Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Kamati hizi mbili. Wenzangu wamelisemea sana suala la kilimo ambapo na mimi nawakilisha wakulima, hivyo ni lazima niwasemee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoona, Wizara ni kama imewatoroka wakulima, wamebaki peke yao. Wakulima sasa hawana msaidizi na tumewatelekeza. Mwaka 2017 Mheshimiwa Waziri alitembelea Wilaya yetu na Mkoa wa Rukwa wakati wa masika, tukifikiri analeta suluhisho ama la mazao yetu yaliyokosa soko au pembejeo zilizochelewa. Yote mawili aliondoka bila suluhisho lolote na tukashuhudia uchelewaji mkubwa sana wa pembejeo. Mbaya zaidi mpaka sasa pembejeo hamna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni nilimsikia Mheshimiwa Rais akikemea kwamba maeneo ambayo yanafanya vizuri kwenye kilimo, yapelekeeni mbolea. Siku mbili, tatu watu wakamdanganya Mheshimiwa Rais wakaleta mbolea nyingi Rukwa, lakini hamna mbolea. Leo ninavyozungumza hakuna Urea, wafanyabiashara wanachokifanya, wanatafuta mbolea, wanaagiza malori na lori likisimama tu, mbolea yote inaisha. Hiyo ndiyo habari iliyoko Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu, kilimo sasa mnakiua, lakini mnawatia zaidi umasikini wananchi ambao wanategemea kilimo kwa kila kitu. Hii hatuwezi kukubali, lazima tuwasemee. Serikali msikwepe wajibu; chukueni wajibu wenu vizuri mhakikishe kwamba mnawasaidia wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la maliasili, mwaka 2017 Mheshimiwa Maghembe pia alitembelea Wilayani kwetu na akapata nafasi ya kutembelea kijiji kimoja ambacho kina mgogoro wa ardhi kutokana na uhifadhi. Ninavyosema hivi mpaka sasa migogoro iliyokuwepo wakati
ule haijasuluhishwa kabisa na tumeambiwa hapa kwamba kuna Kamati ya Wizara nyingi ambayo ilikuwa imeundwa kwa ajili ya kuangalia migogoro. Kamati hii haimalizi kazi? Ni lini matatizo ya wakulima na hifadhi yataisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina vijiji vingi, kuna Vijiji vya Kasapa, King’ombe, Mlambo, vyote viko tunaambiwa viko kwenye hifadhi, wakati vimekuwepo tangu enzi. Yote hii ni kwa sababu Kamati hii haijakamilisha kazi yake. Ninaomba migogoro hii iangaliwe, lakini wapo wahifadhi wa TFS, ni wakatili sana kwa wakulima na kwa wananchi wetu. Mkaa hata debe moja akikamatwa nalo mtu anafanywa vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunavyojua, hakuna nishati nyingine mbadala zaidi ya mkaa, tunaweka nafasi gani ya kuwasaidia wakulima hawa wa ngazi ya chini? Mawaziri wetu waliangalie kwa makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wakulima kutofikiwa na barabara za uhakika. Nina wakulima wangu wa Kata ya Kala hawafikiki kwa barabara na wala hawana mtandao wa simu. Maneno haya nimeyasema kwenye Bunge hili katika vipindi vyote viwili na leo nilikuwa naongea na Mheshimiwa Waziri, Kata ya Kala haina mawasiliano ya simu, ni vipi watafikia masoko? Hawafikiki kwa barabara za uhakika, ni vipi mazao yao yataweza kuuzwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu, waone umuhimu wa kupeleka mawasiliano ya simu katika Kata ya Kala pamoja na kutengeneza barabara. Ahsante sana.