Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Geita kwa kuniamini, kunipa kura nyingi nami ninaahidi sitawaangusha. Naomba kuchangia kwa haraka sana hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunatoka kwenye maeneo ya madini. Katika kura ambazo tumezipata katika Mkoa wa Geita na nina hakika kwamba Mkoa wangu wa Geita mimi ni Mwenyekiti pale, tukifeli sana ni namba tatu kwenye nchi hii kwenye ushindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia kubwa ya wananchi waliotuamini ni wachimbaji wadogo wadogo na ndiyo sera ambayo tulizunguka nayo kuomba kura za Mheshimiwa Rais na pia kuomba kura za Wabunge, ukizingatia Geita pia ilikuwa sehemu kubwa sana ya Kambi ya Upinzani kwenye Kanda yetu ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la madini, toka mwaka 2005 Mheshimiwa Jakaya Kikwete anaingia madarakani mpaka ameondoka wananchi wa Geita wanadanganywa. Na kwa mara ya pili Mheshimiwa Kikwete amekuja na Mheshimiwa Muhongo kwenye ziara. Tumezunguka naye, tukafika Nyarugusu Mheshimiwa Rais aliahidi kurudisha eneo la STAMICO kwa wachimbaji wadogo wadogo, ndani ya miezi miwili, mbele ya Profesa lakini baada ya hapo hatukuona utekelezaji wowote. Tulifuatilia ofisi ya Mheshimiwa Muhongo, bahati mbaya aliondolewa kwenye eneo lile, wanasema suala hili haliwezekani kwa sababu wawekezaji (shareholders) wa eneo lile wako Ulaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana imefika wakati sasa tusidanganywe tena na Mheshimiwa Profesa Muhongo tunakuombea, kwa vile na wewe umepita kwenye changamoto ya kuchaguliwa umeona maswali yanavyokuwa kule kwa wananchi, tunaomba suala hili ulitie kwenye akili zako, hatutaki tena kudanganywa! Amekuja Rais ameahidi miezi miwili, amekuja Mheshimiwa Kinana akaahidi wiki mbili, Mheshimiwa Simbachawene akapiga simu tupeleke watu kwa nguvu. Hatukutaka hivyo kwa sababu sisi ni viongozi.
Kwa hiyo, ninachoomba suala hili watu wameshaahidiwa, hatutaki tena kudanganywa. Kwanza limeshikiliwa na vigogo wa CCM, kwa nini tunaendelea kumkumbatia mtu mmoja tunatesa watu milioni tano. Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala hili Mheshimiwa Profesa kama hulijui tukusaidie documents, tunazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili, hapo hapo kwenye madini. Unafahamu changamoto kubwa ya Mji wa Geita. Tunashukuru juzi kidogo umefunguka ukatuachia magwangala, lakini hatujaridhika! Magwangala ni sehemu ndogo sana. Tunahitaji kuwa na maeneo ya wachimbaji wa kati kwa sababu Magwangala ni ya watu wa hali ya chini wanaookota wanapata shilingi 700,000/= hadi milioni.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, magwangala ni miambataka, waste mine bado hujaelewa Mheshimiwa? Maarufu kama magwangala. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa maeneo ambayo tumeshakaa tukakutumia tunayaomba maeneo ya Nyamatagata na Samina uyarudishe kwa wananchi, kwa sababu sheria inasema baada ya miaka mitano wachimbaji wadogo tupewe eneo, lakini wataalam wako wanatupeleka tofauti, wanakwenda kutupatia maeneo tunachimba visima hatupati dhahabu wakati dhahabu ya kwenye magoti iko kwenye maeneo hayo. Sasa kwa sababu tuko wote humu ndani, usipotusaidia mimi kila siku nitawaka na wewe mpaka kitaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu ya pili ninaomba sana katika suala la maliasili. Maliasili ni tatizo kwenye Wilaya ya Geita na Mkoa mzima wa Geita, kwa bahati mbaya au nzuri nimepangwa kwenye Kamati ile. Mimi sijasomea misitu lakini naielewa kwa sababu nimetokea misituni. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sintofahamu. Mimi mwenyewe kijiji nilichozaliwa miaka ya 1960 tukapangwa kijiji mwaka 1974, juzi ilipoanza bomoa bomoa ya Dar es Salaam kimehamishwa kigingi kutoka porini kimekuja kuwekwa nyumbani tulipozaliwa na wakati kijiji kina watu na kimetoa watu wakubwa sasa. Sielewi hii sintofahamu kwenye Baraza la Mawaziri kwa sababu wanakaa wanapanga sehemu za kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sintofahamu ya bomoa bomoa wengine wanabomoa Dar es Salaam, wengine wanafukuza watu maporini, wengine wanabomoa Mwanza huko, naomba kuuliza, hawa wataalam hili suala la bomoa bomoa, mimi mwenyewe naomba niseme wazi siungi mkono suala la kubomoa, na ninaamini kwamba linaumiza tu watu maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano kwa Mkoa wa Mwanza, ukienda Mwanza nyumba za eneo la Ghana pale nyumba zote zimewekwa alama ya “X” ziko kwenye mto unaopita Kirumba kuingia Ziwani pale, lakini wakati huo huo Serikali imetoa kibali kujenga BOT ghorofa 12 hatua tatu tu kutoka kwenye mto, ukienda kituo cha polisi na custom ya Mwanza iko Ziwani. Sasa tunaipeleka wapi nchi hii na hawa wataalam wetu wanaotoa amri huku na huku wanatekeleza vitu vingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana kwamba eneo hili la maliasili sisi tunatoka misituni tumeshaleta maombi Wizarani kwamba kama tulikuwa na hekta 15,000 za pori kwa nini tusipewe hekta 7,000? Kwa sababu wakati mnatupa tunatunza hekta 15,000 tulikuwa na wakazi 57,000 leo tuko 300,000 mnatulazimisha tukae kwenye heka 5 haiwezekani! Tunakaa kila siku tunapigana na polisi mpaka lini? Nimuombe Waziri mwenye dhamana aliziangatie hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni suala la kilimo. Kwenye upande wa Idara ya Kilimo ninamuomba Mheshimiwa Waziri Mwigulu ukae na wataalam wako. Nataka nikuhakikishie ni wezi wa hatari. Kwa nini nasema hivyo? Mfano Wilaya ya Geita tumeletewa tani 5,300, watu wetu wamepewa vibali wakaenda kulipa Shinyanga, ukishalipa Shinyanga unapewa siku saba. Ukitoka Geita kwenda Shinyanga siku moja, kwenda Sumbawanga siku nne lori linatumia siku nne, kupanga foleni kupakia ni siku tatu. Mtu amepakia lori moja anaambiwa kibali kimeisha, halafu kwenu huku mnaonesha mmeshatoa mahindi, wanayauza tena kwa mtu mwingine, tunaomba ulifuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la afya, Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu ulikuja na Makamu wa Rais, ukadanganywa hospitali nzuri, ukapambwa, sisi hatutaki majengo tunataka dawa. Ile ilikuwa ni bosheni (fake) ya kusafisha mgodi wa dhahabu unaotuibia pale Geita. Tunaomba sasa ufanye follow up ya kuja kuangalia, hakuna chochote, watu wanakuja kufaidi majengo na vitanda hakuna dawa, tunaomba uje uangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kitwanga kama yuko humu, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri hebu buni mbinu nyingine ya kuwakamata hawa boda boda. Kauli yako ulivyotoa ukienda vituo vyote nchi hii vimejaa bodaboda hatuna ujanja mwingine wa kuweza kuwakusanya hao bodaboda na kuwatambua au kuzitambua, kwa sababu hata wale ambao hawana makosa nao wanaombwa hela, tunaomba uliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kiwanda, Mheshimiwa Mwijage, umejipapambanua vizuri sana lakini naomba nikwambie wataalam wako wanakudanganya wana-copy na ku- paste. Unasema tunafungua Kiwanda cha Juice Morogoro. Tanzania hatuna matunda ya kutengeneza juice hapa. Mimi ni mwathirika nimedanganywa na wataalam wako, tumenunua kiwanda, tumeleta wataalam wenye mashine wanatuambia matunda yetu mananasi na maembe ni matunda ya kutengeneza dawa za kienyeji! (Kicheko)
Wataalam wako wame-copy maembe ya Uarabuni wanatuambia yanafaa kwenye viwanda vya Tanzania. Hebu jaribu siku moja ukachukue mti mmoja kila chungwa moja linaladha tofauti, unatengenezaje hiyo juice! Unaongeza pilipili au unatengeneza kitu gani waambie wataalam wako wafanye utafiti na uchunguzi wa kina wasikufanye ukajipambanua hapa watu tunakushangaa. Hatuna matunda, matunda yetu haya yameenda Italy kufanyiwa test yanaonekana ni matunda ya kutengeza dawa za kienyeji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana akina Ndodi mnapambana nao nao huko, na akina nani huyu aliyekamatwa na Mheshimiwa Kigwangalla, hatuna matunda ya juice. Hebu leo tengeneza juice ya mananasi, ukiiacha siku ya kwanza, siku ya pili unapata pombe ya kienyeji. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuwashauri wataalam wetu watumie muda mwingi sana kufanya utafiti wa kina kumshauri Rais vinginevyo mtahamasisha watu wafungue viwanda halafu mnakutana na vitu vya ajabu, tunaingia mikopo ya mabenki hatutalipa tutatangazwa kwenye magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nilizungumza juzi watu wakanicheka sana. Suala la mirungi, mimi siyo mlaji lakini nasema tujifunze Kenya mirungi inasindikizwa na bunduki na jeshi, sisi huku tunaiita mihadalati. Na nikuambie pamoja na kuzuia haihitaji kuwa na Usalama wa Taifa wala Polisi. Sasa hivi tuzunguke Dodoma hapa, hapa wanakula na usalama tunao, Tanga wanakula, Dar es Salaam wanakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. (Makofi/Kicheko)