba boda boda wanakamatwa kila mahali wakiwa wamebeba mkaa, magari yanakamatwa; nataka niseme hivi, kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, bodaboda hawaruhusiwi kubeba mkaa. Hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria, yale hawaruhusiwi kabisa! Kwa hiyo, tunachosema, magari yaliyoruhusiwa yenye vibali ndiyo hayo yaweze kuruhusiwa kusambaza mkaa katika vituo mbalimbali na wananchi waelekezwe wapi mkaa halali unapatikana ili wale wanaochukua kwa rejareja wachukue katika hayo maeneo.

Mheshimiwa Spika, naamini kwamba hilo litapunguza changamoto ambazo zipo katika suala hili la matumizi ya mkaa. Ni muhimu sana wananchi wakaelimishwa matumizi ya mkaa vizuri, tuwe na majiko mazuri, tuwe na namna ya kuendeleza hii sekta, itatusaidia sana katika maisha yetu na itatoa mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, viwanda vingi vinavyotokana na misitu; sasa hivi tuna viwanda vingi vinatokana na mazao ya misitu. Ni imani yangu kabisa kwamba hii Sekta Ndogo ya Misitu lazima tuiimarishe ili vile viwanda vyote vitoe mchango mkubwa kwa sababu Sera yetu ya Taifa inataka tuwe ni nchi ya viwanda. Sasa viwanda vinavyotokana na mazao ya misitu lazima viimarishwe na vihakikishe kwamba kwa kweli vinatoa mchango ule unaohitajika.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba baadhi ya watumishi katika maeneo ya hifadhi wamekuwa wakitoa rushwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)