Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja ambayo imewasilishwa na Serikali hapa Bungeni. Kwanza naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani ambayo yamechambua na kutoa mapendekezo mengi. Hapa ndani ya Bunge upande wa pili mmekuwa na mtazamo wa kuona kwamba hatushauri lakini kuna ushauri mwingi sana umetolewa na mapendekezo mengi, naamini Serikali mtaichukua na kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa maoni yangu kuhusu utekelezaji wa bajeti ambayo tunaimalizia. Bajeti ya mwaka 2016/2017 tulipitisha shilingi trilioni 29 kama bajeti ya jumla lakini katika hizo shilingi trilioni 29 mpaka tunapoongea ni takribani asilimia 38 tu ya fedha zote ndiyo imeenda kwenye miradi ya maendeleo. Katika fedha hizi za miradi ya maendeleo ambayo Serikali mmepeleka ni kama ifuatavyo kwa ufupi kwa mujibu wa kitabu cha Waziri. Ujenzi na ukarabati wa barabara imepelekwa shilingi bilioni 675, miradi ya uzalishaji wa umeme shilingi bilioni 441, malipo ya awali ya ujenzi wa reli shilingi bilioni 300, usambazaji wa maji vijijini shilingi bilioni 186 na huduma za afya ni shilingi bilioni 170.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajiuliza hata hizi fedha tu za miradi ya maendeleo ambayo imepelekwa kwa asilimia chache kiasi hiki, zile ambazo ni muhimu kwa afya za Watanzania ikiwemo afya, maji imepelekwa kidogo ukilinganisha na hizo nyingine za ujenzi na ukarabati wa barabara. Kwa hiyo, unaona kabisa hata umuhimu wa kuwapa Watanzania hizi huduma muhimu za maji na afya haupo na wala hazipewi kipaumbele.

Kwa hiyo, Waziri sasa hivi tunaposema hata hii pia hamtaweza kutekeleza tunamaanisha kwa sababu ya maneno yenu ambayo mmeyaandika humu kwenye hivi vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ya 2017/2018 ambayo sasa tunaitarajia kuanza, mnakisia maoteo ya bajeti itakuwa shilingi trilioni 31.7. Kama hii tunayoimaliza ya shilingi trilioni 29 haijatekelezwa hata kwa asilimia hiyo, je, hii tunayoiendea itatekelezwa? Mnawahadaa Watanzania kwa kuwaambia kwamba hii bajeti haijawahi kutokea, ni bajeti ya karne, mimi naamini ni kweli itakuja kuwaumiza Watanznaia kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati mnafanya bajeti hii kufikia shilingi trilioni 31 maana yake bajeti hii ni shirikishi kuanzia Serikali za Mitaa, watu wamepanga kwa mfumo wa O&OD, wakaibua, wakapanga, tukapitisha kwenye Halmashauri zetu, zikapita kwenye process nzima za kibajeti mpaka Serikali mkaja Bungeni mkasema kwamba bajeti ni shilingi trilioni 31. Sasa muone mnavyojikanganya, hii shilingi trilioni 31 ni pamoja na mapato ya ndani ya Serikali za Mitaa kwa sababu bajeti imeanzia kule chini. Halmashauri zetu zimesema zitakusanya ushuru mbalimbali kama mapato ya ndani baadaye mkafanya compilation mkatuletea bajeti ya shilingi trilioni 31 lakini mnatuletea bajeti ya shilingi trilioni 31 huku nyuma mnafuta vyanzo vingi vya Serikali za Mitaa ambavyo tayari mmeshaweka kwenye bajeti yenu. Mheshimiwa Waziri hiki unachokisema shilingi trilioni 31 hautakaa utekeleze kwa sababu umesahau vyanzo vingine umevifuta wakati viko kwenye bajeti ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unatuambia bajeti zimefutwa, kwanza kuanzia miaka ya 2000-2010 Serikali mlifanya maboresho ya Serikali za Mitaa kwa kuziboresha kwa kuweka mfumo ya O&OD, mkasema mnagatua madaraka, mnaziachia Serikali za Mitaa ziwe na madaraka kamili, zikusanye mapato yake, zijiendeshe, leo mmegeuka baadhi ya mapato mnayachukua, mengine mnayafuta bila kuzishirikisha Serikali za Mitaa, hamtambui umuhimu wa Serikali za Mitaa? Mheshimiwa Waziri Serikali za Mitaa ziko kwa mujibu wa Katiba ya nchi kwanza mnavunja hata hii Katiba ya nchi. Leo umekuja unatuambia umefuta ushuru wa huduma (service levy), Halmashauri zetu nyingi jamani zinategemea ushuru wa hizi guest house na zimeshaweka kwenye bajeti yake. Leo unafuta ada ya machinjio, Halmashauri zetu ndiyo zinategemea ipate hizo ada, umefuta ada ya makanyagio minadani Halmashauri nyingi za vijijini ndiyo zinategema hii ada, umeondoa kodi ya mabango umeichukua umepeleka TRA halafu unasema utazirudisha, hamrudishagi mnatudanganya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema mmepunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano mpaka asilimia mbili kama ni mazao ya chakula na biashara lakini Mheshimiwa Waziri unasahau kwamba Halmashauri zetu tayari zilishaweka fedha hizi kwenye bajeti yao kwa nini mnawadanganya Watanzania? Halafu nitashangaa sana Waheshimiwa Wabunge wa CCM mkiendelea kusema mnaunga mkono hoja, Halmashauri zenu mtaona tukianza mwaka wa fedha hazitakuwa na fedha kwa sababu vyanzo vingi vimefutwa na Serikali Kuu na tayari walishaweka kwenye bajeti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mnaenda kuua Serikali za Mitaa au basi mseme kwamba Serikali za Mitaa hazipo tena, mfanye vitu vyote. Mmekuwa mkiahidi mara zote kwamba mtarudisha hizo fedha na hamjawahi kurudisha. Mheshimiwa Susan Lyimo amesema hapa Kodi ya Majengo tu, mliahidi mtarudisha hamrudishi hata senti tano. Sasa Serikali za Mitaa zitawezaje kwenda kujitegemea na kufanya shughuli zake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Kodi ya Majengo. Serikali ya Awamu ya Tano mlichukua kodi hii ya majengo mkasema TRA inakusanya. Juzi niliuliza swali la nyongeza hapa Bungeni kwa Mheshimiwa Waziri Simbachawene, nikataka kujua kauli ya Serikali ni majengo yapi hasa ambayo yanatozwa kodi hii kwa sababu kwenye Wilaya zetu mpaka nyumba za tembe, nyumba za udongo zinatozwa kodi hii. Mheshimiwa Simbachawene akanijibu hapa akasema majengo yatakayotozwa kodi ni yale yanayotengeneza faida kwa maana ya nyumba zinazofanya biashara. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukasimama ukaniambia kuwa subiri bajeti yangu tutasoma, sasa hii bajeti yako ukurasa wa 48 inasema hivi; “Serikali itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum (flat rate) cha shilingi 10,000 kwa nyumba na shilingi 50,000 kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni zile ambazo hazijafanyiwa uthamini, kati ya shilingi 10,000 mpaka shilingi 50,000, acha zile zingine ambazo zitafanyiwa uthamini. Mheshimiwa Waziri hamuoni ninyi wenyewe mnajikangaya kwenye kauli zetu? Mheshimiwa Simbachawene amesema ni zile ambazo zinaingiza faida, akasema unaweza kwenda vijijini ukakuta mtu ana guest house na kadhalika huyo sawa atozwe kodi lakini wewe unasema nyumba zote, maana yake unasema hata za tembe nazo zitozwe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnasema hii ni bajeti ya kuwakomboa Watanzania au kuwanyonya Watanzania? Mnathubutu kusema kwamba hii bajeti haijawahi kutokea ni bajeti ya karne, hii haiwezekani hata kidogo. Nitawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wa CCM mkasome tena upya hii bajeti yenu ambayo mnasema eti inaenda kumkomboa Mtanzania wakati siyo kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Road License. Wamepongeza sana hapa Wabunge wenzetu wa upande wa pili lakini tunajiuliza hivi ni Watanzania wangapi kati ya Watanzania milioni 40 ambao wana own magari? Inawezekana ni asilimia tano ya Watanzania wote, sasa asilimia tano ya Watanzania wote hawa leo mmewaondolea Road License ambayo watalipa kwa mwaka, mnasema mnapeleka kodi hii kwenda kutozwa kwa shilingi 40 kwa kila lita moja ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunafahamu ukiweka ongezeko lolote kidogo kwenye kila lita ya mafuta nchi hii, kila kitu kinapanda bei. Kwa sababu mafuta yanahusiana moja kwa moja na masuala mengine, utakuta bidhaa zinapanda sokoni, ukisafirisha mazao bei inapanda na kila kitu. Sasa kwa nini tuwaadhibu Watanzania wengine walio wengi ambao hawamiliki vyombo vya moto kwa sababu hawalipii Road License halafu tunawaacha hawa asilimia 5 tu tunawapa msamaha huu wakati itawagharibu Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali ya Awamu ya Nne ya JK...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)