Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kwa sababu muda ni mchache sana nitakwenda haraka haraka. Kwanza naomba nimpongeze Waziri na Manaibu wake wote wawili na watendaji katika wizara kwa jinsi wanavyofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni tunashukuru Serikali kwa kujenga barabara ya Sumbawanga – Kizi- Kibaoni lakini kipande cha Kizi- Lyambalamfipa- Stalike ambacho ni kabla hujafika Hifadhi ya Taifa ya Wanyama ya Katavi kina kilometa 35.5, tunaomba Waziri atuambie ni lini ataiweka kwenye bajeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika barabara hiyo ambayo imeshajengwa na imekamilika ya Stalike – Mpanda bado kuna wananchi ambao bado wanadai fidia. Sasa tutaomba Waziri atuambie katika bajeti hii kiasi gani ataenda kuwalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru na kwenye kitabu nimeona barabara yetu ya kutoka Mpanda – Inyonga – Ipole – Sikonge – Tabora kilometa 346 na tayari wakandarasi wameanza mobilization. Sasa kwa sisi watu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kuna fidia ya utility facilities yaani matenki ya kuhifadhi maji ambapo yapo mawili yanaenda kubomolewa, lakini kwa taarifa ambazo sio rasmi, kuna shilingi milioni 162 tu ambazo zipo katika mkataba ambazo haziendani na gharama halisi ya haya matenki ambayo tunatakiwa kufidiwa. Kwa hiyo, tutaomba Serikali iangalie uhalisia wa gharama za haya matenki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la reli, treni yetu ya kutoka Tabora mpaka Mpanda, njia yake kwa kipindi hiki cha masika inasumbua sana, hapa siku tatu zilizopita wananchi wamelala siku mbili kati ya Kaliua na kilometa 60 kutokana na mvua na kokoto kuondoka. Kwa hiyo, tunaomba katika bajeti hii na ukarabati ufanyike kwa umakini na pia mabehewa yaweze kuongezwa kutokana na hasa kipindi cha kiangazi abiria wanakuwa ni wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wananchi pia wapo tayari kuachia maeneo ambayo yanamilikiwa na shirika letu la reli lakini upimaji wa ardhi mpya ulichelewa kwa hiyo tutaomba hisani ya Serikali watuvumilie kidogo wakati wananchi wanajenga maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la TAZARA, kiuongozi tunaona Serikali ilete sheria iweze kuboreshwa ili angalau tuwe na kupeana miaka mitatu mitatu katika kuongoza shirika hili na lifanye kiufanisi zaidi na kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TTCL, TTCL tumebadilisha sheria mwaka jana. Sasa niombe Wizara na Kampuni ya TTCL wakimbie na wasitembee. Walianzisha code yao 0732 lakini idadi ya wateja wao imekwishashuka na sidhani kama kuna watu wengi sana wanaotumia simu za mkononi za TTCL. Sasa kwa kuwa mkongo wa Taifa upo chini yao, wakimbie; amekuja juzi Halotel lakini ana wateja wengi, kwa nini TTCL bado anatambaa. Kwa hiyo, Serikali na uongozi mzima wa TTCL waje watueleze kwamba watafanya nini ili shirika liweze kufanya kazi kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TCRA, Halmashauri zetu nchi nzima kuna minara ambayo kampuni za simu zina- operate na sasa hivi wameweka kampuni moja na haya makampuni ya simu yanapanga, sasa tunatakiwa tupate service levy kutokana na mapato ambayo wanaingiza katika kila eneo. Kwa hiyo, tuombe kama inashindikana basi service levy inayotoka TCRA iingie na iwe ring fenced labda kwenye Wizara ya Afya kwa ajili ya kusaidia vifo vya mama na mtoto kama inashindikana kila Halmashauri kuweza kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vivuko, tunaona kwamba katika barabara nyingi hakuna hizi underground crossing. Kwa mfano tu ukichukua eneo la NARCO ilitakiwa kuwe na kivuko cha chini ili wanyama waweze kupitishwa, sasa kwa nini TANROAD katika ku-design barabara maeneo mengine wasiweke vivuko vya kupita chini ili tuondoe ajali ambazo wananchi wetu na mifugo wanagongwa na hii itasaidia usalama kati ya wanyama na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni kuhusu ATCL, tunaipongeza Serikali kwa hatua kubwa, nimeona mchangiaji mmoja alisema kwamba kuwe na ndege za kampuni tofauti italeta changamoto kwenye suala la kuwa na hizi anga…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.