Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. JOSEPH MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nitazungumzia kidogo suala la uvuvi. Wabunge wengi tuliomo humu kila mmoja ana neema ambayo Mwenyezi Mungu amempa na kila mtu ana kitu ambacho wananchi wake wanakitegemea. Jimbo la Geita Vijijini sisi dhahabu yetu kubwa ni uvuvi lakini toka nimezaliwa sijawahi kuona hizi sheria zinazotumiwa na Mheshimiwa Mpina. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umri wangu huu nimeshuhudia Mawaziri awamu zote, nafikiria sasa ndiyo tunaanza kutunga sheria au hii sheria ilikuwa imefichwa sasa ndiyo imeibuka. Nataka kutoa rai kwa Mawaziri kwamba Mawaziri wa dizaini kama hizi nawashauri sana mpunguze mihemuko kwa sababu hata sisi tunatamani kuendelea kuwa Wabunge humu ndani, lakini kwa dizaini mnazoenda mtuambie mmewapanga kina nani mnaotaka wakae Wabunge kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza kwa Wabunge wanaotoka Kanda ya Ziwa; Mheshimiwa Lwakatale, Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Tibaijuka, Mheshimiwa Kalemani, Mheshimiwa Lolesia, Mheshimiwa Musukuma, Mheshimiwa Kanyasu, Mheshimiwa Mabula wa Mjini, Mheshimiwa Mabula wa Ilemela, wa Magu, tunaenda kwa Mheshimiwa Bulaya, unaenda kwa Mheshimiwa Airo Musoma, sidhani kama sisi tutarudi humu Bungeni. Sijawahi kuona Waziri anasimama anasema mimi kwetu hakuna samaki natamani wote tusile samaki, Mungu ametupa neema tofauti. Sijawahi kuona unaenda unakamata mitego dakika 10 unaomba faini mtu hana unachoma, hujahakikisha ni ile feki unayoitafuta au original. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Jimboni kwetu na huko kwenye Majimbo ya Kanda ya Ziwa debe la dagaa linauzwa Sh.50,000 yaani maana yake hata dagaa haturuhusiwi kula. Ukisikiliza madaktari wanatuambia tukila dagaa tunaongeza madini joto, akija Mpina anasema ni haramu, tufuate la nani? Namwomba Waziri Mpina atakapokuja hapa atuambie ni sheria zipi anazozitumia kama siyo mihemuko. Kwa sababu hata Mheshimiwa Rais aliyepo sasa hivi Magufuli alikuwa Waziri aliunda BMU watu wakawa wanafundishwa na uvuvi haramu ukaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda kwenye maeneo yetu hakuna samaki inayotakiwa kuliwa. Nina mfano halali, mimi nafanya biashara ya mabasi, basi yangu imesimamishwa na watu wa Maliasili wakaingia ndani kukagua wakakuta mtu ana samaki za kukaanga tatu naombwa kutoa Sh.10,000,000 na nimempigia simu Mpina anasema watu wangu wanasema sijui wamefanya nini, nikawaambia chukueni gari mkauze. Hivi inawezekana vipi watu wa mabasi anakaa ruler yake kupima samaki kwamba hii samaki inatafutwa na Mpina, kwa nini usiweke polisi stendi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mpina pamoja na apizo alilolifanya kwamba asipomaliza uvuvi haramu atajiuzuru, mimi nakwambia…

T A A R I F A . . .

MHE. JOSEPH MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru. Anataka kukaa kwenye Youtube kwamba alimpa taarifa Musukuma. Tunajua Jimboni kwako unazomewa, kwa hiyo, unatafuta kick unatetea wanyonge. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ninachoomba Waziri Mpina pamoja na timu yake wajipange kuwafundisha wavuvi wetu kule siyo kuwafilisi. Nataka nitoe ushahidi mdogo tu kwamba Waziri Mpina wameenda kisiwa kimoja kule Izuma Cheli Jimboni kwangu wakakuta watu wameunda SACCOs wamekopa wanadaiwa shilingi bilioni 1.4, mitego ndiyo wameishusha usiku huohuo asubuhi imekamatwa hata kuombwa risiti wamenunua wapi ili wakapambane nao na siyo haramu imechomwa moto kwa kukosa rushwa ya shilingi milioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Waziri na wengine wanaosikiliza kwamba nashauri sana zoezi analoliendesha Waziri Mpina lazima liundiwe Tume iende ikachunguze na tuone hizo hela watu wetu walizotoa kama zimetolewa risiti za Serikali. Tuna ushahidi wa watu waliofanyiwa uhuni kwenye Majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine yanauma sana, unajua wengine humu ndani hawana hiyo bahati ya kuwa na ziwa, naamini hata Jimbo la Mheshimiwa Waziri wao wanakulaga panki zikikatwa kule kwetu wao wanapelekewa mapanki. Sasa asitake kutufananisha yaani sisi tufe njaa na ziwa liko pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waje na shule maalum itakayotufundisha, hata sisi hatupendi uvuvi haramu lakini siyo kuzuia kila kitu. Kwa sababu kwanza kule ziwani hata ukizuia tusivue sisi Watanzania hakuna barrier samaki wataenda Kisumu, samaki wataenda Uganda na ndiyo kinachofanyika. Rais Magufuli anasema tufanye kazi, tukuze uchumi wetu, mwingine anaenda kusema choma kila kitu, wavuvi wote wa Kanda ya Ziwa wamehamia Uganda na Kenya sasa nani anapata faida? Nyie ziwa lenu mmekuwa mnatunisha samaki wakikua wanatembea wanaenda Kisumu tunavua tunauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri sana Mheshimiwa Mpina utakapokuja kujibu hapa na hata ukichomoa hapa kwenye bajeti tutakutana lazima utueleze ili hii operesheni ya uonevu inayoendelea ikome.