Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwakunipa dakika tano angalau niseme machache kwa ajili ya Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kama kuna Mbunge atasimama kwenye Bunge hili na kusema bajeti ya maji isiongezwe basi huyo Mbunge labda alipata Ubunge kwa kupendelewa na alipewa zawadi tu, hakutafuta kura, lakini kama alikwenda kwa wananchi akaona kero zao hatathubutu akasimama na kusema bajeti hii iziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja za Wabunge wote wanaosema kwamba ile Sh.50 iongezwe mpaka Sh.100 ili wananchi wetu wapate maji. Wale ambao majimbo yao, mikoa yao ina maji, tafadhali mtuache sisi ambao bado wananchi wetu hawana maji ili tuunge mkono hoja hii ya kwamba fedha ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili kwa sababu mimi niko Jimbo la Babati Mjini lakini nina Kata nzima ya Sigino yenye vijiji vinne haina maji. Asubuhi nilikuwa naongea na Mbunge mmoja ananiambia Mheshimiwa Mbunge inawezekana sana fedha hizi zisiongezwe au zikaongezwa, nikamwambia lakini hebu tupige picha siku moja Wabunge tukae wiki nzima humu ndani tusioge na tusiwe na maji itakuwaje? Akaniambia hivi, tutanunua maji ya Kilimanjaro tutaoga. Nikamwambia okay, una uwezo wa kununua maji ya Kilimanjaro lakini mama na bibi yako uliyemwacha kijijini kule hana uwezo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tusiweke itikadi zetu katika suala hili. Niombe Serikali isikilize kilio hiki cha Wabunge wote kwamba fedha hizi ziongezwe ili wananchi wangu wa kata ya Sigino, Jimbo la Babati Mjini wapate maji. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika, wale akinamama walimvika mpaka na mgoroli akawaahidi kwamba katika bajeti hii fedha zitakwenda katika Vijiji vya Sigino, Singu, Dagailoi na Imbilili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye kitabu zimetengwa shilingi milioni 600 tu hazitatosha, lakini fedha zikiongezwa tutapata shilingi 2,700,000,000 ambazo tumeziomba. Kwa hiyo, niunge mkono kabisa hoja ya Wabunge kwamba fedha hizi ziongezwe na wananchi wa Tanzania wapate maji. Ni aibu, akinamama wanateseka, wanachota maji kongoroni, ndoo zao zinavunjika, wengine wanarudi usiku, wengine wanabakwa, wanahangaika wanatafuta maji halafu sisi wanawake humu ndani tuseme fedha zisiongezwe, inasikitisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kabisa Serikali kama mnaona tozo ya mafuta haitoshi twendeni hata kwenye mitandao ya simu, tuna 0.03 ya service charge ambayo siku zote wamekuwa hawalipi. Tumekuwa tukizungumza hata kwenye TAMISEMI hizi fedha haziendi. Hebu Serikali kaeni chini muangalie fedha hizi hata kama ni shilingi 20, 30, 50 tuzipeleke kwenye Mfuko wa Maji ili zipeleke maji kwa wananchi wetu. Wananchihawa wamevumilia kwa miaka hamsini, kwa nini tusiwatendee haki fedha zikaenda wakapelekelewa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sina ugomvi na Mawaziri, wao wamepelekewa asilimia 19, lakini Serikali kama mngepeleka asilimia 100 ya shilingi bilioni 900 ambazo zilipangwa maana yake kero hizi zingepungua. Kwa hiyo pia niombe Waziri wa Fedha pamoja na Serikali kwa ujumla wake Wizara ya Maji wapelekeni pesa. Pamoja na kwamba tunaomba fedha hizi ziongezwe, lakini fedha zile zilizopangwa ambapo miradi iko kwenye mchakato pia ziende.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kwenye Jimbo langu la Babati Mjini, Vijiji vya Haraa na Imbilili tulishampelekea Mheshimiwa Waziri bado kusaini tu mikataba, lakini tunaambiwa zimeenda asilimia 19 tu, bajeti ya Wizara ya Maji ilitakiwa ziende asilimia hata 50, 60, 70 au 80 mbona Wizara ya Ujenzi fedha zimeenda? Kwa nini Wizara ya Maji ambayo inamgusa kila mwanamke katika nchi hii msipeleke fedha?Wangapi waonapita kwenye barabara zenu za lami mnapeleka asilimia zaidi ya 70 au 80 lakini akinamama hawawezi wakapelekewa fedha zao?Kwa hiyo, niunge mkono hoja hii lazima Wabunge tuwe serious kwamba Wizara hii waongezewe fedha.