Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze na hili suala la nyongeza ya fedha kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji. Tunaweza tukakimbilia kufanya maamuzi, maamuzi ambayo yakawa na athari ya ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi, kwa hiyo, badala ya kupunguza tatizo tukaongeza tatizo. Tatizo letu la msingi ambalo naliona katika Serikali hii inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi ni vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kama Serikali inaamua kununua ndege (Dreamliner) kwa quotation ya watu wa Boeing wanasema dola milioni 224 ambayo ni takribani shilingi bilioni 400 Serikali haitaki kusema walichokubaliana hasa ni kiasi gani wanasema ni pungufu ya shilingi bilioni 400. Kama tunaweza tukatoa pesa kununua ndege shilingi bilioni 400 hivi ni nini kinatushinda kutoa shilingi bilioni 400 kuongeza kwenye bajeti ya Wizara ya Maji? Kwa hiyo, ndiyo maana nimeanza kwa kusema kwamba, tatizo letu kubwa ni kipaumbele. Serikali ya CCM kwa awamu zote pamoja na kuwa inatamka kuwa maji ni kupaumbele number one katika nchi hii, lakini kwenye bajeti kwa nyakati mbalimbali maji hayajawahi kufanywa kipaumbele number one katika nchi hii.

Katika mazingira ya namna hii ya Serikali ya CCM kupuuza kero ya msingi ya wananchi, mimi kwa maoni yangu kwa muda ambao nimekaa Bungeni nianze na hili la kwanza, ufumbuzi hauwezi kupatikana katika huu mjadala tulioanza jana unaohitimishwa kesho. Ufumbuzi kwa maoni yangu unapatikana kwa Watanzania kutambua kwamba kwa miaka mingi wamedanganywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ufumbuzi ni kuindoa Serikali ya CCM madarakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyasema haya bila kusubiri Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hotuba kesho. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwishazungumza leo na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo Kiongozi wa Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipojibu maswali, swali mojawapo liliulizwa asubuhi leo kuhusu maji, nilitarajia Mheshimiwa Waziri Mkuu kuelezwa namna ambavyo hii bajeti ya maji imepungua, yaani mwaka jana bajeti ya maendeleo ilikuwa bilioni 915, leo bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 623 yaani tumepunguza bajeti kwa shilingi bilioni 292; nilitarajia Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Kiongozi wa shughuli za Serikali aliposimama hapa kujibu swali Bungeni angesema; kwa kweli nimesikia kilio cha Wabunge kuanzia jana na nimesikia vilevile swali nililoulizwa leo na naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutakaa tena katika Serikali, tutaongeza bajeti ya Wizara ya maji badala yake Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa kauli hapa Bungeni leo kwamba Wabunge tuipitishe bajeti kama ilivyo. Kwa maneno mengine mheshimiwa Waziri huyu wa Maji hatarajiwi kuja na jipya lolote kama Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa mwelekeo wa Serikali tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya namna hii Serikali hii ni vyema ikakiri tu kwamba imekwishashindwa kwenye suala la maji. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 aya ya 67 iliahidi kwamba ikifika mwaka 2010 asilimia 65 ya wananchi vijijini watakuwa na maji na asilimia 90 ya wananchi watakuwa na maji mijini.

Mheshimiwa Nasibu Spika, kwa maneno mengine, wale wananchi wenzangu walionituma Bungeni wa Kata ya Kibamba, iwe ni Kiluvya na maeneo mengine ya pembezoni Kibwegere na kadhalika kule Kwembe kule iwe ni Kisopwa, iwe ni Kwembe Kati katiza mpaka Kata ya Msigani, Malambamawili, nenda Mbezi kule maeneo ya pembeni, Mpiji Magohe, Goba sijui Kinzudi, Matosa maeneo yote haya ya Saranga, King’ong’o, Mavurunza yaani kwa ahadi hii ya Serikali; Serikali ya CCM iliahidi mwaka 2010 asilimia 90 wangepata maji, mwaka 2010 ikafika hawakupata maji, Serikali ikaahidi tena kwenye ilani nyingine ya CCM ya mwaka 2010/2015 kwamba ikifika mwaka 2015 asilimia 90 watapata maji, asilimia 65 watapata maji, ahadi nyingine ya uongo miaka 10 ikapita ikafika 2015, Serikali ikarudia tena ahadi ile ile ya kuahidi tena mwaka 2020 ndiyo matatizo haya yatatauliwa na Mheshimiwa Waziri ulijibu uongo Bungeni naomba tu utakapohitimisha ujibu ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipouliza swali Bunge hili, ukasema kwamba kwa sasa na hata katika kitabu chako umeonyesha tena kwamba kiwango cha maji kimeongezeka kutoka mita 300 mpaka 504 milioni na kwamba sasa kero kwa maneno yako mwenyewe umetumia maneno; “huduma ya maji imeimarika.” Wakati unanijibu swali Bungeni ulisema kuanzia sasa kilomita 12 huku, kilomita 12 huku kwenye barabara ya Morogoro, maeneo yote haya sasa yenye mabomba ya Mchina maji yatakuwa yanatoka. Ukaniahidi hapa Bungeni Mkutano huu huu ukasema maji yameshasukumwa tatizo ilikuwa ni umeme tu, maji yamesukumwa mpaka tanki pale Kibamba na sasa maji yatatoka, lakini Mheshimiwa Waziri ulisema maelezo ya uongo Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema, kwa haya majibu ya Serikali ambayo kimsingi Waheshimiwa Wabunge na hapa nitaomba nafasi kwa mujibu wa Kanuni ya 69(1) kabla ya kuingia kwenye hatua ya Kamati, kama Mheshimiwa Waziri hatatumia Kanuni ya 58(5) kuindoa hii hoja ili Serikali ilete commitment ya kurudisha zile shilingi bilioni 300 zilizoondolewa, kama Mheshimiwa Waziri hatatoa commitment hapa, Wizara ya Fedha haitasema ni kwa nini mpaka sasa imetoa asilimia 19.8 na wakati mpaka sasa ilipaswa pesa zitoke asilimia 75, kama hakutakuwa na commitment ni afadhali mjadala huu tuuahirishe kimsingi ili Serikali ikajipange upya ili bajeti hii ya maji iweze kuletwa ikiwa ina marekebisho ya msingi pesa za maji ziweze kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa Serikali hii ni muendelezo tu wa kusema uongo Bungeni, ni muendelezo wa kutotekeleza ahadi, kama hamtayafanya haya ni wakati wa Watanzania kote nchini wenye kero kubwa ya maji, kero number one kujipanga kuindoa CCM madarakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua kwamba mnaogopa haya yasiende kusemwa kwenye majimbo yenu ndiyo maana mnazuia mikutano ya vyama vya siasa. Lakini nawaambia mtatuzuia humu Bungeni, mtatuzuia majimboni, mtatuzuia maeneo mbalimbali lakini Watanzania wanauelewa ukweli wa kudanganywa na Ilani za CCM za toka miaka niliyoitaja. Bila kero ya msingi ya maji kuondolewa watachukua hatua mwaka 2019/2020.