Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kweli kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kufanya kazi kwa Awamu hii ya Tano, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri wake na Wizara kwa ujumla kwa kufanya kazi nzuri ambayo kwa kweli mimi nai-admire.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri amefika kwenye jimbo langu na kutembelea Hospitali ya Haydom na kwenda pia kwenye Kituo cha Afya cha Dongobesh na kutupatia fedha za kujenga kituo kile. Nakushukuru sana Mheshimiwa Ummy na kwa kweli kwa Serikali nzima pia naishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru ametuma tume ambayo imekwenda kwenye Hospitali ya Haydom na kuangalia Hospitali ya Haydom kama inakidhi kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya kanda. Sasa niombe Mheshimiwa Ummy waone basi namna gani ya kuisaidia Hospitali ya Haydom ili iweze kupanda hadhi iwe hospitali ya kanda. Kwa nini nasema namna hii, Haydom ni hospitali inayohudumia Mikoa mitano, ikiwemo Singida, Dodoma, Manyara bila kusahau Arusha na Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hospitali hii imeshakuwa katika eneo ambalo linafikika na pande zote hizi nilizozitaja ningeomba Serikali iangalie namna nzuri ya kuisaidia hospitali hii ili kupanda hadhi. Kwa mfano leo unaangalia Dar es Salaam kufikika kutokana na mafuriko imekuwa na shida; kwa hiyo angalia tungekuwa tumepandisha hospitali ya Haydom kuwa hospitali ya kanda tungekuwa tumepeleka huduma vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali yetu inapenda kusaidia watu wa vijijini, basi tusaidieni kuifanya hospitali hii iwe hospitali ya kanda ili iweze kutoa huduma nzuri kuliko kwenda kwenye hospitali kubwa ya KCMC. Kutoka Haydom mpaka KCMC kuna kilometa 400, kutoka Haydom mpaka kule tunasema Jakaya Kikwete kilometa 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, kwa sababu tumeshaleta mapendekezo na ameshaikagua na Wizara yake tunahitaji Madaktari Bingwa sasa waliobobea waende vijijini ili wakawasaidie mama na mtoto kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya niombe sasa; maana unaposhukuru maana yake unaomba mara ya pili na hata kwenye Sala ya Baba Yetu ukiangalia sana kwa sisi Wakristo, sala nzima ya Baba Yetu inasema Baba yetu uliye mbinguni jina lako litukuzwe, yote haya ni kumsifu. Unapomsifu Baba yako aliye mbinguni maana yake baadaye unaweka ombi. Kwa sababu unaposema utuongezee mkate wetu wa kila siku maana yake unahitaji kuomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huwezi kuwa na double standard, ukawa unaomba wakati huo huo unatukana. Kwa hiyo niiombe Serikali yangu ambayo inasikia, kwa kweli ahadi alizotoa Mheshimiwa Ummy ya gari ya wagonjwa pale Dongobesh mpaka leo inasubiriwa. Vile vile kubwa nishukuru pia kwa kutupatia hospitali ya wilaya ambayo itajengwa kwenye jimbo langu na nimeona kabisa kwenye bajeti hii ametutengea bilioni moja. Kwa hiyo nimshukuru sana yeye pamoja na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ni kwamba ninao ushauri kwenye Serikali. Nimepata nafasi ya kutembelea katika kiwanda kile ambacho kinatengeneza dawa ya viuadudu. Mimi niombe, kama kweli Serikali inahitaji kumaliza Malaria au kupunguza Malaria tuweze kuhakikisha ya kwamba kile kiwanda kinakwenda kufanya kazi ya ku-supply ile dawa ili kuweza kuua vimelea vya mbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimekwenda pale na hakika Mheshimiwa Rais alishaweza kuziagiza halmashauri zote nchini kuweza kununua zile dawa waka- spray kwenye maeneo yao ili kutokomeza vimelea vya mbu. Kwa msingi huo basi, siamini kama tuna dhamira ya dhati kumaliza tatizo hili la malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kumaliza malaria, niwashauri Wizara watafute namna, washauri hata hospitali zetu, kituo cha afya. Kwa mfano wakiviagiza au kuviomba hivi vituo vya afya, kwamba kila kituo cha afya kikanunua lita tano ya ile dawa, wakaagiza pia dispensary ikanunua kama lita tatu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: …ukaagiza maduka ya dawa yote nchini yakanunua ni rahisi kabisa kutokomeza malaria; lakini vinginevyo…

MWENYEKITI: Ahsante.