Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa mahali hapa katika Bunge lako Tukufu. Pia napenda kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayozidi kuifanya. Mimi binafsi namwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu tele aendelee kutumbua majipu. Ewe Mwenyezi Mungu msaidie Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazozifanya kwa kulitumikia Taifa letu kwa moyo wa dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuwashukuru akinamama wa Mkoa wa Kagera kwa kunipigia kura nyingi za kutosha ili niweze kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. Nawaahidi kwa moyo wangu wa dhati sitowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo ni Wizara nyeti inayotegemewa na watu wengi. Mkoa wa Kagera tumebarikiwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na hali ya hewa nzuri yenye mvua za kutosha. Mkoa wa Kagera kilimo kimekuwa cha kusuasua kwa sababu ya teknolojia duni pamoja na pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera pembejeo hazifiki kwa wakati, unakuta mkulima ameshaandaa shamba lake kwa muda mrefu lakini kupata mbolea au mbegu bora kwa muda unaotakiwa imekuwa ni changamoto kwani mbolea haifiki wala mbegu. Kwa hiyo, naomba Serikali yako Tukufu iweze kuliangalia hilo. Pia kuna miundombinu mibovu ya usafiri wa mazao kutoka shambani hadi kwenye masoko, hilo pia naomba liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera tuna zao kuu ambalo ni mgomba (ndizi). Zao hilo limevamiwa na ugonjwa unaitwa mnyauko hasa kwa Wilaya za Ngara, Karagwe, Muleba na Bukoba Vijijini. Ugonjwa huo wa mnyauko umeshambulia sana migomba. Tunaomba Wizara husika iweze kuangalia jinsi itakavyoweza kutusaidia kutibu ugonjwa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wangu wa Kagera umebarikiwa kuwa na mazao makuu mawili ya biashara nayo ni kahawa na miwa. Kuhusu kahawa masoko yamekuwa ya kusuasua, imefika hatua wakulima wanapata shida, wanaanza kukata tamaa ya kulima zao la kahawa kwa kukosa soko. Unakuta wanaanza kufanya magendo ya kwenda kuuzia nchi jirani ili wapate unafuu wa bei. Tunaomba Wizara husika iangalie zao letu la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu zao la miwa, Mkoa wa Kagera pia umebarikiwa kuwa na Kiwanda kikubwa cha Sukari. Hata hivyo, nashauri wale wakulima wadogo wadogo waweze kusaidiwa kuwapa mashamba darasa ili waweze kuungana na wale wenye mashamba makubwa ili tuweze kupata viwanda vya kutosha vya sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee kuhusu mifugo. Mkoa wa Kagera una mgogoro kati ya Ranchi ya Kitengule na wananchi. Wananchi hawana sehemu ya kufugia mifugo yao, tunaiomba Serikali kushughulikia mgogoro huo haraka iwezekanavyo. Kagera tuna mifugo ya kutosha, inakadiriwa kuwa na ng‟ombe wanaofugwa wapatao 550,070, ng‟ombe wa asili wanakadiriwa kuwa 528,632 na ng‟ombe wa maziwa 21,438, mbuzi wafugwao wanakadiriwa kuwa 593, 607, mbuzi wa asili wanakadiriwa kuwa 583,202 na mbuzi wa maziwa 10,405. Wanyama wengine ni kondoo 53,061 na nguruwe 44,402. Ikitumiwa vizuri na Serikali itasaidia sana ukuaji wa uchumi Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla. Kwani itachochea ujenzi wa viwanda vya mazao ya mifugo na kutoa fursa za ajira kwa wananchi walio wengi hususani vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuongelea upande wa uvuvi. Usalama wa wavuvi siyo mzuri katika Mkoa wetu wa Kagera. Maharamia wanavamia sana wavuvi wanaokuwa ziwani wakivua samaki. Tunaomba Serikali iweke doria ili wavuvi wetu waweze kuwa katika security. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu leseni, nashauri wasitoze zaidi ya mara moja. Unakuta mvuvi yupo Bukoba Mjini akiamua kwenda Muleba akifika pale kuna leseni tena anatakiwa alipie. Tunaomba leseni iwe moja ili waweze kuzunguka kwa unafuu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali yako iangalie kuhusu nyavu. Wavuvi wadogo hawana makosa kununua hizo nyavu, washughulikiwe wale wanaoziingiza ili wapate zinazokubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali yako kwa hiyo shilingi milioni hamsini ambayo inatarajiwa kutolewa iangalie na wavuvi. Hiyo shilingi milioni hamsini imezungumziwa sana upande wa akinamama na vijana lakini kwa wavuvi sijasikia. Naomba pia wavuvi wakumbukwe, wana vikundi vyao nao wagawiwe hela hiyo ili waweze kujiongeza katika uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache naunga mkono kwa asilimia mia moja bajeti ya Wizara ya Kilimo iweze kupita.