Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na uhai. Vile vile napenda kuchangia hii bajeti kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nijielekeze kwenye hoja. Naanza kwa kusema kwamba nimewasikia Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wakisema kwamba ninyi Wapinzani huwa ni watu wa kupinga tu. Siyo kweli, sisi Wapinzani hatupingi kila kitu ila pale ambapo tunaona kabisa Serikali haitendi sawa, tunashauri. Hiyo ndiyo kazi yetu, kusimamia na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, siyo kila kitu tunapinga ila tunapinga kile ambacho tunaona hakiendi sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile msituangalie kwenye ile negative way kwamba Wapinzani hawa; sisi ni kioo chenu ninyi watawala. Wapinzani ni kioo cha Mtawala. Sasa kama utaona kabisa kwamba kioo kinakwambia hapa bwana hujapaka mafuta, halafu bado unabisha kwamba aah, nitakwenda hivyo hivyo, utachekesha. Kwa hiyo, lazima ukiheshimu kikoo chako. Kwa hiyo, Upinzani ni kioo na lazima mkubali kama Watawala, sisi ni vioo vyenu, lazima tuseme pale mnapokosea na mnapofanya sahihi, tunasema kwamba mmefanya sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie bajeti hii kwenye maslahi ya wafanyakazi. Nikiangalia Tanzania tuna makundi makuu mawili, au manne; kuna wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji. Nikiangalia hii bajeti, imewataja wakulima. Ukiangalia kwenye tozo zao wamepunguziwa tukaenda sawa. Wafanyabiashara nao wametajwa, kodi zao nyingi nazo zimeguswa. Wawekezaji nao wametajwa vile vile. Je, mfanyakazi katajwa wapi? Mshahara wake umeongezewa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyakazi huyu sijaona hata sehemu moja mmesema kwamba mnamwangalia kwenye maslahi yake kama hizo posho mbalimbali; au basi hata kama hiki anachostahili kuongezewa mshahara; imepita Mei mosi hapa juzi hatujaona increment yoyote ya mshahara. Tukasema basi bajeti kuu hii tuiangalie labda mtawaongezea wafanyakazi mshahara, hakuna. Vile vile wafanyakazi basi kama hamtaki kuwaongezea mshahara, basi waangalieni makato yao. Bado makato ya wafanyakazi ni makubwa, kuna Pay as You Earn ambayo hiyo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, income tax inasumbua sana. Sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge hapa tunakatwa asilimia 30. Tunalipa kodi kweli kweli, lakini ukiangalia mfanyakazi wa umma naye ana ile two digit sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio cha hawa wafanyakazi hata ukiwasikiliza kwenye vikao vyao ni hii Pay as You Earn kuja kwenye single digit,mnaichukuliaje kama Serikali? Mheshimiwa Waziri, wewe ulikuwa mfanyakazi, usisahau ulikotoka. Wangalie wenzio! Dada yangu Mheshimiwa Angellah vile vile mshauri Mheshimiwa Rais vizuri, awaangalie wafanyakazi hawa, maana yake ni tatizo. Yaani mfanyakazi sasa hivi anajiona kama ni tatizo kufanya kazi. Anaona kama vile yeye ni mtu ambaye anachukuliwa sijui vipi. Watu wote mnawaangalia, lakini bado mfanyakazi anaonekana sijui kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu wafanyabiashara wadogo. Wafanyabiashara wadogo mmesema kwamba mtawatambua. Kwanza napongeza kwa kuwatambua na kuwapa vitambulisho. Hiyo italeta faida gani? Itawafanya hata waende benki kirahisi; lakini unamtambuaje kama hana ardhi; kama hujamtengea eneo? Hivi unamtambua halafu atembee barabarani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam sisi tuna tatizo kubwa sana la wafanyabiashara wadogo wadogo, hawana maeneo sahihi. Basi mtambue, mweke sehemu sahihi pia. Unamtambua halafu anazungukazunguka! Leo yuko Tandika, akigeuka huku, kwenye miji yote mikubwa tatizo ni wafanyabiashara wadogo wadogo. Kama mnataka kweli mwatambue walipe kodi, basi waandalieni na mazingira sahihi. Kwa hiyo, waandalieni mazingira sahihi waweze kufanya kazi zao kama walivyo wafanyakazi wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kodi ya majengo. Kodi ya majengo Mheshimiwa Waziri umeisema. Kuna kodi ya majengo na mabango. Kwanza niseme kabisa, kwa kuchukua kodi hii kwanza kabisa mmepoteza ile zana ya D by D, japo hapa Waziri wa TAMISEMI anatuambia kabisa, mimi ni muumini wa D by D. Basi afanye kwa vitendo! Siyo D by D anaangalia Halmashauri zinanyang’anywa hata bajeti zao saa hizi zimefurugika. Kwa sababu hii kodi ya mabango ilikuwa kwenye bajeti zao. Kwa hiyo, saa hivi ina maana tutavuruga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, kuchukua kodi ya majengo au kodi ya mabango kwenda Serikali Kuu linaweza lisiwe kosa, lakini sasa mngewaachia kule kule. System nzima ya ukusanyaji ingekuwa Halmashauri. Kwa maana wao wenyewe wangekuwa na data na TRA ingekuwa na data. Ninachomshauri Mheshimiwa Waziri, aanzishe Kitengo cha TRA ndani ya Halmshauri zote. Angalau achukue wale wafanyakazi wawili wa TRA waje kwenye Halmashauri wao wenyewe wafanye ile collective responsibility, lakini kazi ya kwenda site, kazi ya kukusanya data, kazi ya kuthamini majengo yote, waachie Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hapa amesema mwenyewe eti nyumba zote atazi-charge kwa flat rate. Ghorofa itakuwa Sh.50,000/=-, nyumba za kawaida Sh.10,000/=. Kwanza kuna ile Urban Authority (Rating) Act ya mwaka 1983. Sijui ameisoma vipi? Sijui inaenda kuwa accommodated wapi? Kwa sababu ile inasema hivi, nyumba yoyote inayochajiwa kodi ni ile nyumba iliyojengwa kwa permanent material au material haya ya muda ambayo ni ya tofali na bati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaponiambia kama huko sijui Chunya au Mbozi huko kwenye Halmashauri hizo za huko ndani; na ile ni Urban Rating inaitwa hivyo; kwa hiyo, kwanza ni kodi ya Mijini. Sasa unaposema kila nyumba Sh.10,000/= mimi sijaelewa. Mpaka hapo labda Mheshimiwa Waziri anitolee ufafanuni akija kuhitimisha. Ana-charge nyumba za udongo? Nyumba za undogo anazi-charge vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri asikwepe jukumu lake, yaani hawezi ku-charge kwa flat rate. Kwanza anaikosesha mapato Serikali. Lazima ufanye uthamini. Uta-charge vipi wewe flat rate? Ghorofa kumi utai- charge vipi Sh.50,000/=? Ghorofa moja uta-charge vipi kwa Sh.50,000/=? Au ata-classify vipi? Sisi atueleze akimaliza hapa, hii flat rate anaifanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachomshauri Mheshimiwa Waziri, apeleke watu wa TRA kwa uchache wao, kwa sababu hawana manpower ya kwenda kila Halmashauri, hawana! Wanachofanya sasa hivi, wanachukua wale wafanyakazi wa Halmashauri wachache wanawapeleka kule. Halmashauri ina manpower, ina Balozi wa Nyumba Kumi, ina Mwenyekiti, ina Mtendaji wa Mtaa. Kwa hiyo, cha kufanya, wale ni watoto wake awalee. Wapelekwe hao watu wa TRA kwenye kitengo maalum kwenye Halmshauri pale, kila Halmashauri wawepo. Kwa hiyo, wao wataangalia ile collection inavyoenda na hao Halmashauri nao watakuwa na data.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye road license. Sisi kwa kweli kilio chetu kilikuwa ni madeni makubwa wanayolimbikiziwa wananchi. Kwa hiyo, tuipongeze Serikali kwa kusikia hilo. Kweli mmefuta, lakini sasa hii 40 mwiangalie tena kwa mapana. Tatizo kubwa bado ni maji. Tatizo la maji bado linatafuta, yaani Tanzania nzima ni issue kwa kweli! Basi kama ndiyo hivyo, hii 40 mchukue asilimia 20 mpeleke kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba kodi hii pia nami niungane na wenzangu isiwekwe kwenye mafuta ya taa, iwekwe kwenye tu kwenye vyombo vya moto. Mafuta ya taa yanatumika kwenye chombo cha moto? Unaweza kuweka kwenye gari! Hii kodi ilikuwa ni kodi ya barabara. Sasa kibatari hakiko barabarani. Mafuta ya taa msiyaingize kwenye kodi hii. Kodi hii iwekeni kwenye diesel na mafuta ya petrol peke yake. Vile vile hiyo Sh.40/= basi mwiangalie na mambo ya maji mnayaingizaje hapo? Kwa sababu hiyo nayo ni huduma sahihi na inatakiwa pia ipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kingine, mmeangalia tu kodi ya majengo, lakini kuna kodi zinazopotea nyingi sana. Kwa mfano, kodi ya ardhi ni chanzo kikubwa mno ambacho kinaweza kikaendesha Serikali nzima hii bila ya kutegemea Wizara nyingine yoyote. Inaendesha Wizara zote; lakini hampangi, hampimi. Hebu wekeni mkakati kabisa wa kupima, kupanga na kuthaminisha ili mpate zile kodi zilizo sahihi. Tukiweza kupata hata asilimia 50 kabisa ya ardhi iliyopimwa hapa, tuaongea mambo mengine, maana ardhi nayo ni madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mlivyosikia kwenye madini, ushauri wetu mkausikiliza mkafanya, naamini kwamba na Mheshimiwa Rais naye atalisikiliza vile vile. Lazima atafute hela apange na apime. Haya nayo ni madini yanayopotea, kwa sababu ardhi kubwa hailipiwi, ardhi haieleweki, ugomvi kila siku, inapoteza mapato ya Serikali. Pimeni, mpange ili mweze kupata mapato. Ahsante.