Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nashukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi nitoe mchango katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara hii kwa hotuba yao mahiri na ni nzuri yenye kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nawapongeza sana Serikali kwa kuweka mikakati mizuri ya kutupeleka kwenye kujenga uchumi wa viwanda. Katika Wizara yetu yako mambo mawili ya msingi ambayo nadhani katika Wizara hii ni muhimu sana tukayafafanua vizuri kama mikakati ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na Waheshimiwa Wabunge, lipo suala la kuzalisha umeme wa kutosha, wa uhakika na unaotabirika. Njia pekee ni kuwa na umeme mchanganyiko. Kuwa na umeme mchanganyiko maana yake utumie rasilimali zote ulizonazo, ukusanye nguvu zote upate umeme mwingi, wa uhakika na wenye gharama nafuu ili kujenga uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya Serikali hadi sasa ni kuzalisha umeme upatao megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 mwaka 2025. Sasa huwezi kuupata umeme huu kwa chanzo kimoja. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema kwamba tunayo rasilimali nzuri sana ya gesi asilia kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa katika umeme tulionao, kama malengo yetu ni kupata megawati 5,000 mwaka 2020, hivi sasa tuna jumla ya megawati 1,513. Kwa hiyo, bado safari ni ndefu. Kwa hiyo, lazima tuzalishe umeme wa kutosha ili kujenga uchumi wa viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika umeme huo hadi sasa, tuna takribani megawati 783 zinazotokana na rasilimali ya gesi asilia, lakini umeme wa maji ni megawati 567.7. Kwa hiyo, bado tupo mbali. Umeme wa mwisho wa kuzalishwa katika miradi ya maji ni huu mradi wa Kihansi wa mwaka 2000. Mradi kabla ya hapo ulikuwa ni umeme wa Kidatu wa mwaka 1975 na 1980. Kwa hiyo, ni miaka mingi tangu tumezalisha umeme wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika rasilimali ya gesi mwaka 2008 tulizalisha megawati 102 Ubungo I na mwaka 2012 tulizalisha megawati 129, mwaka 2016 megawati 150 Kinyerezi I na mwezi Aprili tumezalisha megawati 168 za gesi asilia. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuzalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika gesi asilia bado kuna miradi mikubwa mitano ijayo. Mradi wa kwanza ni wa Somanga – Fungu wa megawati 330 tunaoanza kuzalisha na kuujenga mwaka huu wa fedha na mradi mwingine wa Mtwara megawati 300 za gesi asilia. Mradi mwingine utakaoanza mwakani ni mradi wa Kinyerezi III, megawati 300 na Kinyerezi II megawati 300 na hatimaye Kinyerezi IV megawati 330. Hayo malengo lazima tuyatimize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa nyingine ya kutumia rasilimali ya gesi ni pamoja na matumizi ya viwandani. Tuna takribani trilioni 4.6 zitakazotumika kwa ajili ya kutengeneza viwanda vya mbolea na petrochemicals. Kwa hiyo, hayo ni matumizi ya gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kutumia rasilimali hiyo katika kusambaza mbolea lakini pia kwenye ujenzi wa viwanda vinavyoendelea ambavyo matumizi yake ni trilioni 3.6. Hayo ni matumizi ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna mpango wa kusambaza gesi majumbani na katika magari ambayo itatumika trilioni 1.2 kama gesi asilia ya kutumia kwenye matumizi yetu nyumbani na bado trilioni 1.2 itatumika kwa ajili ya viwanda vya vyuma. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema kwamba matumizi ya gesi asilia bado ni mengi kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kusindika gesi kwenda kwenye kimiminika na matumizi hayo kila mwaka kiwanda hicho kitatumia tani milioni 10 kwa ajili ya kujenga kiwanda hicho cha gesi asilia. Kwa hiyo, manufaa ya gesi asilia bado ni mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii wananchi wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine bado tutanufaika na hii rasilimali ya matumizi ya gesi asilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, potential tuliyonayo, tunavyo vyanzo vingi. Hivi sasa potential tuliyonayo kwa upande wa kuzalisha umeme wa maji, tukizitumia vizuri, tunayo potential ya kuzalisha megawati 4,700 ya maji ambayo hatujaitumia. Hivi sasa tumetumia asilimia 12 tu. Wakati kwenye gesi, niweke sahihisho kidogo, jana nilisikia imesemwa kwamba ni 5%, siyo kweli, tumeshafika asilimia 10 ya matumizi ya gesi asilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya gesi ambayo nimeisema, ukiangalia kwenye matumizi ya maji, kati ya megawati 4,700 tumetumia megawati 567 tu. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuzalisha umeme wa maji ili rasilimali ya maji tuliyonayo ambayo ni kubwa ilete manufaa makubwa kwa ujenzi wa uchumi wa viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kusema mradi wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji na wala siyo Stiegler’s Gorge; maporomoko ya Mto Rufiji ni muhimu sana tukiujenga sasa kuliko kuuacha. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama malengo yetu ni kufikia megawati 5,000 mwaka 2020 na 10,000 mwaka 2025, umeme unaokwenda kutukomboa kwa mkupuo, kwa mchapuo, mara moja, ni megawati 2,100 wa maji ya maporomoko ya Mto Rufiji. Kwa hiyo, naomba sana Waheshimiwa Wabunge kwamba tuunge mkono juhudi za Serikali ili kusudi tuweze kupata umeme huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vyanzo vingine ambavyo nazungumza mbali na kusema Mradi wa Mto Rufiji, ipo miradi ya geothermal na makaa ya mawe. Hivi sasa tuna potential ya makaa ya mawe tani bilioni tano hatujawahi kuzitumia. Tunayotumia sasa ambayo ni proven ni asilimia
25. Kwa hiyo, ni vema sana Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhamasisha energy mix katika kujenga uchumi wa viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna potential ya geothermal ambayo inafikia pia megawati 5,000, hatujaanza kuitumia. Ni vizuri sana Waheshimiwa Wabunge tukiunga mkono juhudi za Serikali kutumia umeme mchanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema Mradi wa Maporomoko ya Mto Rufiji ni muhimu sana kwa kuzalisha umeme lakini pia kwa utalii pamoja na shughuli za umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kulizungumza ni kupata umeme wa uhakika na unaosafirishwa. Ni kweli kabisa tunazungumza hapa suala la umeme kukatika. Kwa sasa umeme tulionao, hali halisi ya umeme inaendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa, changamoto tuliyonayo kidogo ni katika miundombinu. Lakini kama Serikali tumejipanga na tuna miradi mahususi ya kufanya ukarabati wa miundombinu ili kuhakikisha umeme tulionao haukatiki. Hiyo inaenda sambamba na kuwa na umeme wa kutosha ikiwemo na miradi mikubwa niliyoitaja.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nziungumze kidogo kuhusu juhudi za Serikali ya kusambaza umeme vijijini kama juhudi za kuunga mkono ujenzi wa viwanda. Ni dhamira ya Serikali kwamba ni lazima sasa viwanda tunavyovizungumza vianze kujengwa kuanzia vijijini na wala siyo mijini tu. Ndiyo maana kama Serikali tunapeleka umeme katika vijiji vyote mwaka 2020/2021. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika nchi yetu, kati ya vijiji 12,268 ni takribani vijiji 4,878 vimeshapelekewa umeme na vijiji vingine 500 vipo katika kuunganishwa umeme. Ni matumaini yetu kwamba mara baada ya miradi hii ya umeme vijijini kukamilika viwanda sasa vitarejea kuanzia vijiji. Ni matumaini yetu mihogo inazalishwa vijijini, hivyo tukiwapelekea umeme vijijini wananchi wote, viwanda vya kusaga na kukoboa unga vitaanzia vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono juhudi za Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kuhamasisha viwanda, uchumi wa kati ili kujenga uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, nishati ndiyo mhimili pekee tunapokwenda kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.