Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara yake. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa hiyo naungana moja kwa moja na mapendekezo ya Kamati yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania walio wengi takribani asilimia 67 mpaka 70 wameajiriwa kwenye sekta hii ya kilimo. Kwa hiyo, kama Serikali imedhamiria kweli kutupeleka kwenye Uchumi wa Viwanda tunatakiwa kuongeza bajeti kwenye sekta hii ya kilimo. Badala ya bajeti hi kukua bajeti hii inaendelea kupungua kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sikubaliana na kuendelea kuipunguza hii bajeti, naomba Serikali iliangalie kwa jicho la huruma, kwamba eneo hili ndio eneo pekee ambalo linatoa ajira ambayo haina shaka katika nchi hii. Kwa hiyo ni vyema tukaongeza bajeti kwenye eneo hili kusudi watu walioajiriwa kwenye eneo hili waendelee kupata facilities kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na pendekezo la Serikali la ununuzi wa pembejeo kwa pamoja (bulk procurement). Tumeona kwenye mafuta tumefanikiwa sana na naamini kwenye pembejeo vile vile tutafanikiwa sana kwa ajili ya hii bulk procurement. Hii itatusaidia pembejeo itanunuliwa kwa wingi na naamini zitafika kwa wakati kwenye site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kule kwetu Mufindi, ukipeleka pembejeo baada ya mwezi wa Tisa, wakulima hawawezi kulima. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri ambaye amelileta pendekezo hili kwenye Kamati yetu na sisi tumelikubali na Waheshimiwa Wabunge
naamini tutalikubali kwamba hizi pembejeo zinunuliwe kwa wakati na zifike kwenye site kwa wakati. Pia tunaamini kwamba Serikali itakapopata kazi ya kununua hii, hakuna matatizo tena ya bei kwenye hizi pembejeo. Kwa sababu kuna watu walikuwa wanajipatia faida bila sababu. Kwa hiyo, nina hakika kabisa watu wetu wa Mufindi watalima wakiwa hawana shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni Benki ya Kilimo. Tuna benki ya kilimo na takribani ina miaka minne lakini benki hii haikui. Kwa hiyo, kusudi tuwasaidie wakulima walio wengi katika site kule ni vyema Serikali ikaongeza mtaji kwenye hii benki. Mtaji huu utawasaidia wakulima wadogo wadogo kukopa kwenye eneo ambalo halitakuwa lina interest kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, tunaiomba sana Serikali ifungue matawi kwenye site. Unakuta benki ya kilimo matawi yapo Dar es Salam, Arusha, yako wapi, kule site kwenye wakulima wadogo wadogo wa viazi, wakulima wadogo wadogo wa miwa, hatujafungua benki za kilimo. Wakulima wadogo wadogo wa nyanya kama vile ukienda kwenye majimbo ya wenzetu kama ya Kilolo, Ilula, Mufindi na Mdabulo. Tunaomba sana Serikali ifungue matawi kwenye maeneo haya na ihakikishe mikopo inaendelea kuwa kwa riba nafuu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo nyuma, azma ya Serikali ni kutupeleka kwenye uchumi wa viwanda. Ukitaka kuangalia kwa haraka haraka, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni watoto pacha ambao wanakwenda simultaneous. Kwa hiyo, bado naendelea kusisitiza tu kwamba hatutapata mafanikio ya kutosha kama hatutawekeza kwa kiasi kikubwa kwenye eneo hili la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la SAGCOT, hawa wenzetu wa SAGCOT ambao wanawasaidia wakulima wadogo wadogo wamejielekeza kwenye maeneo machache, tunaomba wafike kwenye maeneo mengine hata maeneo ya kule Mufindi. Wakifika kwenye maeneo haya, watasaidia sana kuhakikisha watu wanaboresha miundombinu na wanapata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu katika Wilaya yetu ya Mufindi Jimbo la Kusini na Kaskazini ni wakulima wakubwa sana wa chai. Kwa masikitiko makubwa, chai imekuwa inaharibika, inapotea, kwa sababu hatuna miundombinu ya uhakika. Wananchi wameshaanza kukata tamaa kwenye maeneo haya, kwa sababu wamelima chai na chai ni kilimo cha muda mrefu hawajui wafanye nini. Kuna baadhi ya watu wameshaamua kwamba wakate ile miti ya chai wapande mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri; last time alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkubwa wa chai lakini hakufika. Namwomba Mheshimiwa Waziri afike kwenye site aone adha wanayoipata wakulima wa chai katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo tuliyokuwa nayo ya chai katika Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Iringa kwa ujumla, kwa maana ya Kilolo ni makubwa sana na kama yatahudumiwa vizuri tutalima chai nyingi kuliko wanavyolima wenzetu wa Kenya. Kwa hiyo, utaalam unatakiwa uongezwe katika maeneo haya. Ni aibu kuona chai ya Mufindi, Kilolo na Njombe soko lake linaenda kufanyiwa Mombasa kwenye Taasisi inaitwa KATEPA, wakati TATEPA hapa Tanzania haifanyi juhudi za kutosha. Hatuna sababu ya kuendelea kutumia masoko ya wenzetu, wakati sisi wenyewe tunatakiwa tujiangalie na tuimarishe masoko yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala ambalo limekuwa tatizo la muda mrefu, madai ya mawakala. Mawakala wanadai hela zao muda mrefu sana na kuna baadhi ya mawakala wengine wameshaanza kupata matatizo, wengine wameshaanza kufa na wengine wameshaanza kuuziwa assets zao ambazo walizitumia kupata mikopo. Kwa hiyo, atakapokuja Mheshimiwa Waziri aje na majibu hapa. Last time waliambiwa wamwone Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini mpaka leo hii mawakala wapo hapa Dodoma wanataka wasadiwe kwenye hili eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo la kilimo cha umwagiliaji pamoja na kilimo cha vinyungu. Wilaya ya Mufindi hekta 350,000 zimechukuliwa na Maliasili; kwa hiyo watu wengi katika Wilaya ya Mufindi wanalima katika vinyungu, hawana ardhi. Ukiwaambia wasilime kwenye vinyungu hawana sehemu yoyote ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri alione jambo hili. Hata siku zile wakati tunaomba kura tulikuwa na lengo, kwamba tuwasaidie na wapiga kura wengi ambao walitupa kura ni kutoka katika eneo hili la vinyungu. Sasa leo hii unawaambia watu kwenye vinyungu wasilime, wakalime wapi hawa watu? Leo unawaambia wasilime kwenye vinyungu wakalime wapi? Mbadala wake ni nini? Labda kuna lengo hapa hamtaki Kigola, Chumi na Mgimwa warudi kwenye majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri atakapokuja, kama kweli Serikali wameamua sisi tusilime kwenye vinyungu, watuambie mbadala wake tuujue hapa leo hii. Kwenye jambo hili tutashika shilingi. Kwenye jambo hili Mheshimiwa Tizeba ni rafiki yetu lakini hatutamwangalia kwa sababu tukiendelea kumbembeleza kwenye jambo hili sisi ndio tutakuwa si Wabunge tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili, ndiko tunategemea kupata viazi vya uhakika, kwenye eneo hili tunategemea kupata mpunga wa uhakika na kwa eneo hili tunategemea kupata miwa. Sasa badala ya kuongeza ajira kwa watu, tunataka watu wengi wawe majambazi. Hoja ya kuwaambia leo hii watu waondoke kwenye vinyungu sisi hatukubaliani nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna jambo sasa hivi linaendelea, naomba Mheshimiwa Waziri kwa mamlaka aliyonayo alizuie. Kule kwetu sasa hivi wameshaanza kufyeka mahindi kwenye vinyungu. Kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aseme na watu wanahitaji elimu. Namwomba sana Mheshimiwa Tizeba atuangalie sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nameomba sana Mheshimiwa Tizeba, atakapokuja kuhitimisha hotuba yake hapa atuambie mbadala wa vinyungu ni nini.