Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, kuhusu sekta ya utalii nchini. Sote tunatambua kuwa masuala ya sekta ya utalii si masuala ya Muungano, hivyo kujumuisha idadi ya watalii wanaoingia Zanzibar kama sehemu ya Muungano kwa mujibu wa randama ndiko kunakozua mtanziko. Serikali ituambie ni lini hasa imeamua mambo ya utalii kuwa sehemu ya Muungano kama ambavyo Serikali imekuwa ikijinasibu na idadi ya watalii inayojumuisha Tanzania Bara na Tanzania Visiwani?

Mheshimiwa Spika, ni vizuri Serikali ikaweka wazi dhamira yake ya kujumuisha idadi ya watalii ikiwemo ya Zanzibar. Vilevile pamoja na mazingira mazuri ya kibiashara na faida zake, sekta hii ya utalii inaweza kukua pale ambapo nchi inakuwa katika hali ya amani na utulivu. Amani na utulivu huja pale ambao mamlaka zinazingatia haki za kiraia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la uwindaji, ni nini hasa kinachosababisha kushuka kwa mapato katika sekta hii tofauti na miaka ya nyuma? Pia Serikali imeshindwa kudhibiti uwindaji haramu na ujangili. Biashara ya uwindaji inaonekana kutafsiriwa tofauti miongoni mwa wananchi walio wengi. Serikali imeshindwa kutoa ajira za kutosha kwa walinzi wa wanyamapori, kushindwa kulinda mazalia ya wanyamapori, kushindwa kufanya tafiti za mara kwa mara juu ya ongezeko na upungufu wa wanyama na viumbe hai, wananchi kutoshirikishwa juu ya kulinda wanyama wetu na badala yake wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi wamechukuliwa kama maadui au wanyama. Hii yote ni kutokana na kutowapa elimu na mafunzo ya ulinzi shirikishi katika suala zima la kulinda rasilimali hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kudhoofika kwa biashara ya uwindaji na athari zake, tukumbuke kuwa biashara ya uwindaji ndiyo biashara inayoingizia Serikali fedha nyingi zaidi za kigeni kwenye sekta hii ya utalii ni jambo la kushangaza Serikali imefuta vibali kinyume cha Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo inaeleza wazi taratibu na makosa ambayo yanaweza kusababisha kampuni kufutiwa vibali.

Ikiwa ni pamoja na kushindwa kutimiza masharti ya leseni, endapo kampuni imepatikana na hatia au kushindwa kulipa ada na tozo mbalimbali na si kufuta vibali kwa ghafla pasipo kufuata sheria na taratibu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikikiuka utaratibu mara kadhaa jambo ambalo linaathiri mazingira ya kibiashara na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wawekezaji wa ndani na wale wa kigeni.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ushuru wa maendeleo ya utalii, kutokupeleka fedha katika akaunti ya tozo ya maendeleo ya utalii ina athari za moja kwa moja katika utendaji kazi ndani ya Wizara. Mpaka sasa Wizara hii imekuwa ikitegemea zaidi wahisani na hivyo kuendelea kukwamisha jitihada za Wizara. Kutokuhamisha fedha kwa wakati maana yake ni kuifanya Wizara kushindwa kutekeleza majukumu yake. Pia ndiko hasa kunaporuhusu matumizi mabaya ya fedha kuanza kujipenyeza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu migogoro sugu baina ya Serikali na wananchi wanaoishi kando ya hifadhi za wanyamapori, kumekuwa na tatizo sugu la migogoro baina ya Serikali na wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi ya wanyama pori kwa muda mrefu sasa. Pamoja na jitihada mbalimbali za kuizungumzia na kushauri hatua stahiki za kuitatua bado hali inaonesha migogoro hii imekuwa na nguvu kubwa kuliko uwezo wa Serikali wa kuitatua.

Mheshimiwa Spika, vilevile migogoro hii imedumu kwa muda mrefu ambapo imegharimu maisha ya wananchi wengi. Tumepoteza wanyama ambao ndio fahari yetu na chanzo cha mapato. Migogoro hii imesababisha kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na wanyama pori, mifugo na hivyo kuathiri afya za wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini. Kwa baadhi ya maeneo migogoro imekuwa ni ya muda mrefu kutokana na tuhuma kuwa kuna baadhi ya mapori ya akiba na hifadhi kupanua mipaka yake bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Idara ya Misitu na Nyuki, sekta ya ufugaji wa nyuki imekuwa haifanyi vizuri kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutopewa kipaumbele ipasavyo. Miradi mingi inayoanzishwa na Serikali imekuwa haifanyi vizuri na mingi imeshindwa kuendelea kutokana na kutokutunza vizuri na kukosa ufuatiliaji wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uharibifu wa mazingira katika hifadhi za misitu, suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu sana kwa ikolojia ya misitu, bahari pamoja na mbuga zetu kwani uwepo wa maji, hali nzuri ya hewa na udongo vinapelekea mimea na wanyama kuzaliana na kuwa katika hali bora zaidi. Sote tunatambua umuhimu wa kutunza ikolojia na madhara makubwa yanayojitokeza nchini kwa sasa kutokana na kuharibu wa ikolojia na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Pia kukauka kwa vyanzo vya maji, kuharibika kwa ardhi, na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua madhara haya makubwa kwa binadamu na mimea Serikali iliamua kuridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa ya kulinda mazingira. Pamoja na kuweka sheria na sera za kulinda mazingira nchini ni vyema Serikali ikaamua kufanya mkakati wa tathmini ya mazingira kwa miaka mingi ijayo. Bado nchi yetu ina namna nyingi ya kuzalisha umeme katika maeneo mengi ambayo athari zake za mazingira si kubwa kama itavyotokea kwenye chanzo cha Mto Rufiji. Vilevile Pori la Akiba la Selous limekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya wananchi na ajira. Mpaka sasa pori hili limeorodheshwa katika maliasili zilizo, hatarini kupotea. Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Urithi wa Dunia kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya tembo na kuharibika kwa mapitio ya wanyama. Vilevile kuna maeneo mengi ambayo wananchi wamefukuzwa na wengine kuhamishwa kutokana na kulinda ikolojia ya maeneo hayo.