Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala,lakini nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu hapa wamezungumza mambo mengi sana na hasa hasa suala zima la uzalendo la Daktari Janabi, nami niungane nao kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba anajitoa na haya maendeleo tunayoyaona kwenye upasuaji wa moyo ni kwa sababu ya jitihada binafsi za Daktari Janabi ambaye ameamua kutumikia Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuna suala limeleezwa na Waheshimiwa Wabunge hapa, suala la delivery kits wale akinamama wanavyokwenda kijifungua katika hospitali zetu wanakuwa na changamoto kubwa sana juu ya vifaa vya kujifungulia. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa sana, tumekuwa tunaongea kwa muda mrefu sana ndani ya Bunge hili kwamba vifaa hivi viweze kutolewa katika hospitali zetu za Serikali, lakini jambo la kusikitisha sana mpaka leo hivi vifaa havitolewi kwa ajili ya akinamama wanapokwenda kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Mtwara Mjini nilipochukua pesa zangu nilinunua vifaa hivi vya milioni 30 zaidi ya akinamama 5,000 nimeweza kuwagawia, kila mmoja ujauzito ukifika miezi nane au miezi tisa anafika Ofisi ya Mbunge, nimeweza kuwagawia bure kabisa hizi delivery kits. Naomba sana Serikali iweze kuendeleza zoezi hili katika Majimbo yetu yote ye Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala hili la hospitali za Kanda. Tumekuwa tunazungumza sana ndani ya Bunge hili kwamba Kanda zote Tanzania zina hospitali za Kanda isipokuwa Kanda ya Kusini pekee mpaka leo bado hatuna hospitali ya Kanda. Tumekuwa tunaongea sana kila Bunge, hii ni mara yangu ya tatu nazungumza ndani ya Bunge hili na Serikali inaahidi kwamba tunajenga lile jengo. Mpaka leo jengo la OPD limejengwa kwa muda wa zaidi ya miaka 10, utafikiri hili jengo unajengwa mnara wa Babeli ambao ndiyo haujakwisha mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwamba hospitali ya Kanda ya Kusini tunamaanisha Mtwara, tunamaanisha Lindi, tunamaanisha pia kule Ruvuma mpaka leo hatuna hospitali ya Kanda, bajeti inayotengwa kwa ajili ya hospitali ya Kanda ya Kusini kila mwaka ni bajeti ambayo haitoshi hata lile jengo mpaka leo halijakamilika na tunaambiwa kila mwaka tutatenga pesa. (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha sana, unaweza ukaangalia kuna hospitali zingine za Wilaya tu, hospitali za maeneo mengine zimetengewa zaidi ya bilioni nne, zingine bilioni tano, lakini hospitali ya Kanda ya Kusini, taarifa nikipitia kwenye randama hapa naambiwa bilioni mia moja lakini mpaka leo hizo bilioni 100 zenyewe inakuwa ni kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa dada yangu Ummy Mwalimu tunamheshimu sana, hiyo hospitali ya Kanda ya Kusini, Mtwara, Lindi na Ruvuma tunaomba atenge pesa katika Bunge hili katika bajeti hii ili hospitali iweze kwisha, tumechoka kuzungumza neno moja kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba sana hospitali ya Mkoa wa Mtwara, hospitali ya Ligula X-Ray hakuna. Nimezungumza sana ndani ya Bunge hili, nimepiga kelele sana, nimeandika sana, hii ni bajeti yangu ya tatu nazungumzia suala hili kwamba hospitali ya Mkoa wa Mtwara haina X-Ray iliyoko yenyewe ni mbovu na hawa watu wa Ligula hospitali walifanya jitihada kuiomba NHIF waweze kuwanunulia kwa mkopo lakini hawataki na hili ni kwa sababu Wizara haiko serious. Tunaomba sana vifaa tiba hivi, x-ray ya hospitali ya Mkoa wa Mtwara iweze kununuliwa na isiwe ahadi kila siku, tulikuwa tunaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia CT Scanner hatuna kwenye hospitali ya Mkoa, CT Scanner haipo sasa ni jambo la ajabu sana. Tumekuwa tunaomba sana, tunazungumza sana, tunaandika sana, namwomba dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu safari hii aweze kuiangalia kwa namna ya kipekee kabisa hospitali ya Mkoa wa Mtwara hospitali hii ya Ligula juu ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala la watumishi. Ukija hospitali ya Mkoa wa Mtwara watumishi wanaohitajika ni watumishi 681, watumishi waliopo Madaktari, Wauguzi na wengine wote ni 255 pekee, upungufu ni zaidi ya watumishi 455. Tunaomba sana Wizara hii ilete watumishi katika hospitali ya Mkoa wa Mtwara, hospitali ya Ligula ili sasa tuweze kupata huduma hizi za afya kama maeneo mengine ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ajabu sana kwenye hospitali hii, tunaye Specialist mmoja pekee, hospitali ya Mkoa inayohudumia Majimbo 10 ya Mkoa wa Mtwara lakini ina Specialist mmoja tu. Naomba Wizara watuletee Specialist hospitali ya Ligula, hospitali ya Mkoa ili na sisi tuweze kupata tiba hizi kama maeneo mengine ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala hili la dawa ambalo limesemwa hapa na hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba sasa hivi upatikanaji wa dawa ni asilimia 85. Pia katika upatikanaji huo amezungumza suala la watu ambao wamepewa misamaha ya dawa, kwa mfano, watoto chini ya miaka mitano, lakini pia watu wenye magonjwa maalum kama vile pressure na kisukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi iliyopo kule ukipitia, ukienda hospitali, ukienda katika zahanati zetu, dawa zikishafika ndani ya muda mfupi tu wagonjwa wanaambiwa dawa zimekwisha waende wakanunue kwenye pharmacy. Sasa unashangaa hii misamaha, mtoto kapewa msamaha, mzee kapewa msamaha, lakini mwisho wa siku wanaambiwa kwamba eti zile dawa hazipo waende wakanunue kwenye pharmacy wakati tumempa msamaha wakati hana uwezo wa kujiendesha, hana uwezo wa kujihudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera inasema wazee kuanzia miaka 60 wapate zile card za matibabu bure, lakini kuna jambo ambalo linatendeka huko wilayani, huko mikoani ambalo naomba usimamizi sana wa Mheshimiwa Waziri kwamba hizi card zitolewe sawasawa na takwimu
zinazotolewa hapa, kwa mfano, pale kwangu takwimu zinasema wazee 1,500 ndiyo wamepewa zile card za matibabu bure, lakini ukienda huko mitaani hata hao wazee kiuhalisia 1000 hawafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kwamba suala la kupewa takwimu ambazo siyo sahihi na Watendaji wa Serikali huko Halmashauri na huko Mikoani Mheshimiwa Ummy Mwalimu uweze kuzipitia na uweze kuhakikisha kwamba takwimu unazopewa kweli ni takwimu za ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la dawa hizi ambazo ni dawa maalum, dawa za kisukari, dawa za UKIMWI na dawa zingine ambazo ni dawa maalum ambazo zinatolewa na Specialist tu. Hapa nimeeleza kwamba Mtwara hospitali ya Mkoa ina Specialist mmoja tu sasa wagonjwa wanatoka wilayani huko, wanatoka kwenye Kata za mbali huko wanakwenda kuchukua dawa hizi kwenye hospitali ya Mkoa. Naomba sana hawa wanaoitwa Medical Assistance hawa wapewe mafunzo na Serikali huko huko waliko hizi dawa ziweze kupatikana, wagonjwa wasiwe wanatembea umbali wa kilomita 80 kuja kufutilia dawa za UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mhesimiwa Ummy Mwalimu kwa sababu tunamfahamu, uwezo huo anao, ahakikishe kwamba analeta mafunzo maalum kwa hawa Specialist kwenye hospitali zetu za Kata, vituo vyetu vya afya ili dawa hizi maalum ziweze kupatikana huko ili wagonjwa wetu wasitembee kwa umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi.