Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara yenye majukumu muhimu katika maendeleo ya nchi yetu. Sisi kama Wabunge tuna wajibu wa kuwakumbusha na kuwashauri. Majukumu ya Wizara hii ni kama ifuatavyo:-

(i) Kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na nje ya nchi pamoja na matumizi yake;

(ii) Kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera za uchumi na kijamii kwa ujumla;

(iii) Kuandaa na kutekeleza bajeti ya Serikali;

(iv) Kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kupunguza umaskini katika sekta mbalimbali;

(v) Kusimamia Deni la Taifa na upatikanaji wa rasilimali fedha;

(vi) Kusimamia Tume ya Pamoja ya Fedha;

(vii) Kulipa na kuandaa watumishi Serikalini;

(viii) Kudhibiti biashara haramu ya fedha pamoja na ufadhili wa ugaidi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sasa umefika kwa Serikali kulipa deni la ndani. Kwa kulipa madeni ya ndani itatufanya tuweze kuendelea katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kutimiza vizuri mikakati tuliyoiweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upatikanaji wa fedha kutoka Hazina limekuwa ni la kuchelewa sana. Kwa muda mrefu sana sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikichelewesha sana kupeleka fedha kwenye Wizara na Idara mbalimbali za Serikali kama zilivyoidhinishwa na kufanya shughuli za kimaendeleo kushindwa kufanyika na kushindwa kutimiza malengo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Muungano ni changamoto ya muda mrefu. Iko wazi kabisa kwa kuwa kuna mamlaka tatu ambazo ziko dhahiri wala haziepukiki lakini imekuwa utamaduni fedha za Muungano kutumiwa na Tanganyika wakati Zanzibar ikikoseshwa fedha hizi ambazo ziko kisheria. Hivyo, tunaiomba Wizara ya Fedha kupitia Serikali kutatua kero hii ya muda mrefu na mamlaka hizi zipewe haki zake na zionekane ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya mazingira imetengewa fedha kidogo sana ukizingatia mazingira ni eneo muhimu kwa maisha ya viumbe vyote vyenye uhai. Kwa hiyo, nashauri sekta hii iongezewe fedha ili iendane na hali halisi ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti naishauri Serikali kupunguza utitiri wa kodi kwa wananchi na wafanyabiashara. Jambo hili linapelekea biashara nyingi kufungwa na Serikali kukosa mapato ya kuendesha nchi yetu. Pia Serikali ifike mahali ifahamu kwamba katika biashara ya kila Mtanzania Serikali ni shareholder kwa asilimia 30% hivyo iwawezeshe wafanyabiashara wafanye biashara ili kuendeleza biashara na kuleta pato kwa Tanzania badala ya kuwafukuza na kufunga biashara na Serikali kukosa mapato kwa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwe inatekeleza ahadi zake na utekelezaji uonekane. Hii imeonekana kwani mwaka jana Serikali iliahidi kugawa EFD machine kwa wafanyabiashara lakini mpaka leo haijagawa machine hizo. Hili linarudisha nyuma maendeleo ya umma. Pia napenda kujua ni utaratibu gani unatumika kugawa EFD machine na watu gani wanapaswa kutumia hizi EFD machine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakiki madeni ya watumishi na watoa huduma. Bado tunasisitiza Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea kuhakiki na kulipa madeni mbalimbali ya ndani hasa watumishi, wakandarasi, wazabuni na watoa huduma wengine ambao baadhi yao walikopa benki kupata mtaji ili waweze kutoa huduma kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.