Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichangie kuhusiana na suala zima la COSOTA. COSOTA ni kitengo ambacho kilianzishwa makusudi kabisa kwa ajili ya kuwasaidia wasanii ili waweze kumiliki kazi zao ipasavyo, lakini pia kuondokana na wizi ambao unafanywa na watu kutokana na hizi kazi za wasanii. Cha kustaajabisha ni kwamba kitengo hichi cha COSOTA kimepelekwa katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Niishauri Serikali kwamba kitengo hiki cha COSOTA kiondoke kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara na kuweza kurudi katika Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu ukiangalia COSOTA kazi yao ni kuwatetea wasanii, kulinda kazi zao na hizo hati miliki zao. Sasa unapokipeleka kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara yenyewe inajihusisha na mambo mengine kabisa. Sasa unapopeleka chombo hiki kwenye Wizara kama ile tusitegemee accountability ya chombo hiki. Nashauri Serikali iweze kurudisha chombo hiki cha COSOTA kwenye Wizara ya Habari na Utamaduni kwa ajili ya accountability yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia chombo hiki ni muhimu sana katika kulinda haki za wasanii. Tunaona kazi za wasanii zinaibiwa sana, lakini adhabu yake pia inayotolewa kutokana na ile sheria ambayo tulipitisha hapa Bungeni ya hati miliki yaani copy right kwa kweli ni ndogo sana. Unakuta sheria inasema kwamba kazi za msanii zinapokuwa zimeibiwa mtu aliyeiba zile kazi anaadhibiwa kwa adhabu ya faini ya shilingi milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni juzi tu hapa tuliona mtu ameiba kontena kubwa sana la kazi za wasanii na adhabu aliyopewa ni faini ya shilingi milioni tano. Hivi mimi nikiiba kazi ya msanii ambayo najua kabisa kwamba kazi hii inaenda kunipa pesa zaidi hata zaidi ya shilingi milioni 20 halafu leo unaniambia kwamba nilipe faini ya shilingi milioni tano, sitaacha kweli kuwaibiwa wasanii kazi zao? Hili liko wazi kabisa, kazi za wasanii zitaendelea kuibiwa endapo tutaacha COSOTA kutosimamia kazi hizi za wasanii na adhabu zake kuwa ni ndogo kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri nini Serikali? Naishauri Serikali adhabu za kuiba kazi za wasanii ziwe sawa kabisa na adhabu za unyang’anyi, sijui kama niko sahihi lakini nazungumzia piracy. Kwenye Penal Code mtu akiwa amefanya unyang’anyi (piracy) anapelekwa jela kwa muda wa miaka saba, lakini sasa kazi za wasanii zinapoibiwa tunaona kama ni kitu cha kawaida tu. Nashauri kabisa Serikali iweze kuuchukulia huu wizi wa kazi za wasanii kuwa kama wizi mwingine tu wa aina ya piracy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wasanii ambapo wanakuwa wanaibiwa kazi zao kwa namna ya kupigwa kwa mfano redioni. Let’s say mwanamuziki ambapo nyimbo zake zinakuwa zinapigwa redioni, lakini huyu mwanamuziki hafaidiki na wimbo wake kupigwa redioni. Nitakupa mfano mzuri sana. Tuna wanamuziki maarufu sana hapa Tanzania nikimtaja King Kiki kila mtu anawaza kitambaa cheupe na ndani ya Bunge hili naamini kabisa hata leo hii nikisema mimi natoa offer kwa Waheshimiwa Wabunge kwenda kumsikiliza King Kiki wote mtakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukumbuke na kuweka kichwani kwamba tunapomsikiliza huyu mwanamuziki King Kiki pamoja na kupiga wimbo wake wa kitambaa cheupe, tunashangilia kwenye sherehe kwenye harusi au popote pale ambapo mtu unakuwa na shughuli yako nzuri, unamaliza kushangilia pale lakini huyu mwanamuziki King Kiki ukienda kumuangalia na ile kazi ambayo wewe umekuwa ukiishangilia anafaidika vipi? Unamchukua huyu mwanamuziki unamuweka hapa haendani kabisa na muziki ambao unapigwa redioni na kushangiliwa na kila Mtanzania. Naomba sana Serikali iweze kusimamia na kuzilinda kazi za wasanii ili waweze kufaidika ili basi siku moja hawa wasanii tuwaone kwamba kweli wanaendana na muziki ambao sisi Watanzania tunapenda kuusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na suala la kurekebisha Sheria ya Hati Miliki. Nasema hivi kwa sababu gani? Sheria hii kwanza imeshapendekezwa katika kamati mbalimbali kwamba iweze kufanyiwa marekebisho. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo ambao tuna- deal na hizi kanuni ambazo zinatungwa. Tuliipitia hii Sheria ya Hati Miliki tukaona upungufu uliomo katika sheria hiyo. Upungufu mmoja ambao tuliugundua ni kwamba wakati sheria hii inatungwa hakukuwepo na ushirikishwaji wa wadau ambao ni wasanii, wanamichezo na wadau wengine mbalimbali ambao wanahusika katika suala zima la utamaduni na sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo linakuja kwamba pale ambapo wale wadau ambao wanahusika na sheria inayotungwa hawajashirikishwa, utaona kabisa kunakuwa na gap ambalo limewekwa. Kwa hiyo, naomba sana pamoja na mambo mengine yote ambayo yanaitaka sheria hii kurekebishwa kama vile adhabu, kwa sababu katika sheria hii ndiyo pale tunaona ile adhabu ya kuwaadhibu wale ambao wameiba kazi za wasanii ndiyo hiyo ya shilingi milioni tano ambayo ni ndogo.

Kwa hiyo, kama ungeshirikisha wale wadau ambao wanahusika ungeona wangeweza kupendekeza jambo ambalo mimi leo nalisema na kulipendekeza mbele ya Serikali kwamba iwe ni adhabu sawa kabisa na wizi mwingine. Kwa hiyo, nashauri kabisa Serikali iweze kutuletea hii sheria ili tuweze kuifanyia marekebisho lakini baada ya kuwa imewashirikisha wadau wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti jambo la mwisho ni suala la michezo. Suala la michezo hapa Tanzania hatulichukulii maanani kabisa. Ukiangalia enzi za zamani michezo ilikuwa ni kitu ambacho tunakitilia maanani sana. Kila mahali unakoenda hata mwanafunzi anafahamu kabisa kwamba mimi bila kushiriki michezo sitaweza kufaulu darasani kwa sababu darasani tulikuwa tunaambiwa hivyo na walimu wetu kwamba ili uweze kufanya vizuri lazima ushiriki michezo. Hiyo inaendana kabisa na usemi kwamba ili mtu uwe active kwenye akili zako lazima kwanza ushiriki michezo kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, suala la michezo hapa Tanzania tumekuwa tukilichukulia tu kama jambo la kawaida. Mimi naiomba Serikali ianze sasa kurudisha michezo mashuleni na kuweza kuweka mkazo huko mashuleni ili hawa akina Samatta watokee kule na hata kina Diamond hawa watokee kule kule kwa sababu hata kwenye kuhamasisha michezo kuna uimbaji pia huko mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kurahisisha suala hili ili liweze kufanyika vizuri ni kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba tuanzishe sports academy. Nchi kama Kenya tu msifikiri kwamba Kenya wanaposhinda kwenye Olympics mkadhani kwamba huwa wanaenda tu, wanaibuana from no where wanapelekwa kwenye michezo, hapana! Kenya wanachukua wachezaji kutoka kwenye sports academy zao na sasa hivi Kenya wanaenda mbali zaidi wanaleta International Sports Academy ambayo hiyo sasa itakuwa inawarahisishia kuweza kutoa wachezaji kutoka kwenye zile sports academy kuwapeleka kwenda kufanya mashindano lakini sisi hapa tunaibuana tu, mtu akisema anajua kuogelea anabebwa, anapelekwa, akifika kule ameshindwa. Tanzania hakuna mchezo ambao tumewahi kufanya vizuri hata siku moja. Nadhani hizo ni historia za nyuma kabisa labda hata nilikuwa sijazaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya mapendekezo hayo, naamini Serikali itachukua mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge wote na kuweza kuboresha Sekta hii ya Habari, Utamaduni na Michezo. Nashukuru sana na naunga mkono hoja.