Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo nami kuweza kuchangia katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri kwa bajeti hii nzuri ambayo ameiwasilisha katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018. Tunashukuru sana kwa sababu bajeti hii sasa inaenda kupunguza ama kuleta picha fulani ya unafuu kwa wananchi wetu ambao tunawaongoza. Nami niseme tu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Manonga, Wilaya ya Igunga pia wananchi wa Mkoa mzima wa Tabora, tumeipokea vizuri sana bajeti hii ya mwaka huu wa fedha, hasa katika kuainisha baadhi ya maeneo ambayo kwa kweli kwa namna moja ama nyingine yanaenda kupunguza makali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa mfano katika uondoshwaji wa hii kodi ya road license, kuna watu watabeza kwa namna moja ama nyingine, lakini niseme tu tumeiondoa kutoka kuilipa moja kwa moja na tumeipeleka kwenye mafuta kwa maana tunapokwenda kununua mafuta ndipo tunakwenda kuilipa kidogokidogo. Hii pia inasaidia kupunguza kero kwa trafiki maana yake Police Traffic walikuwa wanapata usumbufu wa mara kwa mara kusimamisha magari na kukagua kama hawa watumiaji wa magari wamelipia ama hawajalipia, kwa hiyo imewapunguzia kwa namna moja ama nyingine kero ya kusimamisha magari. Naamini kabisa bado tutaendelea kupunguza kero zaidi za hawa Police Traffic itafikia hatua barabarani trafiki watakuwa hawaonekani maana yake tutaweka hata zile kamera zinazoweza kukamata kama ni mwendo kasi na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika bajeti hii, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, katika suala zima ambalo limetokea muda siyo mrefu la makinikia kupitia Wizara hii ya Madini. Hii vita si ndogo kama ambavyo tunaweza tukaichukulia na sisi Wabunge kwa umoja wetu tukiweka itikadi za vyama vyetu pembeni, tuungane pamoja tumsaidie Rais katika jambo hili, vita ya uchumi ni vita kubwa kuliko vita nyingine ambazo tunaweza tukazifikiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vita hii ni kubwa kuliko hata vita ya kudai uhuru wa nchi, kwa sababu vita ya rasilimali ndiyo iliyowafanya hata baadhi ya Marais duniani kuondolewa madarakani. Hii ni vita ambayo kwa namna moja ama nyingine kama Viongozi wa Taifa hili la Tanzania kama tuna mapenzi ya dhati na Taifa hili ni katika sehemu hii sasa tunahitaji kuungana, kusimama pamoja na Mheshimiwa Rais, kumsaidia kuhakikisha kwamba ile dhamira yake safi inatimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wa aina au caliber ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni wachache sana duniani. Hiyo ndiyo napata siri ya kwa nini Mheshimiwa Dkt. Magufuli hajaenda nje ya nchi kwa muda wa miaka miwili sasa. Maana yake unaposafiri kwenda nje ya nchi unakutana na wakubwa, wakubwa hawa watakuomba mambo, mambo mengine wanayokuomba unaweza ukashindwa kuwakatalia. Sasa, sasa hivi kwa sababu tuko katika jitihada za kujikwamua kudai uhuru wetu wa uchumi, sio uhuru wa bendera, uhuru wetu wa uchumi, tupate fedha kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasema Taifa hili linatakiwa liwe donor country, tuwe Taifa la kutoa misaada kwa Mataifa mengine, ni jambo ambalo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina rasilimali nyingi sana, ukiangalia Dubai wana mafuta tu lakini wanaweza kuwa wanafanya mambo makubwa sana, lakini Tanzania tuna kila kitu, kwa sababu tumepata sasa Kiongozi ambaye anaweza akasema bila aibu, bila kupepesa macho, hilo jambo si jepesi, hii kazi tukimpa mmoja wetu tukampa nafasi ile ambayo anaifanya Mheshimiwa Dkt. Magufuli nafikiri kila mmoja anaweza akajificha hapa. Ni jambo ambalo linahitaji uondoe sura ya aibu ndani ya macho yako, sasa inahitaji viongozi na Wabunge tuungane tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua tupo baadhi ya Wabunge tunatumika kusaidia ama kudhoofisha jitihada mbalimbali katika jukumu hili. Hata kama kuna makosa, hayo makosa tuyafanye lakini tuhakikishe kwamba tunapata haki zetu za msingi. Haiwezekani makosa tuyaone tuseme kwa sababu tuna makosa tunaonewa tunaibiwa, tuseme kwa sababu tulikosea, haiwezekani! Tufanye masahihisho katika makosa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo tunamuunga mkono na Wabunge tunahitaji kumuunga mkono na kum- support na kumpa moyo Mheshimiwa Rais, tufikie dhamira ya dhati. Leo hapa Wabunge tunasimama kila mmoja anadai barabara, anadai maji, anadai miundombinu, kila mtu anataka mara afya; fedha zinatoka wapi? Ndiyo hizi fedha za makinikia, ndiyo hizi fedha za rasilimali zetu tulizonazo, tuzidhibiti hizi fedha.Tutakapodhibiti tutaweza kutengeneza fly overs, tutaweza kutengeneza reli ambayo sasa hivi imeshaanza, naipongeza sana Serikali, tumeanza na ujenzi wa standard gauge, hizi zote ili kuhakikisha kwamba tunafikia malengo haya ni lazima tudhibiti rasilimali zetu tupate fedha ambayo itasaidia kujenga miundombinu yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza bado tunaona kabisa katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri tuna ujenzi wa reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam inakuja Mwanza, itapitia Tabora itaenda Kigoma pia in future itakwenda Rwanda, itakwenda Burundi na Congo. Hii yote itasaidia kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua. Tunavyoboresha miundombinu tafsiri yake tunakuza uchumi wa nchi yetu kwa sababu itarahisisha usafiri wa mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, mzigo ambayo ilitakiwa itoke China iende Congo itapita Tanzania kupitia reli hii itakusanya mapato, kupitia mapato haya ndiyo tutatatua changamoto mbalimbali za maeneo yetu tunakotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali katika kuboresha bado tumeweza kuona tumenunua ndege mbili kubwa ambazo zinafanya kazi na bado Serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine, hii yote ni kufufua uchumi wa nchi yetu. Jamani, lazima tuiunge mkono Serikali hii, sasa tusipoiunga mkono mnataka tufanye nini? Kila kitu kukosoa tu, kila kitu kukataa, kila kitu kupinga, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wabunge wa Vyama vyote, Wabunge wa Upinzani wenyewe kazi yao kupinga, haiwezekani. Ifike hatua kwenye mambo ya msingi, masuala ya uchumi tusaidiane, tupeane moyo, ikifika uchaguzi twende tuzungumze kila mmoja anadi yake lakini kwenye masuala ya maendeleo tuungane pamoja ku- support nchi yetu isonge mbele. Ninyi mnasikia furaha gani tunapokuwa na miundombinu mibovu, mnabaki tena mnalalamika, tukija hapa tupitishe bajeti ninyi mnasema hapana! Sasa nashindwa kuelewa ninyi ni watu wa aina gani? Lazima ifike hatua tubadilike, nchi hii inataka tusonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jitihada za Mheshimiwa Rais kwenye ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga, bado kuna watu humu wanapinga. Hebu jamani tuache hizi kasumba za kupinga kila kitu, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, tuiunge mkono Serikali hii mpaka 2020, tukifika kwenye uchaguzi, haya mtaleta sera zenu lakini hapo tayari tutakuwa tumeshapiga hatua mbele ambazo zitahakikisha kwamba tunawakwamua wananchi wetu kuwatoa katika shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengi sana ya kuzungumza lakini pamoja na yote naiomba Wizara kwamba next budget, bajeti iwe imeelekezwa kwa kiwango kikubwa sana kwenye utatuzi wa maji hasa wa vijijini, tuchimbe visima vingi sana vya maji kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo hili ambalo nafikiri kwa namna moja ama nyingine tutamtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama muda wangu utakuwa umekwisha, basi napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi.