Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. KABWE R. Z. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu kufungamanisha viwanda na kilimo. Kufunganisha viwanda na kilimo kungeepusha uhaba wa bei kubwa ya sukari nchini. Serikali ingesikiliza ushauri mwaka 2016, nchi isingesumbuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa mara ya tatu tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Bunge linajadili na baadae kuidhinisha fedha kwa ajili ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka 2018/2019.

Kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Wizara hii ndiyo Wizara mama inayotoa taswira ya kufeli au kufaulu kwa Serikali hii. Maana ahadi ya msingi ya Serikali hii kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ilikuwa ni kuwa itajikita kujenga Tanzania ya viwanda huku lengo kuu likielezwa kuwa ni kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa kati unaongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Bunge tunao wajibu wa kuhakikisha tunasaidia Serikali ili itimize ahadi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma hiyo ya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda ni njema na ni yetu sote, kwa nafasi zetu tunasaidia kuifikia azma hiyo. Tulipitisha hapa Bungeni Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Serikali (FYDP2), kwa miaka ya 2016/2017 - 2020/2021 na kwa hiyo ni mpango wa nchi. Hivyo sote kwa pamoja tunafanya kazi ya kuhakikisha tunafikia malengo ya mpango husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa upande wa upinzani tuna dhima kubwa zaidi ya Wabunge kutoka Chama Tawala. Tunao wajibu wa kukosoa pale ambapo tunaona walio kwenye Serikali wanakosea, kupendekeza sera bora zaidi za kutumia ili kufikia lengo (Tanzania ya viwanda) na kushauri mbinu nzuri zaidi za utekelezaji wa sera hizo. Naomba nitumie nafasi hii kukumbusha Bunge kuwa sisi upinzani tulitimiza wajibu wetu, ni hivyo tu Serikali haikusikiliza ushauri wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana mengi ya matatizo ya karibuni ya Wizara hii, hasa kwenye suala la uhaba na bei kubwa ya bidhaa za mafuta ya kula na sukari, si mapya, ni zao la uongozi mbovu wa CCM. Serikali ya Awamu ya Tano imerithi, imeendeleza na pia imezalisha zaidi matatizo ya uhaba na bei kubwa ya sukari na mafuta ya kula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 wakati wa bajeti ya Wizara ya 2016/2017 Wabunge wa Upinzani tulishauri njia za kutatua matatizo hayo. Ushauri wetu haukusikilizwa, tunakumbusha tena leo ili Serikali itatue matatizo ambayo ilipaswa iyatatue mwaka 2016. Mchango wangu wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ulijikita kwenye kuishauri Serikali juu ya umuhimu wa kufungamanisha sekta ya viwanda pamoja na kilimo ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu na kuhakikisha kuwa aina ya viwanda vyetu tunavyovianzisha nchini ni vile ambavyo vitategemea kwa kiasi kikubwa malighafi kutoka ndani ya nchi yetu hasa bidhaa za kilimo, ikiwemo sukari na mafuta ya kula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa tatizo la sukari nchini, ukurasa wa 140 wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda ya 2016/2017 unaeleza malengo ya Serikali kwenye sekta hii ya viwanda. Mambo tisa ya msingi yalipaswa kutekelezwa na Serikali ili kufikia azma ya kuwa na viwanda na katika mambo hayo tisa, hakukuwa na mpango mkakati wa kufungamanisha uzalishaji viwanda na bidhaa za kilimo zenye soko zaidi nchini (sukari na mafuta ya kula).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kurasa za 25 na 44 za hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo na Uvuvi kwa mwaka 2016/2017 zinaeleza juu ya mikakati ya kukabiliana na uhaba wa sukari nchini. Kiambatisho namba sita cha hotuba hiyo kilieleza kwa kina changamoto nzima ya sukari na miradi inayopaswa kutekelezwa ili kumaliza kabisa suala la uhaba na kupanda kwa bei ya sukari nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejumlisha miradi ile kutoka kila kona ya nchi na nimekuta ni takribani hekta 300,000 za kulima miwa. Kwa hesabu ya chini ya wastani wa kuzalisha sukari kwa kila hekta, miradi ile kama ingetekelezwa Tanzania ingeweza kuzalisha tani milioni 1.5 za sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoa sukari ya kutumia nchini, ziada ambayo ingeuzwa nje ingeweza kuliingizia Taifa fedha za kigeni USD milioni 500, sawa na asilimia 30 ya malengo ya mpango wa maendeleo kwa sekta ya viwanda wa kupata mapato ya fedha za kigeni kiasi cha USD bilioni tatu. Hapo ni bila kutazama kiwango cha ajira zitakazozalishwa, ukuaji wa biashara kwenye sekta nyingine, umeme na kadhalika (multiplier effect).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ile ya mwaka 2016/2017 hakukuwa kabisa na mafungamanisho kati ya ulimaji wa hekta hizo 300,000 za miwa na uzalishaji wa tani milioni 1.5 za sukari. Maana Wizara ya Viwanda na Biashara hata haikujua juu ya mkakati huo wa kupunguza uhaba wa sukari wa Wizara ya Kilimo. Wizara mbili zilizo ndani ya Serikali moja hazikuwa zikisomana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri mambo matatu kama ifuatavyo:-

(i) Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Kilimo kwa mwaka 2016/2017 iondolewe na ikapitiwe upya ili isomane na bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka husika. Tuliomba Wizara mbili ziwianishe na kuoanisha mipango yao kwa lengo la kuratibu ulimaji wa miwa na uanzishaji wa viwanda vya sukari vya kutumia miwa ile.

Serikali haikusikiliza, Rais akatoa tu matamko ya zuio la sukari kutoka nje wakati hakukuwa na mpango wa Taifa wa namna ya kufidia nakisi ya sukari itokanayo na uzalishaji mdogo wa bidhaa hiyo nchini. Matamko ya zuio ya Rais yaliishia kuleta uhaba wa sukari na kupandisha bei kutoka shilingi 1,800 mpaka shilingi 6,000 katika maeneo mbalimbali nchini na tangu hapo bei ya sukari haijashuka tena, imebaki kuwa shilingi 3,000 kwa kilo.

(ii) Kwenye sukari kuna suala la low hanging fruits, kila mwaka miwa yenye uwezo wa kuzalisha tani 50,000 ya sukari huoza huko Kilombero na Mtibwa. Mkoani Morogoro wakulima wanalima miwa mingi zaidi kuliko uwezo wa viwanda kununua, miwa hii inaishia kuoza tu bila kutumika. Bodi ya Sukari ilipaswa kutoa leseni ili vikundi vya wakulima au wawekezaji wadogo wazalishe sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi leo Bodi ya Sukari nchini haijatoa leseni kwa viwanda vidogo vya uzalishaji sukari nchini na wala Serikali haijahamasisha Watanzania kuwekeza kwenye viwanda vidogo vya sukari ili kuwezesha miwa yote inayozalishwa nchini itumike kutoa sukari. Kama jambo hili lingefanyika, tungeweza kupunguza nakisi ya sukari nchini kwa zaidi ya tani 50,000.

(iii) Uwekezaji wa bidhaa kama sukari unahitaji vivutio vya punguzo la kodi kutoka Serikalini. Kule Uganda, Rais Museveni tangu aingie madarakani aliweka vivutio maalum kwa viwanda kama Kakira Sugar ili wazalishe sukari ya kutosha. Viwanda vya sukari Uganda hata umeme hulipiwa na Serikali kwa asilimia 50 ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuvilinda dhidi na ushindani wa sukari kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Serikali haijaona kuwa vivutio (subsidies) kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji ili kuwezesha kuzalisha sukari, kutengeneza ajira na kupata faida ni jambo la lazima. Sisi Kigoma mwaka 2016 kuna mwekezaji alitaka kuzalisha sukari tani milioni moja kwa mwaka kwa kulima miwa Kasulu, Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Viwanda walibishana kuhusu vivutio (kama wanavyobishana sasa juu ya mafuta ya kula), leo mradi ule wa uwekezaji umekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanywa na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kwa kutumia Kampuni ya LMC International, ulibaini mahitaji ya sukari kwa mwaka 2016/2017 ni wastani wa tani 590,000 ambapo kati ya hizo, tani 455,000 ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na tani 135,000 kwa matumizi ya viwandani. Leo mwaka 2018 nakisi hiyo ya mahitaji ya sukari imekua zaidi, bei ya sukari iko juu zaidi ya shilingi 1,800 iliyokuwepo mwaka 2016 kabla ya Serikali kuweka zuio la kuagiza nje sukari bila kwanza kuwa na mpango wa kuondoa nakisi iliyopo, sasa bei ni wastani wa shilingi 3,000 nchi nzima. Serikali ingetusikiliza mwaka 2016 leo tusingekuwa hapa tulipo, hata miradi inayopangwa sasa kupunguza nakisi, kama ya Mkulazi, ingeanza mapema zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, thamani ya fedha tunazotumia kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ni zaidi ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2018/2019. Serikali ingekubali ushauri wa mwaka 2016 wa kufungamanisha sekta ya viwanda na kilimo isingesumbuliwa mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nchi iendelee, maendeleo ya viwanda yanapaswa kufungamanishwa na sekta nyingine za uchumi kwa sababu kuna kutegemeana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tanzania ili tuendelee ni lazima kufungamanisha shughuli za uchumi zinazohusisha wananchi wengi zaidi na sekta ya viwanda ili huo uchumi wa viwanda uwe na tija kwa watu. Sekta ya kilimo kwa ujumla ikihusisha uvuvi na ufugaji huhusisha asilimia 75 ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta za viwanda na kilimo kwa pamoja zinachangia nusu ya Pato la Taifa (GDP) na nusu nyingine ni sekta ya huduma. Nadharia za uchumi zinatuambia kuwa tija ikiongezeka kwenye sekta ya kilimo, inawezesha sekta ya viwanda kukua na kisha sekta ya huduma. Hapa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, sekta ya huduma iliruka hatua hizi za ukuaji, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa zaidi kwenye GDP kuliko kilimo au viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunaambiwa uchumi unakua lakini umaskini wa wananchi haupungui, ni kwa sababu ya huduma haiajiri watu wengi kama sekta ya kilimo na hivyo uchumi unaokuzwa na sekta ya huduma hauajiri watu wengi kama sekta ya kilimo na hivyo uchumi unaokuzwa na sekta ya huduma ni nadra kuondoa umaskini. Sekta za kuondoa umaskini ni kilimo na viwanda maana zinaajiri watu wengi zaidi. Hivyo ili tuendelee ni lazima kufungamanisha viwanda tunavyotaka kuvijenga na kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano tuliieleza haya wakati wa mwaka wa fedha wa 2016/2017, mwaka wake wa kwanza wa bajeti lakini ikashindwa kusikiliza ushauri wetu. Hivyo kushindwa kufungamanisha kilimo chetu na viwanda tunavyotaka kujenga hasa vya bidhaa tunazozitumia zaidi kama mafuta ya kula, bidhaa ambayo ina mahitaji makubwa na sasa bei yake imepanda toka shilingi 55,000 mpaka shilingi 70,000 kwa ndoo ya lita 20 kutokana na masuala yanayohusu uingizwaji wake kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa tatizo la mafuta ya kula nchini na utatuzi wake; suala la mafuta halina tofauti na suala la sukari, ukipanda gari ukapita njia ya Singida unaona wananchi wamepanga madumu ya mafuta ya alizeti wanauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu Kigoma sisi ndio wazalishaji wakuu wa mafuta ya mawese nchini, lakini bado bei ni haba, uzalishaji wenyewe ni duni na hautoshelezi hata soko la ndani. Kimsingi tarehe 17 Mei, 2016 wakati wa kusomwa kwa bajeti ya Wizara hii kulikuwa na matatizo matatu makuu kwenye sekta ya mafuta ya kula nchini na niliyaeleza katika mchango wangu kama ifuatavyo:-

(i) Suala la unafuu mkubwa wa kodi kwa mafuta yanayoingizwa kutoka nje ambao Serikali iliutoa kwa waagizaji nchini. Unafuu huo ulivunja hamasa ya uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya kula ndani ya nchi. Mazingira ya unafuu ule wa kodi yaliwafanya wafanyabiashara waone ni nafuu na kazi rahisi zaidi kuagiza mafuta nje kuliko kuzalisha ndani. Jambo hili la unafuu wa kodi kwa waagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje likaua ushindani wa bei na viwanda vya ndani vikashindwa kushindana kwenye soko na hivyo kupunguza uzalishaji, jambo lililoifanya nguvukazi ya wananchi wanaolima mawese na alizeti (mazao makuu ya kuzalishia mafuta nchini) kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule wa bajeti ya mwaka 2016/2017 tuliishauri Serikali iondoe unafuu huu wa kodi inaoutoa kwa waagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ili kulinda na kunusuru viwanda vyetu vya ndani na tuchochee uzalishaji zaidi wa ndani wa mafuta ya kula, jambo ambalo lingechangia ukuaji wa kilimo cha mawese na alizeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017 kodi kwenye mafuta ya kula kutoka nje ni 10% (imports duty) na 18% VAT tu. Tukashauri jambo hili libadilike. Mwaka huu ndiyo Serikali imekubali kubadili ushauri wetu wa kuondoa unafuu wa kodi kwa waagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje baada ya kuwa tumepoteza zaidi ya mwaka mmoja na nusu wa kuviathiri viwanda vyetu vya ndani.

(ii) Kama ilivyo kwenye sukari, tuna nakisi kwenye uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula. Mwaka jana uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ulikuwa ni tani 180,000 tu wakati mahitaji yalikadiriwa kuwa ni tani 400,000 mpaka tani 520,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa uzalishaji ndani ukiwa ni asilimia 30 ya mahitaji na uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ukiwa ni asilimia 70; pia asilimia 55 ya mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni mafuta ya mawese (palm oil) yanayoagizwa kutoka nje ya nchi. Inakadiriwa kuwa mafuta ya alizeti yanayozalishwa yanatosheleza mahitaji ya ndani kwa asilimia 40 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa katika uzalishaji wa mafuta ya alizeti na mawese nchini inatokana na upungufu wa mbegu zenye ubora stahiki wa kutoa mafuta kwa wingi. Pia uwepo wa viwanda vichache vya kuzalisha mafuta yatokanayo na mazao hayo. Hivyo fursa ya kuwafanya wakulima wetu kuzalisha zaidi na kuziba nakisi hii kukosekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri kuwa Serikali inapaswa kuwekeza kwenye uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula kwa kuhamasisha kulimwa zaidi kwa mazao yanayozalisha mafuta ya kula (pamba, karanga, alizeti na mawese) pamoja na kufungamanisha uzalishaji zaidi wa mazao hayo na sekta ya viwanda kwa kuweka unafuu wa kodi kwenye uagizaji wa mashine za kukamulia mafuta ya kula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hamasa ndogo ya Serikali kwa wakulima wawekezaji wa viwanda. Serikali imeshindwa kufanyia kazi ushauri huu tangu mwaka 2016, katika wakati ambao mahitaji ya mafuta ya kula yanapanda nchini, bado uzalishaji wa ndani umebaki ulivyo.

(iii) Kwa lengo la kujazia nakisi ya uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula uliopo, nchi yetu inatumia sehemu kubwa ya akiba ya fedha za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Kwa wastani kwa mwaka tunatumia USD milioni 340 sawa na shilingi bilioni 782 zaidi ya bajeti yote ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2018/2019 ambayo ni shilingi bilioni 727.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa maskini zaidi nchini. Shilingi bilioni 782 tunazopeleka Malaysia kununua mafuta ya mawese kwa ajili ya kujazia nakisi yetu ya ndani zingeweza kabisa kufuta umaskini wa Kigoma. Tuna mradi Kigoma wa kupanda michikichi ili kuzalisha mafuta ya mawese ulio chini ya Serikali ya Mkoa. Mpango wetu ni kila familia kupanda hekta moja ya michikichi, lengo ni kuzifikia familia 100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa familia hizo za Kigoma kwenye kilimo cha mawese unaweza kuondoa kabisa suala la Tanzania kuagiza mawese kutoka nje maana tutaweza kuzalisha tani 200,000 za crude palm oil (CPO) kwa mwaka, kuzalisha ajira nyingi, kupandisha hali ya maisha ya wananchi/wakulima na kukuza biashara nyingine. Uzalishaji ni ndani ya miaka miwili tu tangu upandaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi biashara ya uzalishaji wa mafuta ya kula ni fursa kubwa kwa nchi yetu ambayo ingetumika vyema ingeweza kufuta umaskini wa wananchi wetu. Leo hii ninapozungumza hapa Bungeni bei ya lita moja ya mafuta ya alizeti/mawese ni shilingi 4,000 ikiwa imepanda kutoka shilingi 3,500 na ni bei kubwa kuliko bei ya lita ya petroli kwenye soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutimiza lengo hilo Kigoma wanahitaji watu watakaowekeza kwenye viwanda vya kuzalisha mawese. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ishirikiane na uongozi wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha tunazalisha mafuta ya kula ya kutosha ili kuondokana na uagizaji huu. Mawese na alizeti ndiyo suluhisho la kudumu la suala la mafuta ya kula. Ni imani yetu kuwa sasa Serikali itabeba ushauri huu ili miaka miwili kutoka leo tusijikite kujadili tena suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kwamba vyuma vitazidi kukaza tukipuuza fungamanisho la miradi mikubwa na ujenzi wa viwanda nchini. Serikali ibebe ushauri wangu wa mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukumbushia ushauri wangu juu ya namna bora ya kupunguza nakisi na kupunguza bei ya bidhaa za mafuta ya kula na sukari nilioutoa wakati wa bajeti ya Wizara hii kwa mwaka 2016/2017 sasa naomba pia nikumbushie jambo la tatu muhimu nililoishauri Serikali kuhusu hali ya uchumi wa nchi yetu, juu ya sababu ya fedha kupungua nchini (vyuma kukaza) na namna ya kuitumia miradi mikubwa tunayoifanya nchini kuendeleza sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nililieleza kwa undani wakati wa bajeti ya Wizara hii ya mwaka 2017/2018. Serikali haikuchukua ushauri ule, kwa sababu ya umuhimu wake, naomba niikumbushe tena Serikali juu ya umuhimu wa kuifungamanisha sekta ya viwanda na ujenzi wa miradi mikubwa tunayoifanya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama vile barabara, ndege, madaraja, mabomba ya gesi, mafuta na kadhalika. Fedha nyingi za ndani na za wafadhili zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza miradi hii. Nitajikita kwenye kurudia mfano nilioutoa mwaka jana juu ya mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha SGR. Kwenye mradi huu wastani wa shilingi trilioni 17 zinahitajika kukamilisha ujenzi wake kati ya Dar es Salaam na Mwanza (kilometa 1,200).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kilometa moja ya reli unahitaji chuma cha pua (steel) chenye ubora wa hali ya juu kiasi cha tani 40 mpaka 60. Sisi tunajenga kilometa 1,200 za reli kwa sasa hivi na baadae zitaongezeka kwa vipande vya Tabora - Kigoma, Kaliua - Mpanda - Karema, Uvinza - Musongati na miradi mingine kama Mtwara - Mbamba Bay, Ruvu - Tanga, Tanga – Musoma - Kigali na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi, Tanzania inahitaji siyo chini ya tani 500,000 za chuma cha pua (steel) katika kipindi cha miaka michache ijayo. Kwa mipango iliyopo sasa ni kwamba mataruma ya reli yataagizwa kutoka nje na kuletwa nchini na hivyo kuzalisha ajira huko kwenye nchi za nje ambazo mataruma hayo yatazalishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za miradi hii zitakwenda nje ya nchi, kama ilivyo kwenye fedha za mafuta ya kula na sukari, Watanzania hawatafaidika kabisa. Je, Serikali imeweka mikakati ya kufungamanisha maendeleo ya viwanda na miradi hii? Je, kuna mipango shirikishi ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi hii unawasaidia zaidi Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, sekta binafsi ya Tanzania kwa ushirikiano na Serikali imeandaliwa kuzalisha bidhaa na malighafi zinazotakiwa kwenye miradi hii? Hivi Serikali imeambatanisha faida, ajira, mapato ya kodi na mapato ya fedha za kigeni kwenye fungamanisho la miradi hii ya maendeleo na sekta yetu ya viwanda? Maswali haya niliyauliza mwaka 2017 hayakupata majibu, nayarudia hapa ili Serikali ichukue hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mikubwa yote duniani ina mikataba ya ziada iitwayo Offsets Agreements. Offsets Agreements ni makubaliano maalum kati ya Serikali na mzabuni wa miradi (kwa mfano ubia kati ya kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki na Kampuni ya Contrucao Africa SA ya Ureno ulioshinda zabuni kipande cha reli kati ya Dar es Salaam - Morogoro) makubaliano ambayo huweka msukumo maalum wa kisera na kisheria ili kuhakikisha watu wetu wanafaidika wakati wa ujenzi wa miradi mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida husika huwa ni kwa kushirikiana kwenye uzalishaji wa sehemu ya malighafi zitakazotumika wakati wa mradi na pili katika kuhakikisha kuwa sehemu ya utaalam uliotumika wakati wa ujenzi unaachwa nchini ili kuhakikisha tunawajengea uwezo Watanzania wa kufanya miradi ya namna hii siku za usoni (transfer of knowledge).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina chuma kingi sana kule Mchuchuma na Liganga na pia tuna makaa ya mawe ya kuchenjua chuma hiki ili kupata chuma cha pua (steel). Mradi huu wa reli peke yake ungeweza kuchochea maendeleo makubwa kwenye sekta ndogo ya migodi na viwanda vya chuma. Tungekuwa na mipango thabiti, sisi Tanzania tungekuwa ndio wazalishaji wakubwa wa chuma nchini na hata uzalishaji wa chuma cha kujenga reli kwenye eneo la Mashariki mwa Afrika na Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa reli unaweza kufungamanishwa na sekta ya kilimo nchini kwa bidhaa za ngozi na mkonge kutumika katika utengenezaji wa vitanda na viti vya mabehewa ya treni. Sekta yetu ya ngozi pamoja na ile ya katani zingeweza kufaidika sana kwa mradi huu mmoja tu wa reli kwa kuhakikisha kuwa mapambo ya ndani ya mabehewa yanakuwa ya bidhaa za ngozi na viti vinakuwa vya bidhaa za katani. Hivi ndivyo namna nchi nyingine zimeweza kuchochea viwanda kwenye mnyororo wa thamani. Najua tunatangaza zabuni ya mabehewa haya, tumetilia maanani jambo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa hizi Offsets Agreements kati ya Serikali na Mzabuni kwenye mikataba kungehakikisha Serikali inawakutanisha wakandarasi wa reli na wazalishaji wa bidhaa za ngozi na katani na kungehakikisha uwekezaji kwenye sekta ya uchimbaji madini na viwanda vikubwa vya chuma. Tunaweza kufanya haya kwenye miradi mikubwa ya maji, ujenzi wa bomba la mafuta na kadhalika. Naisihi Serikali itazame hii miradi mikubwa na kuifungamanisha na mkakati wetu wa viwanda ili fedha za miradi hii zibaki zaidi nchini, zitumike kuinua sekta yetu ya viwanda, zitoe ajira kwa watu na zisaidie kuchochea mzunguko wa fedha na kupunguza ugumu wa maisha (vyuma kukaza).

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni kwamba tuwe na mkakati maalum ili kuingiza dola bilioni moja kwa mazao ya biashara na India. Mei 2016 tulipokuwa tunajadili makadirio na matumizi ya Wizara hii, viwanda vyetu vilikuwa vinazalisha na kuuza nje ya Tanzania bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.408 (takribani shilingi trilioni 2.6)

na hivyo, kuwa sekta ya pili kwa kuingiza fedha za kigeni nchini kwetu baada ya sekta ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mei 2017 hali hiyo ya uzalishaji na uuzaji wa bidhaa zitokanazo na viwanda haipo tena, tunaweza kusema kwa uwazi kuwa biashara hiyo imeshuka mno. Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Serikali yenyewe, kupitia taarifa ya Benki Kuu ya sasa (BoT Monthly Economic Review), sekta ya viwanda inauza nje ya nchi bidhaa za thamani ya dola za Marekani milioni 879 tu (takribani shilingi trilioni 1.962). Hivyo sekta hiyo kushuka na kuwa ya tatu katika kuchangia mapato ya fedha za kigeni baada ya utalii na dhahabu. Ushukaji huu ni wa zaidi ya asilimia 38 yakiwa ni mapato kidogo zaidi tangu mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mei 2018 BoT hata hawaweki takwimu za mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani maana hali ni mbaya zaidi. Serikali inaona aibu kuwa sera zake mbaya za kiuchumi zimeshusha uzalishaji kwenye viwanda na sasa imeamua kuwakataza BoT kutoa takwimu za mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani. Ni kilio kwa wakulima wa mbaazi, choroko, dengu na giligilani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauzo ya bidhaa za viwanda kwenda nje ya nchi siyo pekee yaliyoshuka, lipo pia eneo la biashara ya mazao ya kitaifa. Mchango wangu kwenye bajeti ya Wizara hii kwa 2018/2019 utajikita zaidi kwenye eneo la biashara ya kimataifa, hasa biashara ya mazao ya kilimo jamii ya mbaazi, choroko, dengu na giligilani kwenda nchini India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera mbaya za uchumi, utekelezaji mbaya wa diplomasia yetu na juhudi ndogo za Serikali kutafuta masoko ya bidhaa zetu kimataifa ndani ya miaka miwili na nusu ya Serikali ya Awamu ya Tano vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuanguka kwa biashara ya mazao hayo kimataifa na hivyo Taifa letu kukosa fedha za kigeni. Miongoni mwa biashara za kubwa za mazao nchini ni biashara ya mbaazi tukiwa na soko kubwa nchini India. Mwaka 2015/2016 mauzo ya nje ya mbaazi (kwenda India) yalifikia USD milioni 224 sawa na shilingi bilioni 515 yakiweka rekodi ya juu kabisa ya mauzo yetu ya mbaazi India na pia yakiweka rekodi kwa wakulima kuuza hadi shilingi 3,000 kwa kilo moja ya mbaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 9 Julai, 2016 Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliwasili nchini kwa ajili ya ziara yake ya kwanza Afrika, ambapo alitembelea pia Msumbiji, Afrika Kusini na Kenya. Lengo la kuja nchini likiwa ni kuonesha uhusiano mzuri kati ya nchi hiyo na Tanzania na pia kusaini mkataba wa ununuzi wa mbaazi kati ya nchi zetu mbili hasa kwa kuwa Tanzania ilikuwa imeuza mbaazi zenye thamani ya nusu trilioni kwa nchi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkutano wake na Waziri Mkuu Modi, uliofanyika tarehe 10 Julai, 2016 Rais Magufuli alisema yafuatayo na nanukuu: “Mwaka jana (2015), Tanzania iliiuzia India tani 100,000 za mazao ya kunde ambayo yalikuwa na thamani ya USD milioni 200. India inahitaji tani milioni saba za mazao hayo kwa mwaka, kwa hiyo, kuna fursa kubwa ya kufanya biashara katika kilimo hicho.” Mwisho wa kunukuu na akawahimiza wakulima wa mbaazi kulima zaidi zao hilo kwa kuwa soko la uhakika liko India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali yetu kwa zembe tu ilichelewa kusaini makubaliano hayo ya ununuzi wa mbaazi kati ya nchi zetu mbili mpaka muda wa kikomo iliopewa na India ulipopita. Jambo hilo la kuchelewa kusaini makubaliano hayo limetufanya tutolewe miongoni mwa nchi zinazoruhusiwa kuuza mbaazi India na hivyo kusababisha tukose soko la kuuzia mbaazi zetu kwa miaka hii miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa haikuwa na mkataba wa kuuza mbaazi India, kwa kuwa ilichelewa kusaini makubaliano, lakini Serikali ilikaa kimya tu na taarifa hizo, haikuwaeleza wananchi waliohamasika kulima zaidi mbaazi kwa sababu ya bei kubwa ya shilingi 3,000 kwa kilo ya mwaka 2015/2016 kuwa haina mkataba na India. Matokeo yake wakulima na wafanyabiashara wetu wameishia kupata mateso tu na kufilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017 thamani ya mauzo ya mbaazi kwenda India ikashuka mpaka USD milioni 131 sawa na shilingi bilioni 303.3. Mapato yakipungua kwa zaidi ya bilioni 200. Kwa mwaka 2017/2018 mauzo ya mbaazi kwenda India yakishuka zaidi hadi kufikia USD milioni 75 sawa na shilingi bilioni 172.5 na kusababisha ufukara kwa wakulima, kiasi sasa kilo moja ya mbaazi kuuzwa kwa shilingi 150 kutoka shilingi 3,000 ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo baya zaidi ni kuwa Serikali yetu imeshindwa kabisa kutumia mahusiano yetu ya kibiashara, kidiplomasia na kihistoria na India kuhakikisha tunamaliza jambo hili na kunusuru soko letu kimataifa. Katika wakati ambao hatuwezi kuuza mbaazi India, kwa mwaka jana tu India alisaini makubaliano na kununua mbaazi kutoka Nigeria zenye thamani ya USD bilioni mbili sawa na zaidi ya shilingi trilioni 4.6, wakati ambao mbaazi zetu zilibaki kuozea kwa wakulima. Utafiti wa Januari, 2018 uliofanywa na Taasisi za Tanzania Pulses Network na East Africa Grain Council unaonesha kuwa hasara iliyopatikana kutokana na mbaazi zisizouzwa ni kubwa mno, kipato cha mwananchi kikitajwa kushuka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si mbaazi tu hata giligilani hali ni hiyo, bei yake imeshuka kutoka shilingi 300,000 mwaka 2016 mpaka shilingi 150,000 kwa gunia kwa mwaka 2017 wananchi wa Mkoa wa Manyara wanaumizwa sana na hali hiyo. Hali hiyo ya maumivu na kilio ipo pia kwa wananchi wa Misungwi, Mkoani Mwanza ambao mwaka 2016 waliuza choroko kwa shilingi 300,000 kwa gunia lakini bei hiyo ilishuka mpaka shilingi 150,000 kwa mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao mengine yaliyoshuka bei ni mazao ya jamii ya dengu, mwaka 2016 wakulima wa mazao haya waliuza kilo nne za dengu kwa bei ya shilingi 7,500 lakini tangu mwaka jana bei ya mazao haya kwa hizo kilo nne imeshuka mpaka shilingi 2,500 tu, soko la mazao haya likiwa ni India. Ukitazama kwa undani, ni dhahiri kuwa mazao haya ya mbaazi, choroko, dengu na giligili, yanao uwezo wa kuliingizia Taifa zaidi ya USD bilioni moja kama tutaweka mipango ya kuongeza uwezo wa uzalishaji pamoja na kutumia diplomasia na historia yetu na India kutatua changamoto ya soko iliyoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike ili kufikia lengo la kuingiza fedha za kigeni, USD bilioni moja kupitia mazao haya maalum yenye soko India? Baada ya kuonesha upungufu wa Serikali ya CCM katika fungamanisho la kilimo na biashara ya nje, natoa pendekezo la jawabu la hali hii, kama ifuatavyo:-

(i) Tusahihishe mahusiano yetu na India. Tuna faida mbili za kimahusiano na India, ya kwanza ni historia kati ya nchi zetu tangu wakati wa Baba wa Taifa, Mwalimu na Waziri Mkuu Nehru. Pili, ni uwepo wa jamii kubwa ya wafanyabiashara wa Kitanzania wa jamii ya Kihindi wenye asili ya Jimbo la Gujarati ambapo anatokea pia Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi. Kuna kulegalega kwenye mahusiano yetu, tusahihishe.

(ii) Tuitumie vyema diplomasia yetu. Kwa vyovyote ni lazima Serikali yetu ifanye diplomasia ya hali ya juu sana na Serikali ya India kwenye suala la soko la bidhaa za pulses hasa mbaazi, choroko, giligilani na dengu. Nchi yetu haiwezi na haipaswi kuzidiwa na nchi nyingine za Afrika katika suala zima la soko la bidhaa zake nchini India. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambayo inahusika na biashara ya nje, inabidi ifanye kazi ya ziada kwenye eneo hilo, biashara ya nje ni diplomasia, tuitumie.

(iii) Tuhakikishe tunarudisha soko letu. Nguvu yetu ya historia na mafungamanisho na India pamoja na diplomasia yetu vitumike vyema kwa pamoja kuhakikisha tunarudisha soko letu la kuuza mazao haya. Hili la kurudisha soko linapaswa kuwa jambo la kufa na kupona kwa Wizara hii. Ikibidi Waziri, Mheshimiwa Mwijage aende tena kuonana na Waziri mwenzake wa Viwanda na Biashara wa India, Suresh

Prabhu hasa kwa kuwa alishindwa kuambatana na msafara wa Makamu wa Rais juzi kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola kule London, mkutano ambao Waziri Mkuu Modi alihudhuria.

(iv) Tuongeze uzalishaji wa mazao haya. Juhudi za diplomasia ya kurudisha soko letu ziende sambamba na kuongeza uzalishaji wetu katika kulima mazao haya. Ni lazima kuongeza uzalishaji wa mazao haya ili kuweza kupata mapato zaidi ya fedha za kigeni kwa mauzo ya nje.

Pia biashara ya mbaazi, choroko, dengu na giligilani inaweza kuchangia kwenye juhudi za kuondoa umaskini wa wakulima wetu ikiwa tutaweka mkakati maalum wa uendelezwaji wa mazao haya. Mkakati huo unapaswa kuhusisha kuwahamasisha wakulima waliokata tamaa kuanza upya kulima mazao haya, kisha kuwaunganisha kwenye vyama vya ushirika, kuhakikisha vyama hivyo vya ushirika wa wakulima tunaviunganisha na masoko moja kwa moja bila kupitia watu wa kati (madalali wanaowanyonya) na kuongeza tija ya kilimo chao kwa kuwaunganisha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuweka fao la bei kwenye mifuko hiyo ili kuwalinda pale bei ya mazao inapoanguka

Mheshimiwa Mwenyeikiti, tukifanya haya, ni imani yangu kuwa tutaweza kabisa kuongeza uzalishaji hata kwa tani tano tu kutoka sasa ili kufikia mapato ya USD bilioni moja ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuwasilisha.