Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nianze na kumpongeza Dkt. Harrison Mwakyembe Waziri, Naibu Waziri Anastazia Wambura, Makatibu Wakuu na watendaji wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba hapa Bungeni ili tuijadili. Yapo mambo ambayo nahitaji kuyachangia ambayo ni:

Moja, ufinyu wa Bajeti; siku zote Wizara hii imekuwa ikipatiwa bajeti finyu sana na kusababisha Wizara hii kufanya kazi zake katika wakati mgumu sana na mbaya zaidi pamoja na kupatiwa bajeti kidogo lakini hata bajeti iliyopangwa haipelekwi kwa wakati hivyo kusababisha Miradi mingi iliyopangwa kutokamilika kwa wakati. Ni vema Wizara hii ingepewa kipaumbele kwa sababu pia imekuwa ikifanya kazi ya vijana wetu inayohusiana na sanaa.

Mheshimiwa Spika, uvamizi wa viwanja vya michezo katika Halmashauri, vijana wetu wanakosa haki yao ya msingi kutokana na uvamizi uliofanywa katika viwanja vilivyoachwa wazi kwa ajili ya michezo kuvamiwa na kugawiwa kwa watu kujenga. Nakumbuka Serikali ilitoa tamko kuwa waliovamia viwanja vya wazi waondolewe lakini mpaka leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali kwa ajili ya jambo hilo. Hivyo, ningependa kupatiwa ufafanuzi wa agizo hilo la Serikali sababu vijana wengi hawana maeneo ya michezo.

Mheshimiwa Spika, Vazi la Taifa; ningependa kujua mpango wa Serikali kuhusiana na vazi la Taifa, nakumbuka Serikali ya Awamu ya Nne ilishawahi kutuletea taarifa kuhusiana na mchakato wa kupata vazi hilo lakini mwisho wake mpaka leo hatujui limefikia wapi.

Mheshimiwa Spika, (TBC) Shirika la Utangazaji la Taifa; naomba Serikali ifanye jitihada za kutosha kuhakikisha TBC inapatiwa pesa ya kutosha ili iweze kusikika nchi nzima. Tunasikia vibaya kuona maeneo ya mipakani wanapata mawasiliano toka nchi jirani. Pia vitendea kazi viboreshwe viendane na hadhi ya chombo cha Serikali.

Mheshimiwa Spika, watu wenye ulemavu; naomba Serikali iwatendee haki watu wenye ulemavu kwa kuweka Sheria ya kuhakikisha wamiliki wote wenye Television wanaweka watafsiri wa lugha katika Television ili watu wenye ulemavu wa kusikia nao waweze kuona. Pia itawasaidia kupata ajira kwa watu waliosomea kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, michezo ya UMISETA; naiomba Serikali yetu iweke kipaumbele kikubwa sana katika kutenga pesa kwa ajili ya michezo hiyo ili tuweze kuibua vipaji vya watoto wetu ili tuviendeleze kwa ajili ya kusaidia nchi hii kwa upande wa maendeleo ya michezo. Michezo ni ajira, michezo ni afya na michezo inajenga mahusiano.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.