Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hakuna Mtanzania yeyote mwenye akili timamu, mpenda maendeleo ya Taifa lake, anayependa Taifa hili, anayeweza kupuuza juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kusaidia kuokoa rasilimali za Tanzania, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Bunge hili wapo Wabunge ambao wana miaka 30, wengine 25, wengine tuna miaka 10. Kilio chetu, miaka yote ndani ya Bunge hili ni juu ya sekta ya madini kugeuzwa kuwa shamba la bibi miaka yote. Kwa miaka yote sekta hii imekuwa hainufaishi Taifa, tumekuwa tunaomba mikataba ije ndani ya Bunge hili miaka yote. Tumekuwa tunapewa majibu na Serikali ilizopita kwamba mikataba ya sekta ya madini ni siri kali. Tulikuwa tunauliza hii siri anafichwa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia sekta hii na namna ambavyo Watanzania hata wale wanaozunguka maeneo ya madini wanavyonyanyasika, wanavyoumia hawana maji, barabara zinabomolewa hawatengenezewi ni suala la uchungu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, yale ambayo tuliyokuwa tunayaomba miaka yote hayafanyiwi kazi, nikiona leo anatokeza mtu, Rais anaweza kuyafanyia kazi angalau kwa hatua za mwisho, mimi binafsi napongeza, napongeza juhudi yoyote kuhakikisha kwamba rasilimali ya Watanzania inanufaisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba maamuzi yote, mapendekezo yote likiwepo la kuleta mikataba Bungeni ije haraka Wabunge tuipitie sisi ni wawakilishi. Unapoingia kwenye nyumba yako hata kwa maisha ya kawaida, ukikutana na changamoto huwezi kutatua zote kwa wakati mmoja unakwenda step by step. Kwa hiyo, tumeanza na hili hapa, ije mikataba yote tatizo kubwa ni kwenye mikataba ndiko tunapopigwa madini, mchanga wa makinikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia hatua kuna mikataba ya madini imekwenda kuingiwa Ulaya, Karamagi hapa alipeleka mkataba Uingereza kwenda kusaini, una mbuzi wako baada ya kuita mnunuzi ndani ya nchi yako unambeba unampeleka kwenda kumuuzia nje ya nchi ulifanyika ufisadi. Kila aliyeweka kidole chake kiwe ni kidole kidogo, kikubwa chochote lazima ashughulikiwe vizuri ihakikishwe kwamba adhabu inatolewa ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hotuba ya Waziri kuendelea kushuka kwa shilingi ya Tanzania. Katika hotuba ya Waziri tumeona kwamba shilingi ya Tanzania inaendelea kushuka na tumekuwa tunazungumza hapa Bungeni hatuoni mikakati kama Taifa, hakuna mikakati ya kuweza kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania na kuporomoka kwa shilingi yetu kunasababisha mambo mengi yanakwenda vibaya, kunasababisha kupanda kwa vyakula na mambo mengine kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashangaa ni Tanzania pekee ambapo dola ya Marekani inauzwa kama njugu mitaani, ni Tanzania pekee ambapo Bureau de Change, vioski vya kubadilisha fedha vipo kila kona kama vioski vya soda. Tanzania pekee unaweza kuona kwamba bidhaa zinanunuliwa kwa fedha ya nje, nendeni nchi nyingine hata hapa Kenya huwezi kutumia shilingi ya Tanzania kununua kitu Kenya huwezi! Tumejisahau kama Taifa na kwa kweli hapa nasema, Gavana wa Benki Kuu ameshindwa kabisa kusimamia kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania, kabisa nasema kila siku, ni kwa nini tunashindwa kusimamia?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunataka mikakati sio kila siku bajeti tunasema kwamba shilingi inaporomoka, tuilinde shilingi yetu tusikubali fedha za nje ije i- overhaul shilingi ya Tanzania. Tunaomba sana shilingi yetu iendelee kupanda ipande kwa sababu inazidi kushuka matokeo yake kama Taifa kiuchumi inaathiri uchumi pia inaathiri maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali ya uchumi, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha hali ya uchumi wa Taifa, ukiangalia mazao mengi ambapo yalikuwa yanaingizia pato kubwa kwa Taifa hii, page 49, mazao mengi yamepungua sana kusafirishwa nje, tukianza na kahawa, kuna cocoa kuna mazao mengi kuna katani, kuna pamba. Kutokusafirisha mazao mengi ina maana uchumi wetu unazidi kwenda chini, kwa nini tunashindwa kusafirisha mazao kwa sababu tumepunguza mapato, mazao yapo kidogo ndani ya nchi yetu kwa sababu hatujaweza kuwekeza vizuri kwenye kilimo hiyo ni ishara tosha, kupungua kusafirisha mazao nje hatuwekezi vizuri na kama hatusafirishi sisi tunakuwa ni masoko kuonyesha kwamba tunauza vitu vya wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kama Taifa tuweze kuinua sekta ya kilimo hakuna namna nyingine. Tuinue sekta ya kilimo tuhakikishe kwamba mazao yote ambayo ukisikia leo Mkoa wa Kilimajaro umeendelea ilikuwa ni kahawa, leo Kagera Bukoba ni kahawa, ndizi, ukisikia Mbeya wameendelea ilikuwa ni cocoa, tumeyasahau yale mazao tumeyaacha. Leo mkulima wa kahawa anang’oa kahawa kwa sababu pembejeo ni ghali hawezi kununua, Serikali haiangalii, kwa hiyo hatuwezi kuinua kilimo kama tunashindwa kuhakikisha kwamba pembejeo zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri amesema amebadilisha mifumo kwa ajili ya kutoa pembejeo, tulikuwa tunatumia mfumo wa voucher ukawa ni hasara kubwa wakulima hawanufaiki. Tukaja na mfumo mwingine Serikali ikasema itaunda vikundi then itoe dhamana benki vikundi vikakope benki, mfumo ule haukutekelezwa, matokeo yake mwaka uliopita mpaka ndani ya Wilaya yangu Kaliua watu hawakupata pembejeo kwa sababu Serikali haikupeleka pembejeo na waliopewa kusambaza pembejeo hawakupeleka kwa wakati. Kwa hiyo, lazima kama Taifa tuwe na mfumo ambao ni endelevu na ni wa uhakika kuhakisha kwamba wakulima wetu wanapata pembejeo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta nyingine ni sekta ya mifugo, Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kuwa na mifugo mingi, lakini kwa bahati mbaya sana mifugo yetu hatujaweza kuitumia vizuri kuongeza kipato cha Taifa. Leo wafugaji wamekuwa wanatangatanga hapa na pale, mifugo imeaachwa inazagaa karibu nchi nzima, hakuna maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya wafugaji, hakuna malisho, hakuna viwanda, hakuna kuchakata mazao yao, hatujaweza kutumia sekta ya mifugo vizuri. Nilitegemea bajeti kama ya leo Waziri angekuwa anatuambia mifugo yenyewe inaingiza zaidi ya robo percent kwa sababu tunayo mifugo mingi inakufa tu, wakati wa ukame inateketea yote kwa sababu hatujaweza kujizatiti vizuri kwenye mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunazo ranchi za Taifa, ranchi zile Serikali haiwekezi chochote, ranchi zimekuwa ni mapori majengo yale yanaharibika, tunaiomba Serikali kama wameshindwa kuwekeza kwenye ranchi za Taifa wayagawe yale maeneo wawape wafugaji, waweze kufungua ranchi zao kule wafuge kisasa Serikali inufaike. Kuacha yale maeneo yanateketea wakati wafugaji wanasambaa nchi nzima, siyo sahihi na wala hatuangalii uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Serikali kubana matumizi au udhibiti wa upotevu wa fedha za Serikali. Serikali imesema huku nyuma kwamba itahakikisha samani zote za Serikali za ofisini, samani zote za ofisi za Serikali kuanzia Serikali Kuu mpaka Local Government wananunua samani kutoka ndani ya nchi. Pia tumeambiwa huko nyuma kwamba watanunua magari ya bei ya kawaida sio mashangingi lakini leo yote hayo hayafanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri atuelekeze ni kwa nini Tanzania hii tuna mbao nzuri, tuna vijana wenye uwezo, tuna viwanda vidogo vidogo wanazalisha samani, Serikali inanunua samani za Kichina ambazo ni low quality ni expensive na hazina ubora, wakati huo tuna viwanda vidogo vidogo ndani ya nchi yetu wanashindwa kununua. Tunao Magereza, tunao JKT, tunao vijana wote wana capacity nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri aje atuambie ni lini Serikali itaacha utaratibu wa kuagiza fanicha/samani kutoka nje ya nchi za Kichina na kuhakikisha kwamba zote zinanunuliwa ndani ya nchi yetu, ili tuweze kutoa ajira kwa vijana lakini pia tuweze kulinda viwanda vya ndani vidogovidogo na hivyo kuweza kuinua uchumi wetu ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya utalii, tunayo rasilimali nyingi sana tuna vivutio vizuri ndani ya nchi yetu, tatizo kubwa hatuwekezi vya kutosha. Ukiangalia hapa Ruaha National Park ni National Park kubwa kuliko nyingine zote Afrika, lakini National Park ile barabara ya kutoka Iringa tu kwenda Ruaha Serikali zaidi ya miaka 15 mmeshindwa. Matokeo yake watalii hawaendi kule. Hebu tuhakikishe tunawekeza kwenye utalii tunavyo vivutio vizuri, leo sio watu wa kushindwa na Kenya, inatushinda kwa ajili ya kipato cha utalii kwa sababu hatuwekezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuvuna pasipo kupanda, lazima tupande tuweze kuvuna. Kwa hiyo, naiomba Serikali tuwekeze vizuri kwenye sekta ya utalii, tuweze kuvuna vizuri kwenye utalii. Nina imani kabisa kwamba kwa vivutio vyetu vilivyo vizuri kuliko nchi zote za Afrika tunaweza tukaingiza kipato kikubwa na hivyo kuongeza uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi, sijaona hotuba ya Mheshimiwa Waziri namna gani ya kuweza kudhibiti au kupambana na mabadiliko ya tabianchi ndani ya nchi yetu. Climate change ni suala la Kitaifa, nchi zote duniani wamejiwekea mikakati kwenye nchi zao kwa njia namna gani ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, leo ndani yetu tunaona jinsi gani tutapata madhara makubwa kwa mabadiliko ya tabianchi, tumeona tetemeko kule Kagera limeua watu, mafuriko kila siku...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)