Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia afya njema nikaweza kuchangia Wizara ya Afya kwa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa inayoifanya. Niseme, maendeleo ni hatua kwa hatua. Kama ambavyo kwenye familia zetu huwezi kufanya kila kitu kwa siku moja, leo hii hata ukipata mabilioni ya pesa ukinipa siwezi nikamaliza matatizo niliyonayo na ndivyo ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje hatua kwa hatua ambayo yamefanyika katika Wizara ya Afya. Hatua ya kwanza, upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watoto; hatua ya pili, upandikizaji wa figo na hatua ya tatu, chanjo ya saratani. Hizi ni hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezifanya katika Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba afya zetu zinakwenda kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua hizo, kipekee kabisa naipongeza Wizara ya Afya, Mheshimiwa Ummy na Naibu wake na watendaji wake wote kwa kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kwamba tunakwenda kuboresha na kujenga vituo vyetu vya afya katika kata zetu. Yeye kama mama ameweka historia katika Wizara ya Afya, kama mama ameweka historia katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiishie kupongeza watu walioko juu tu, nampongeza RMO wangu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kazi kubwa anayoifanya kwa sababu mpaka sasa hivi chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa Mkoa wa Shinyanga semina imekwishaanza. Wananchi wa Shinyanga wanapewa semina na hivi tunavyoongea, leo kuna semina inaendelea kwa ajili ya chanjo ya saratani ya kizazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie moja kwa moja sasa katika hoja nilizonazo. Katika hatua ambazo wamepitia Wizara ya Afya, niwaombe NHIF ni kwa nini yale malipo ambayo mmeyaweka kwa vikundi hamtaki kuyaweka kwa mtu mmoja mmoja? Watu wengi hawapo kwenye vikundi,
lakini wana utayari wa kuchangia hiyo shilingi 76,000 kwa ajili ya Bima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri NHIF ruhusuni Bima ya Afya shilingi 76,000 ichangiwe kwa mtu mmoja mmoja na isiwe kwa vikundi. Tunakwenda kuwanyima haki wananchi ambao wako tayari kuchangia Bima ya Afya, kwani vikundi na mtu mmoja mmoja vina tofauti gani? Kwa sababu kama kikundi kina watu 20, mwisho wa siku watu watabaki 20 wale wale. Kwa hiyo, nawashauri muibadilishe iende ikachangiwe na mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashauri NHIF siyo kwamba wananchi wetu ni wagumu kulipa Bima ya Afya, tatizo elimu haipo. Shukeni mpaka kule chini, katoeni elimu kwa wananchi wetu, nini maana ya Bima ya Afya? Mtu akishaugua, ukishaenda hospitali, kama una Bima ya Afya ndiyo utatambua nini maana ya Bima ya Afya na kama hauna, utajuta kwa nini hukuwa na Bima ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawashauri NHIF, shukeni kule chini kwa wananchi wetu na ninawakaribisha Mkoa wa Shinyanga, njooni mtoe mafunzo kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ili waweze kujiunga na Bima ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 118. Ni mwaka wa nane niko ndani ya ukumbi huu wa Bunge, hakuna mwaka ambao sijawahi kusemea Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Nimeangalia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri; ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga haimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa, Mheshimiwa Ummy ni ndugu yangu na rafiki yangu, lakini kwa hili nitakamata shilingi. Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga una miaka zaidi ya mitano toka umeanza. Jengo lililokamilika pale ni jengo la utawala na wagonjwa wa nje. Unawezaje kusema kwamba pale tumekamilisha ujenzi? Nawashauri Wizara ya Afya, hakuna sababu ya kwenda kuanzisha majengo mapya wakati yale ambayo yameshaanza hamjayakamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili iitwe Hospitali ya Rufaa kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kukamilishwa. Kuna jengo la mama na mtoto linatakiwa lijengwe ambalo hatujaanza hata msingi, jengo hili la mama na mtoto litakuwa na maabara na chumba cha upasuaji ndani yake. Kwa nini msitupe angalau shilingi bilioni tatu tukaenda kujenga jengo hilo la mama na mtoto ndani yake kuna chumba cha upasusaji, kuna maabara, ili huduma zikawa zinafanyika pale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo ambalo wanasema kwamba liko tayari la utawala, halina hata furniture moja. Sasa tunakwendaje kutoa huduma za Hospitali ya Rufaa wakati tuna jengo la utawala peke yake? Hapo utasema kuna huduma inafanyika? Hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili naomba Wizara ya Afya litizameni, mkakamilishe ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga ili nisisimame tena hapa kila siku kusema Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga una upungufu mkubwa wa watumishi. Nianze na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Halmashauri hii watumishi wanaotakiwa ni 571; watumishi waliopo ni 196 tu; upungufu ni 375; Halmashauri ya Mji wa Kahama ina upungufu wa watumishi 214; Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ina upungufu wa watumishi 189.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Wizara ya Afya, upungufu huu wa watumishi unasababisha kwenda kutukanwa watumishi wetu wa afya kwamba hawafanyi kazi inavyotakiwa. Hii ni kwa sababu wanafanya kazi kwa kiwango kikubwa. Unakuta mtu mmoja anaandika, anakwenda kutoa dawa, anakwenda kuzalisha mtu huyo huyo mmoja. Matokeo yake, wale ni binadamu, kuna muda unafika mtu amechoka, anaweza akakujibu vibaya mgonjwa ukachukia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili lote lipo ndani ya Wizara ya Afya, liangalieni suala la upungufu wa watumishi katika sekta ya afya, limekuwa ni tatizo kubwa na hivi tunavyokwenda kujenga na kuboresha vituo vyetu vya afya ni lazima tuhakikishe kwamba tuna watumishi wa kutosha, kwa sababu huduma nyingi zaidi zitakuwa zimeongezeka katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, naomba nisemee delivery pack. Kwa uelewa wangu, huduma ya mama na mtoto siyo kwamba imeondolewa kwenda kutolewa bure kule kwenye zahanati zetu na vituo vyetu vya afya kwa sababu ile dawa wanayochomwa akina mama wakati wa kujifungua bado itatoka kama kawaida na gloves zitapatikana kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyoielewa, sijui kama niko tofauti, Mheshimiwa Waziri atasema; nilivyoielewa delivery pack, ni ule mfuko uliobeba vitu vyote ambao unamfanya mama huyu mjamzito aende nao hospitali siku ya kujifungua ukiwa na vifaa vyote tofauti na kubeba kanga na vitenge na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.