Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono mawazo mazuri ya Kambi Rasmi ya Upinzani hapa Bungeni kwa namna ambavyo wameichambua kwa kina bajeti hii lakini kwa kutoa mawazo mbadala ili Serikali waweze kuyachukua na kuiboresha bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa naamini siyo jambo geni kwa Serikali kuchukua mawazo ya Upinzani na kuyafanyia kazi kwa sababu hata Mheshimiwa Rais ameanza kuonesha njia kwa kuyachukua yale mawazo mazuri ambayo upande wa Upinzani tukiyatoa na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze sana viongozi wetu wa Kambi kwa pamoja Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa James Mbatia na Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali kwa namna ambavyo wanatu-groom vizuri ili tuendelee kutoa michango hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami pia ni miongoni mwa wanaoshangazwa na bajeti hii. Kama ambavyo mnasema bajeti ya kihistoria maana yake imeduwaza wengi na mimi pia ni miongoni mwa watu ambao tumeduwazwa na bajeti hii hasa kwa kutotarajia kuona kwamba bajeti ingeongezeka kufikia shilingi trilioni 31.7 wakati ya ile shilingi trilioni 29 tulishindwa kufikia. Naona ni kama vile mgonjwa ambaye ameshindwa kunywa uji sasa tunampatia pande la mhogo. Kwa mtazamo huo unaona kabisa tunatengeneza bajeti ambayo hatuwezi kwenda kuitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifikiri baada ya kuona kwamba bajeti ya 2016/2017 tumeshindwa kuitekeleza hata kwa asilimia 40, Serikali ingerudi nyuma na kujiuliza wapi ilikosea. Kwa sababu unapokuwa na bajeti ambayo unashindwa kuifikia maana yake ama mli-overestimate kwamba makadirio mliyoyafanya yalikuwa makubwa kuliko uwezo halisia. Kwa hiyo, nilitegemea leo bajeti yetu ishuke kwenye shilingi trilioni 29 iende kwenye uhalisia badala ya kuipandisha kuipeleka kwenye shilingi trilioni 31.7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu moja ya vitu ambavyo vimechangia bajeti yetu 2016/2017 ku-fail ni mazingira mabovu tuliyonayo sasa kati yetu na wahisani wetu. Mazingira hayo bado hayajaondoka, mazingira yetu hayawavutii wahisani kuendelea kutupatia zile fedha ambazo walikuwa wakiahidi. Kwa hiyo, maana yake hata kwenye bajeti hii tunayoendelea nayo na yenyewe itapata changamoto zilezile ambazo bajeti ya 2016/2017 ilizipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wahisani hawaridhiki na uchaguzi wa Zanzibar ulivyoendeshwa. Tuliyasema haya wakati tunachangia bajeti ya 2016/2017, kwamba haya mazingira yaangaliwe. Tumekuwa tukijinasibu kwamba sisi ni kisiwa cha amani, kisiwa cha utulivu lakini kiukweli mazingira ya siasa za Zanzibar hayaoneshi kama kweli sisi ni watulivu na tuna amani kiasi hicho. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri ili yale makandokando yaliyozunguka yaweze kuondoka na wahisani hawa waendelee kutuamini na kutuletea misaada yao kama ambavyo ilikuwa hapo awali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili mambo mengine haya ya kuiminya demokrasia. Bado demokrasia katika Awamu hii ya Tano imeendelea kuminywa hapa nchi, tunazuiwa kufanya mikutano ya kisiasa. Kwa mfano, mikutano ya kisiasa ipo kwa mujibu wa sheria. Sheria iliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi inavitaka vyama kuendeleza mitandao yao huko nje. Leo mnaambiwa kwamba msifanye mkutano ya kisiasa kwamba kila mtu afanye mkutano kwenye eneo lake aliloshinda.

Mheshimiwa Spika, tuna vyama vilivyosajiliwa zaidi ya 22 si kila chama kimeshinda uchaguzi, kuna vyama havina hata mjumbe wa Serikali ya Mtaa, huyu akafanyie wapi siasa yake? Kwa nini huyu abanwe kufanya siasa? Kwa nini tutenge kwamba watu walioshinda tu ndiyo wafanye siasa wengine wakafanyie wapi? Ni lazima na wao wafanye siasa ili uchaguzi ujao waweze kushinda wapate wawakilishi kwenye nafasi hizo. Sasa tunapowanyima nafasi watu hawa tunaiminya demokrasia kwa upana wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi wasiwasi uko wapi, kama sisi Wapinzani tunasema uongo tufanye kwamba CUF tumefanya mkutano pale Mwembe Yanga Temeke tukasema kwamba maisha ni magumu kwa Watanzania, si kesho CCM na wenyewe wafanye mkutano Jangwani waseme maisha ni mazuri. Kwa sababu hii siasa tunayoifanya ni vita ya maneno tu, hasira zinatokea wapi? Mwenzio akisema hivi na wewe sema lile unaloliona la ukweli, halafu wananchi watakwenda kutupima 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niishawishi Serikali na naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri amepata Uwaziri kama mtaalam na siyo kama mwanasiasa japokuwa ameanza kuonesha interest za kulitaka Jimbo la Buhigwe, nikutakie kila la kheri, lakini kwenye haya mambo ambayo ni ya kisiasa lakini yanaharibu uchumi aiambie ukweli Serikali kwamba tubadilishe mazingira haya wahisani hawa waendelee kutusaidia, lakini akiyakalia kimya mwisho wa siku mzigo unakuja kubebeshwa wewe. Watu wanaamini Mheshimiwa Waziri ni mtaalam mzuri sana, amefanya kazi ya kuishauri Serikali ya Awamu ya Nne na ilifanya vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iweke mazingira sawa ili wahisani waendelee kutoa zile pledges zao kama walivyokuwa wanafanya kwenye awamu zilizopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ahadi za Mheshimiwa Rais, naamini kabisa Serikali hii inafanya kazi za kumsaidia Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameahidi kwenye kampeni zake kutoa milioni 50 kwenye kila mtaa.

Tunakwenda kwenye bajeti ya mwaka wa pili huu hiyo milioni 50 haionekani, huku ni kumgombanisha Mheshimiwa Rais na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama wana wasiwasi wa utekelezaji wa hiyo ahadi wangechagua hata pilot regions au districts kwamba hizi wilaya mbili au tatu tupeleke hizo milioni 50, tuzisimamie tuone utekelezaji wake utakuwaje. Hata Watanzania wangeona ile nia ya kweli ya kutekeleza ahadi hiyo, lakini wamekaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais pia aliahidi kutoa laptop kwa Walimu wote leo tunakwenda kwenye bajeti ya mwaka wa pili huu, tumepitisha hapa Wizara ya Elimu, Wizara ya TAMISEMI hakuna hata moja imetenga fedha kwa ajili ya hizo laptops za Walimu na hii ni bajeti kuu pia hili halizungumziwi. Kwa nini tunamgombanisha Mheshimiwa Rais na wananchi wake? Naitaka Serikali imsaidie Mheshimiwa Rais kutekeleza ahadi zake ili aendelee kunukia na kupendeza mbele ya macho ya watu aliowaahidi na walimpa kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nataka kuchangia hapa ni namna ambavyo Serikali inazidi kupoka madaraka kutoka kwenye Serikali za Mitaa. Mwaka jana wametuchukulia Property Tax kibaya zaidi siyo kuzichukua hizo Property Tax lakini hazikukusanywa. Mpaka tarehe 31 Machi, Serikali ilikusanya asilimia 20 tu katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hata hao watumishi wenyewe wa kwenda kukusanya TRA hawana kwa maana hawajajipanga, wanaazima humo humo kwenye Halmashauri ndiyo wapate watu wa kwenda kuwakusanyia. Kama walikuwa hawajajipanga kwa nini wanalichukua jukumu hili, kwa nini wasiendelee kutuachia sisi tukakusanya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hapa badala ya kujikita kwanza wajipange vizuri kwenye kukusanya Property Tax

wameongeza na mabango pia maana yake wanakwenda kuziua Halmashauri zetu kwa kutunyang’anya vyanzo vya mapato.

Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja hii.