Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na leo hii kuweza kupata fursa ya kuweza kuchangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa na maswali zaidi kwa Mheshimiwa Waziri ili atakapokuja hapa aweze kutupa ufafanuzi. Kwanza ukiangalia kitabu cha Waziri cha mwaka 2017/2018 kinasema kwamba Waziri aliomba bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa ndege tatu za Bombardier; Q400, tatu; pamoja na CS300, mbili; na ndege kubwa ya 787.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Mpango ambao tumewasilishiwa Machi mwaka huu na Waziri wa Fedha pia anasema kwamba amelipa bilioni 7.8 kwa ajili ya kutekeleza mkataba wa ununuzi wa ndege, lakini pia ameomba bilioni 495.6 kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ndege mbili za CS300 kwa malipo ya asilimia 30 na ndege kubwa ya 787 kwa malipo ya asilimia 52.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwaka jana amesema Waziri kwamba ameomba hizi fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya ndege hizi, lakini mwaka huu huu tena ameomba tena karibu bilioni zile zile 500 anaenda kulipia tena ndege hizi hizi ambazo ziliombewa fedha wakati ule. Sasa namwomba Waziri atakapokuja hapa atufafanulie ni ndege zipi nyingine ambazo zinazoenda kulipiwa na kule mwanzo katika kitabu cha mwaka 2017/2018 hakueleza kwamba analipia asilimia 30 ya hizi ndege mbili CS300. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye Waziri wa Fedha amesema kwamba ameomba fedha kwa ajili ya kulipia tena ndege ya Bombardier Q400, sasa naomba Waziri kujua haya maelezo ambayo ameyatoa Waziri wa Fedha je, kuna Q400 nyingine ya nne ama ni zile zile tatu za nyuma ambazo zilinunuliwa hapo kabla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza mwaka juzi na mwaka jana tulitoa ushauri hapa kwa Waziri kwamba hakuna anayekataa shirika la ndege kuanzishwa ili lilete tija katika Taifa letu, lakini tulisema kwamba biashara ya ndege ni biashara ya ushindani na tunahitaji wataalam wa biashara za ndege wapewe shirika hili ili waweze kulianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa haraka haraka limeanzishwa shirika lakini hadi hivi leo Kamati hapa imesema kwamba shirika hili limeshindwa kuungwa katika hii Taasisi ya Mashirika ya Ndege ya IATA ili kuweza kujiendesha shirika hili na badala yake tunatafuta kampuni nyingine ili ifanye kazi hii kwa niaba yetu ambayo ina uwezo wa kufanya kazi na IATA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii inaonesha wazi kwamba yale tuliyokuwa tunayasema ndiyo ambayo yanayojitokeza sasa hivi. Ukiangalia ripoti hii ya CAG. CAG anasema kwamba ununuzi wa ndege umekiuka taratibu za manunuzi. Hatusemi hivi kwamba tunaipinga Serikali, sio kwa sababu ya kuipinga Serikali lakini tunaisaidia Serikali ifanye kazi zake na iwe ni tija kwa wananchi; lakini leo shirika hili linakwenda kuwa mzigo kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mmoja, kabla shirika hili halijarejeshwa hapa kuwa marehemu na South African Airways yalijitokeza mashirika matatu kulifufua hili shirika. Shirika la kwanza ni British Airways pamoja na Emirates na la tatu ni hili South Africa. British Airways walikuwa na lengo la kuifanya Air Tanzania iwe ndiyo kama career yao kwa East Africa pamoja na Africa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Emirate walitoa offer kwa Air Tanzania kwamba wakipewa hili shirika wakilitumia kwa ajili ya East Africa hii liweze kufanya kazi kupitia Emirate kwa pamoja, pamoja na shirika la Emirate wangefanya matengenezo ya viwanja vyote vya ndege ambavyo leo tunavipigia kelele hapa ndani ya nchi yetu. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana kutokana na kwamba hatuna viongozi ambao wanauzalendo na nchi hii wakatanguliza maslahi yao binafsi na British Airways na Emirates wakajiondoa na shirika likachukuliwa na South African Airways likarudi hapa shirika likawa marehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Emirates kukosana na Air Tanzania walikwenda kuingia makubaliano na shirika la Srilanka na wakafanya nao kazi kwa muda mrefu na wakawajengea kiwanja cha ndege cha kimataifa chenye shape kama ile ambayo imetengenezwa Dubai International Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo tunapozungumza utaratibu kwa sababu jambo lolote bila ya sera na utaratibu maalum Serikali haiwezi kufanya biashara ya ndege. Leo tuangalie Shirika la Air Rwanda, Serikali hiyo ilijitwika kifua kulichukua shirika wakawa wanaliendesha. Sasa hivi wanatafuta wawekezaji waliendeshe kwa sababu Serikali imeshaona kwamba ina mzigo mkubwa wa kulihudumia shirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri tunayasema haya kwa maslahi ya Taifa la Tanzania. Tuliposema kwamba waje wataalam, mtaalam unapompa kazi anaangalia mpaka liability ya taasisi husika.

Kwani kulikuwa na ulazima lazima tuseme hii inaitwa ATCL. Leo hapa tukiangalia Emirates kuna mashirika matatu sasa hivi, kuna Emirates yenyewe, kuna Fly Dubai kuna Etihad.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote yanafanya kazi na mashirika yote matatu haya yanakuja hapa Tanzania, yanafanya kazi zake yote matatu kila siku na yanafanya kazi kwa mafanikio makubwa. Sasa na sisi ilikuwa lazima tukae tutafakari ili kumsaidia Rais wa nchi hii aweze kufikia yale malengo ambayo anayakusudia, lakini naona sasa kwamba upande wa Mawaziri wanamwangusha Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ikiwa Rais alikuwa na nia ambayo ya kuonesha kabisa kunyanyua uchumi kupitia shirika la ndege lakini leo badala ya kufuata zile taratibu za kuonyesha kwamba shirika hili lingeweza kuleta tija na maslahi kwa Watanzania matokeo yake linakwenda kuwa mzigo. Hapa leo ukiangalia kwenye kitabu hiki hapa cha Waziri ambacho amekitoa tulisema hapa kwamba unapochukua career tofauti za ndege lazima na base ya matengenezo zinakuwa tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana leo Waziri kakubali maneno yangu na ndiyo maana kaingia mkataba na Ethiopian Airline kuzifanyia service ndege hizi za Air Tanzania. Tuliyasema haya katika Bajeti ambayo ilipita kuonesha kwamba lazima kutakuwa na cost za kuendesha shirika, sasa leo kwa sababu hatuwezi kujiendesha wenyewe ilibidi tutafute sasa shirika lingine liweze kutusaidia katika kufanyia maintenance ndege hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Waziri hii nchi ni yetu sote, tukiharibikiwa tumeharibikiwa sote. Sasa wasianze kulitoboa jahazi halafu tuzame sote. Ikiwa kuna uwezekano wa kuweka kalavati, tuweke hilo kalavati ili tusizame tufike safari yetu; lakini haiwezekani kwenda katika namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ukija katika suala la reli ya kati. Mheshimiwa Rais alimwomba aliyekuwa Rais wa South Africa, Jacob Zuma kwamba atusaidie kujenga reli ya kati, lakini haikuwezekana. Hata hivyo, tukapata bahati nyingine akaja Rais wa Uturuki na Rais akamweleza nia ya kujenga reli ya kati kwa standard gauge na Rais wa Uturuki alikubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunapata mkanganyiko, tunasema Rais alivyomaliza kuzungumza na Rais wa Uturuki anasema tumefanikiwa tumezungumza na Serikali ya Uturuki, tumeweza kupata reli ya kati ya standard gauge, lakini huku tunaambiwa kwamba fedha ambazo zinatumika kujenga hii reli ni fedha za ndani. Sasa part yao hao Waturuki ni ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba akija hapa Waziri atueleze inakuwaje kwa sababu inawezekana pengine watu wakawa hawana uelewa wa kutosha halafu taarifa zikatoka vingine. Hebu leo waje watueleze hapa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ajibu maswali.