Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa na nzuri inayofanyika katika kufanya mabadiliko kwenye maeneo mbalimbali ambayo tumekuwa tukiyalalamikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa baadhi ya Wabunge ambao nimesikia hapa wakijaribu kutuelekeza namna ya kusema; nawaomba wasifanye hivyo, kwa sababu Wabunge hapa tuko wengi, nchi yetu ni kubwa na mazingira yanatofautiana sana. Kwa hiyo, mawazo ambayo nitayatoa kutokana na mazingira yangu ya Msalala ni tofauti sana na mawazo ya Mbunge mwingine. Kazi ya Serikali ku-coordinate na kuweza kuchukua hatua za kurekebisha pale ambapo pana marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba mambo yaliyofanyika ni makubwa. Changamoto zilizoko kwenye kilimo ni kubwa sana, lakini hatua zinazofanyika zinaonekana. Tumelalamikia sana kwa mfano suala la tozo mbalimbali, kwamba linaumiza wakulima. Hatua zimechukuliwa, tumeona, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi kumekuwa na tatizo kubwa sana la uratibu na usambazaji wa mbolea. Mpango na utaratibu uliokuwepo kwa miaka yote ulikuwa unasababisha matatizo makubwa ya upotevu wa fedha za Serikali, lakini kubwa zaidi hata usambazaji wenyewe ulikuwa unafika wakati mbolea inasambazwa kwa kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa hatua iliyochukuliwa ya sasa ya kufanya uratibu na usimamizi wa ununuzi wa mbolea kwa kutumia huu mtindo wa bulk procurement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuunge mkono wazo hili, naamini litatusaidia. Tumekuwa na matatizo, hii ni hatua mojawapo ya kupata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushauri wangu kwenye hili eneo la mbolea ni kwamba ni lazima sasa kwa sababu mbolea itaagizwa na sekta binafsi ni lazima Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuthibiti bei; kama ilivyo kwenye mafuta kwamba wanaagiza na wanaelekezwa bei ya kuuzia kwenye maeneo mbalimbali watakayosambaza, pia bei elekezi ya mbolea itakayosambazwa iweze kutolewa na hao wasambazaji na mawakala wao kwenye hayo maeneo, waweze kutangazwa na wajulikane kwamba Wakala wa Mbolea kwa eneo kwa mfano kwangu Kahama ajulikane ni fulani na bei yake itakuwa ni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nishauri hivyo kwenye eneo la mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika utangulizi, mimi natoka Mkoa wa Shinyanga. Mkoa huu kwa miaka yote tumekuwa tukilalamikia tatizo la njaa. Naomba nifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba hata sasa hivi Mkoa wa Shinyanga hali ya chakula hairidhishi. Tumetoka kwenye kipindi chenye changamoto za mvua za vuli mwezi, Novemba, Disemba, zimenyesha kweli. Kufika mwezi Januari, mvua zilikata kabisa na sehemu kubwa waliokuwa wamelima mahindi, hasa Wilaya ya Kahama, mahindi yote yalinyauka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa mvua za masika zimeanza kunyesha tena mwezi wa Pili, wakulima wakajaribu tena kulima kwa mara nyingine, lakini cha ajabu kukatokea funza! Siyo viwavijeshi, lakini ni aina fulani ya funza wa ajabu sana ambao wameharibu mazao yote. Mheshimiwa Waziri tuliongea kwamba moja ya tatizo kubwa tulilolipata kama wananchi na wakulima ni kutokupata mwongozo wowote kutoka kwa Maafisa Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi walikuwa wanahangaika kukabiliana na hawa funza bila kujua watumie dawa gani? Wapo waliokuwa wakishauriwa watumie sabuni na kuchanganya na majivu, haikusaidia; wapo walioelekezwa kutumia dawa za mifugo, haikusaidia; na mwisho mazao hayajapatikana. Kwa hiyo, naomba katika msimu ujao wa kilimo ni muhimu Serikali kuwa imeshajua tatizo la hawa wadudu ni nini? Au hao wadudu ni wa aina gani? Dawa gani itumike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoiomba Serikali hapa, siyo lazima itununulie dawa, ielekeze tu kwamba wadudu hawa wanauawa kwa dawa hii, wakulima tumieni dawa hiyo. Itawasaidia sana wakulima. Watu wa Shinyanga ni wakulima wazuri, wala hawahitaji kusukumwa kwenda shambani. Kwa mazingira tuliyonayo kwa sasa, kabla ya kufika msimu ujao wa kilimo, tutakuwa na tatizo la njaa. Nilikuwa naiomba sana Serikali, kumekuwepo na utaratibu wa Serikali kusaidia mbolea kwa miaka ya nyuma na kusaidia kuwezesha maeneo mengine ambayo mvua zinanyesha, wazalishe kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtizamo ni kwamba huko wanakozalisha, mikoa ile ya G5 Iringa, Morogoro, Rukwa na kadhalika, wazalishe kwa wingi. Halafu baada ya kuwa wamezalisha chakula kile kiweze kuuzwa kwa bei nafuu kwenye mikoa ambayo ina shida kama Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kwa hiki kipindi isaidie kuratibu zoezi hili. Wafanyabiashara ukiwaelekeza tu bila kuwasaidia namna yoyote ya kuwapa incentive, bado hawawezi wakafanya biashara na hawawezi wakapunguza tatizo la bei. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kwa hiki kipindi kabla ya msimu ujao wa mvua, ifahamu kwamba Mkoa wa Shinyanga tuna tatizo la uhaba wa chakula na isaidie kuratibu upatikanaji wa chakula cha bei nafuu kabla ya kufika msimu ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu ujao utakapofika, naimba sana Serikali isaidie jitihahada za Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kuanzisha kilimo cha umwagiliaji. Kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge Azza kwamba mwaka 2010/2011 Serikali ya Mkoa wa Shinyanga iliandaa mpango kabambe wa kupambana na njaa katika mkoa na iliweka mkoa katika kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda mojawapo iliyobuniwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, ni Halmashauri ya Wilaya Shinyanga Vijijini kwa maana ya Jimbo la Solwa pamoja na Jimbo la Msalala ambalo lina bonde zuri sana linalotoka maeneo ya Mwakitolyo kuungana kule kutoka mkondo wa Ziwa Victoria hadi kuja kwenye Kata za Mwanase, Kashishi, Bulige, Isaka pamoja na Isakajana kwa jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maeneo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji na taarifa zilishafika Wizarani. Naomba sana, jitihada hizi zilizoanzishwa na mkoa ziungwe mkono na Serikali ili badala ya kuomba chakula kila wakati, badala ya kuomba Serikali iingilie kati kupunguza bei ya chakula katika eneo hili, wananchi hawa waweze kulima na mvua zinanyesha, pamoja na kwamba zinanyesha kwa muda mfupi, maji yanapatikana, basi waweze kulima kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu tulipendekeza kuanzisha Soko la Kimataifa la mchele kwenye eneo la Bulige na mradi ukawa umekwishaanza kwa maana ya kuanza kujenga soko. Kwa bahati mbaya uendelezaji wa mradi huo mwaka 2013/2014 ukawa umesuasua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara isikume mradi huu utekelezwe ili kama mkoa tulivyopanga na Halmashauri na Jimbo kwamba mpunga uzalishwe kwa wingi kwenye eneo hili la Solo na Msalala na soko kubwa la mchele liweze kuwepo pale Bulige; na kwa kufanya hivyo umasikini utapungua na wananchi wataweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia kwa dakika chache zilizobaki, nataka kuishauri Serikali kwa upande wa uvuvi, ielekeze nguvu katika ufugaji wa samaki. Uvuvi wa samaki kutoka kwenye mabwawa na maziwa ambayo tayari yapo, hauna tija sana. Tujifunze kutoka nchi kama Vietnam ambayo zaidi ya asilimia 80 ya samaki wanaouzwa kwenye soko ni wale wanaofugwa kwenye vidimbwi vidogo vidogo. Jambo hili linawezekana na linaweza kikaongeza sana tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa migogoro ya wakulima na wafugaji, naomba sana Serikali iongeze juhudi katika kusaidia wafugaji kupata malisho. Ukisikiliza chanzo cha migogoro, ni malisho versus maeneo ya kulima. Sehemu kubwa ya maeneo makubwa ambayo yamekuwa malisho miaka ya nyuma kwa mfano Mkoa wa Shinyanga ambao unalima na kufuga, maeneo mengi ambayo yamekuwa ni ya mifugo, sasa wanalima. Kwa hiyo, wafugaji wanajikuta hawana maeneo ya kufugia, wanaendelea kuhama kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na mjadala kuhusu suala hili kwamba yatapatikana maeneo ya kuwasaidia wafugaji wawe na maeneo yao watakayoyamiliki na kufuga bila kuhama. Naomba Serikali iharakishe kukamilisha zoezi hili ili maeneo ya wafugaji yajulikane, maeneo ya wakulima yawepo ili migogoro iweze kwisha. Siyo jambo zuri kukaa tunalalamikia jambo hilo miaka nenda, rudi na mwisho wa siku tunashuhudia mauaji ya wakulima au wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, mpango wa Serikali ni mzuri, pamoja na kwamba kuna maeneo ambayo naiomba Serikali iongeze nguvu. Naiunga mkono bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Tizeba na rafiki yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Olenasha, ongezeni juhudi, sisi Wabunge tunaelewa mnachokifanya, tunajua mnafanya kazi kubwa na tutaendelea kuwaunga mkono. Tusaidieni katika hayo ambayo nimeyasema na Wabunge wenzangu wameyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.