Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, niruhusu na mimi niungane na wale waliompongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri, lakini nimewasikiliza Wabunge wenzangu kwa umakini sana tangu jana na leo, tatizo hapa ni rasilimali fedha. Hakuna zaidi ya hapo kwa sababu hata tukipiga kelele namna gani, tukiimba namna gani kama hakuna pesa hata hii miradi tunayoiombea saa hizi haiwezi kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe ombi kama alivyotoa Mheshimiwa Kangi Lugola pale, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu, wa vyama vyote tukubaliane kimsingi, yale mapendekezo ya mwaka jana ya tozo ya shilingi 50 yaongezeke sasa yaende shilingi 100. Yakiwa shilingi 100 yatatupa shilingi bilioni 316. Hizi ukizijumlisha na fedha za ndani ambazo ni shilingi bilioni 408 ukajumlisha na fedha za nje ambazo ni shilingi bilioni 214 unapata jumla ya shilingi bilioni 940 na zaidi. Fedha hizi shilingi bilioni 940 inazidi hata ile bajeti ya mwaka jana. Sasa ili tufike huko, tukubaliane tu kimsingi tutoke kwenye 50 ya tozo twende shilingi 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka kweli miradi yetu hii ambayo tunaizungumzia humu ndani iende ikatekelezwe, tukubaliane kwamba shilingi bilioni 316 kila mwaka ziende kwenye miradi ya maji. Tukijipa miaka mitatu, tutakuwa na karibu shilingi trilioni moja, zote hizi zinakwenda kwenye maji. Najua matatizo ya maji kuanzia 2018, 2019 na 2020, kama tutakuwa na pesa hizo shilingi trilioni moja na zaidi, nina uhakika matatizo ya maji yanaweza kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili matatizo ya maji yapungue, ni lazima tuamue kwamba sh.50 itoke huku iende sh.100. Lazima tuamue! Bila kuamua kwa sababu hakuna sehemu nyingine, tukitegemea bajeti ya Serikali ya shilingi milioni 408 na pesa za nje shilingi milioni 214, fedha za nje zinaweza zikaja kidogo au zisije. Sasa ili tuondoke huko, ni lazima Bunge lako liamue, kwamba shilingi 50 tuachane nayo, twende kwenye shilingi 100 itakayotuzalishia shilingi bilioni 316 kila mwaka na hizi zinakwenda kwenye maji. Bila kufanya hivyo, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuamue sisi Wabunge wote. Naomba Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Mama Hawa Ghasia, naomba mwende mlisimamie hili. Mwaka 2016 tulikubaliana humu ndani, lakini halikutekelezwa, tunaomba mwaka huu, mlibebe kama lenu, lakini ni la Bunge zima. Yale maneno kwamba itashusha inflation, inflation hii itashuka lakini in multiple effect itakuwa ni kubwa zaidi, kwa sababu matokeo ya kuongeza sh.100/= multiple effect yake itakuwa ni kubwa zaidi tofauti na tunavyofikiria. Naomba sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mama Hawa Ghasia hili walibebe ili kusudi waende kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali angalau kwa kuanza mradi wa maji wa Ziwa Victoria. Naomba process zilizoanza ziharakishwe. Mwaka 2016 tulitenga shilingi bilioni moja, hakuna kilichofanyika; mwaka huu imetengwa shilingi bilioni mbili, najua yupo hapa Mheshimiwa Lwenge, hili suala nafikiri ni la kusukuma haraka haraka ili kusudi mradi huu ukamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kwimba, tayari nimeshamwandikia Mheshimiwa Waziri kwamba kuna visima vya maji 188 Wilaya nzima, havifanyi kazi, vimezeeka, maji hayatoki na pampu zimeibiwa. Visima 188 kwa Wilaya nzima ya Kwimba, Majimbo mawili Sumve na Kwimba, maana yake mimi ndio Mbunge ninayejumuisha Majimbo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hii dhana ya kuwatua ndoo akinamama ili ikamilike na iwe na uhalisia visima hivi 188 tuangalie namna ya kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mingine minne ya maji ya World Bank imekuwa ya muda mrefu sana, leo ni zaidi ya miaka 10 na kila siku nimekuwa nikiuliza swali humu ndani. Mheshimiwa Lwenge, matatizo yaliyoko kule hayasemeki! Watu wana urasimu wa kumwaga. Ukiuliza hiki, unaambiwa Mkandarasi; ukiuliza hivi, utaambiwa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kuondoa kero iliyopo kwenye maeneo hayo. Kadashi na Isunga tatizo ni kubwa, nimemwandikia, mengine yako chini ya asilimia 45 mengine 50, tatizo wanasema hela mnazo ninyi, wengine wanasema hela ziko huku. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hili alisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kuomba tena, hata ukitaka maji kule Tukuyu, najua kuna mvua nyingi tu huko, kwa Mheshimiwa Spika pia anataka maji,; bila kukubaliana hapa ongezeko la shilingi 50 kutoka kwenye shilingi 50 kwenda kwenye shilingi 100 tutakuwa tunasema hapa, tutaimba umwagiliaji sijui vitu gani; tutazame REA! Tulivyoanza REA, tulikubaliana humu ndani; leo tazama vijiji karibu vyote vinakwenda kupata umeme kwa sababu ya makubaliano ya humu ndani. Pesa za Mfuko wa Barabara sabini kwa thelathini, tazama barabara zetu leo ni sababu ya kukubaliana. Naomba na hili sasa na lenyewe tukubaliane tutoke kwenye shilingi 50 twende kwenye shilingi 100 ili tupate shilingi bilioni 316 kila mwaka ili tuweze kujenga visima na vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja.