Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kupata nafasi hii ili niweze kuchangia hoja za Kamati hizi mbili; Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Kamati ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono taarifa ya Kamati zote mbili. Taarifa imechambuliwa vizuri; na kwa kweli kama Serikali inaweza ikasimamia utekelezaji wa maazimio ya Kamati, tunaweza tukapiga hatua kubwa sana. (Makofi)

MheshimI Mwenyekiti, nizungumzie suala la kilimo, naona kama Serikali imefika mahali inaenda tofauti na wakulima wa zao la mahindi, yaani wakulima wa zao la mahindi wakizalisha, wakianza kupata soko zuri, Serikali inazuia ili wapate hasara, na mimi sijajua ni kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wananchi wangekuwa na fursa ya kuja hapa Dodoma, lugha ambazo wangezisema, Serikali sijui ingesema nini! Sisi tunatumia lugha ya kiuongozi, lakini Serikali ilivyo kwa wananchi ni mbaya mno, wananchi wamepata hasara kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, wananchi hawakuelewi kabisa! Ni kama Wizara hii haipo kabisa! Cha ajabu mwaka 2017 bei ya mazao ilianza kuwa nzuri, wananchi wakaanza kuuza shilingi 70,000 na shilingi 80,000 kwa gunia. Ghafla tu Serikali ikakata mrija, kwamba hamna kupeleka mazao nje. Sasa kilichotokea, wananchi sasa hivi debe moja la mahindi wanauza shilingi 3,500. Gunia shilingi 21,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiuliza Serikali, hivi ina vyombo inavyotizama hali hii? Ina wataalam wanaochunguza hali hii? Hivi Serikali inapata taarifa sahihi za jambo hili? Hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa mahindi wana hali mbaya kupita maelezo. Wamepata hasara kubwa sana. Sasa cha ajabu hata wale waliozalisha kwa sababu hawana maghala ya kuhifadhi mahindi, yamekaa yanaoza, yamepecha, hakuna kwa kupeleka. Sasa mnatarajia nini? Jambo hili linaumiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali mwaka 2017 ilisema itapeleka mbolea mwezi Novemba, lakini mbolea ya kupandia inaenda palizi ya pili, halafu mbolea ya kukuzia inaenda wakati mazao yameshakua, ni kinyume kabisa na matamshi ya Serikali. Na mimi nashindwa kuelewa kama Wizara hii ina wataalamu sahihi kweli, lazima Serikali ifuatilie jambo hili, ni maumivu makubwa sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie maliasili. Kamati imeeleza vizuri sana juu ya mgogoro wa hifadhi na wananchi. Mimi nizungumzie juu ya mgogoro wa Hifadhi ya Uwanda Game Reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanda Game Reserve ramani yake ya kwanza ilichorwa mwaka 1959 ikafanyiwa marekebisho mwaka 1974 kuonesha kwamba reserve inaishia humu. Cha ajabu kuna mgogoro mkubwa sana. Na mimi niseme kwa ujumla kwamba reserve ile imebaki kama ni ya watumishi wa Maliasili, kwa sababu hata ukienda sasa hivi, wamechukua rushwa, mifugo imejaa mle ndani. Sasa hata reserve yenyewe iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nimekueleza juzi kwamba ng’ombe wamejaa, lakini wafugaji wanalanguliwa, bila shilingi milioni mbili au tatu huingizi ng’ombe. Hata ukienda sasa hivi, utakuta mifugo imejaa, hakuna hata maana ya reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu juzi wamemwendea mfugaji mmoja, tena yupo nje ya reserve, wakamwambia tupe hela, akawaambia siwapi hela. Wamefyeka mazao yake. Mimi nimekupa majina ya watumishi hao, lakini nashangaa kwa nini Serikali haichukui hatua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu umeanza toka Waziri wa Maliasili akiwa Mheshimiwa Maige. Ametoka Mheshimiwa Maige, akaja Mheshimiwa Kagasheki, ametoka Mheshimiwa Kagasheki, akaja Mheshimiwa Nyalandu, ametoka Mheshimiwa Nyalandu akaja Mheshimiwa Maghembe juzi ameenda kujionea, akakuta kweli wananchi wanaonewa. Akatoa suluhu kwamba atatuma wataalam wake kwenda kumaliza jambo hili, lakini mpaka sasa jambo hili bado linaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ajue, akitaka aondoke hata sasa hivi, atakuta reserve hii imejaa mifugo, wala haieleweki. Kwa hiyo, vitu vingine hivi vinafanya wananchi wapate hasira kubwa sana. Ipo siku moja mtashuhudia mauaji ya ajabu, jambo ambalo siyo zuri kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Waziri wa Maliasili, kama atapata nafasi, aondoke hata kesho aende akajionee hali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wanyama waharibifu. Juzi mamba amekamata mwananchi mmoja Mto Momba. Tumetoa taarifa Maliasili; Maliasili hawana habari, kwa sababu wanajua kwenda kumuua mamba hawapati rushwa, wamekaa tu wanaangalia. Mimi mwenyewe nimewajulisha, lakini hawana habari na mamba yule bado anavizia wananchi katika Kijiji cha Kipeta na Kinyamatundu. Kwa hiyo, naomba, kwa sababu Mheshimiwa Waziri umesikia, jaribu kuwapigia simu waende wakatatue tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yalikuwa ni hayo tu. Ahsante.