Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina mambo machache ya kuzungumza lakini kimoja nitakisema in passing tu juu ya mwenge. Tusipeane majina wala tusipunguziane uzalendo kwa sababu tu hatuukubali mwenge. Mimi kwa bahati nilikuwemo katika Tume ya Warioba na katika kitu Watanzania walichokikataa na wakasema waziwazi uende makumbusho ni Mwenge wa Uhuru. Kwa hiyo, wanaosema kwamba mwenge upumzike au kama msemaji wa sasa hivi aliyesema tutafute modality nyingine mimi ni mmojawapo na hii hainipunguzii uzalendo kwamba mimi ni Mtanzania na naipenda Tanzania yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sisi kama Taifa tunaishi katika zama za sasa, hatuwezi kuishi sasa kisha tukabakia kizamani. Sasa hivi dunia imepanuka, kuna technology mbalimbali na kuna njia mbalimbali za kuwasiliana. Wakati njia za kuwasiliana zinapanuka na wakati sisi tunapimwa kwa ajili ya kuwa wawazi kwa wanachi wetu na sisi kuwa huru kujieleza, ndipo sisi tunapofunga milango ya uhuru wa habari na uhuru watu wetu kujieleza. Hii hai-augur well na vipimo ambavyo sisi tunapimwa kama nchi na ndiyo maana ripoti ya Amnesty juzi imetu-condemn na kutushusha sisi katika suala la uwazi na uhuru kwa waandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii katika upande wa habari, mimi maisha yangu yote ni mwandishi wa habari na nimepita wakati ambapo tulikuwa tunabanwa hata kusema tulikuwa hatuwezi. Wakati naripoti Zanzibar naweza kuiandika story leo nikaenda Dar es Salaam nikakaa siku tatu nasubiri mshindo kule Zanzibar utakuwa vipi, tusiishi tena hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii wakati tunapanua demokrasia mwaka mmoja tunapitisha sheria tatu za kubana uhuru na kubana watu namna ya kujieleza, nafikiri hii si sahihi. Hii ni dalili ya woga na dalili ya kuogopa watu wako wenyewe wasiseme. Kiongozi mzuri, Serikali nzuri ni ile ambayo inaruhusu watu wao watoe joto lao, wajieleze ili wajue kuna kitu gani katika Taifa. Kwa hiyo, mimi nafikiri tusijivunie kwamba tunazuia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine tu kwa mfano, leo tumezungumza vitu vingi sana kuhusu wasanii na utamaduni, lakini tumejifungia humu ndani. Tumezuia wananchi wetu wasisikilize na wasipate taarifa juu ya mijadala ya Bunge kwa hofu tu kwamba wakisikia watabadilika mawazo, tusiogope hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuzungumzia ni suala la kiswahili, watu wengi wanazungumzia habari ya kiswahili. Kwa wale ambao hawajui, mimi ni mpenzi sana wa Kiswahili na ni mwandishi wa mashairi lakini pia ni mwandishi wa vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wakati tunajivuna kwamba Tanzania ndiyo mabingwa wa kiswahili lakini kusema kweli Kenya wametutangulia. Graduates wa Kenya kwa kiswahili hatufiki sisi hata one third yao kwa kila mwaka. Sasa hivi katika mashirika mengi ya kimataifa, translators wengi walioko nje, vyuo vingi vikuu, walimu ni kutoka Kenya na siyo Tanzania. Nchi hii ya Tanzania ambayo inajivuna ina kiswahili niambieni kuna literature prize gani ndani ya nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya katika zawadi ambayo inaongoza duniani kwa kiswahili ni Cornell-Mabati Kiswahili Prize ambapo mimi mwaka huu nime-submit kitabu changu kinaitwa La Kuvunda. Wenzetu hawa wanatoa zawadi kila mwaka kwa miaka mitano sasa na kuna commitment ya kampuni ya Mabati na Cornell University kuendelea kwa muda wa miaka kumi ijayo, hata hili hatuwezi kubuni ku-approach corporate world ya Tanzania ikashirikiana na chuo kikuu kimojawapo kukawa na literature prize kwa kila mwaka? Hii itaibua waandishi, tutabaki tunaimba tu tulikuwa na Ibrahim Hussein, Profesa Lihamba, Profesa Penina, wako wapi watu kama hao, hakuna tena caliber kama hiyo kwa sababu hatuwatengenezi. Tusitarajie tu kwamba watuzuka bila kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni suala zima la culture ya michezo ya kuigiza. Tunazungumza sana habari ya bongo movie lakini moja katika culture nzuri sana ni michezo ya kuigiza ambapo Tanzania imekufa. Nilipokuwa chuo kikuu ilikuwa wakija wale waigizaji Nkurumah Hall inajaa, sasa hivi hata sijui kama kuna michezo ya kuigiza ndani ya nchi hii kwa sababu hata waandishi wa michezo ya kuigiza hawapo tena na hawatengenezwi na hawatayarishwi. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri alitizame hili, tuwe na competition za kila mara ili kuweza kukuza jambo hili. Sasa hivi tuna vyuo vikuu vinafika 50, jambo kama hilo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije katika area ya michezo ambayo naielewa vizuri sana kama ninavyoelewa suala la habari na hapa nitazungumza zaidi kidogo.

Mimi nafikiri ni katika wale ambao siamini kwamba Wizara au Serikali ndiyo yenye jukumu la michezo, mimi siamini. Mimi naamini Serikali kazi yake ni kutengeneza sera, lakini corporate world ndiyo ambayo inaweza kusimama na kukuza michezo na mfano mzuri ni huu wa Simbu hivi sasa. Niliwahi kuzungumza na Mheshimiwa Nape wakati akiwa Waziri kwamba tuache kumpa mzigo mtu mmoja kumwambia tunataka shilingi milioni 200 kwenda Olympic au shilingi milioni 500 kwenda Commonwealth, unakwenda kwa mtu mmoja mmoja, uache kila corporate imwambie wewe chukua dhamana ya mwanariadha huyu hapa, wewe chukua dhamana ya mwanariadha huyu hapa, tutafika mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wanalalamika wanasema hatupati timu kubwa za nje kuja Tanzania, wanalalamika kwamba rank ya Tanzania haipandi kwa sababu hatuchezi na timu kubwa. Kucheza na timu kubwa ni gharama kubwa sana, kuileta Brazil mimi mwenyewe nilijaribu, minimum wanataka dola milioni moja za kucheza uwanjani, mbali ya gharama zao. Kuileta Argentina inahitajika kama dola 800,000 kuwaleta wakacheza uwanjani mbali ya gharama zao nyingine za ndege na kila kitu. Kwa hiyo, kama corporate Tanzania hatujaishirikisha vya kutosha ikaweza kuchangia, hatuwezi kuzileta timu kubwa na maisha yatabakia kule kule zero. Maana yake unataka ulete timu lakini kiingilio unataka uweke shilingi 5,000, unasema eti unawajali watu wadogo, haiwezekani, lazima kimojawapo utakikosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine watu wamezungumzia hapa habari ya vipaji, vipaji vinatengenezwa na tena siyo Serikali yenye jukumu la kutengeneza academy, ni mimi na wewe. Wabunge pia wana uwezo, wana haki na wajibu wa kutengeneza vipaji kwa sababu vipaji ni biashara, unaweza ukatumia shilingi milioni 100 lakini wakati ukiuza mchezaji mmoja unaweza ukapata shilingi bilioni moja. Kesi ya Samata kwa mfano, mimi nilikuwa involved mara nyingi katika biashara zake, najua namna ambavyo amefikia pale.

Kwa hiyo, watu wajue kwamba kuwekeza kwenye riadha, soka, vipaji inalipa kwa mchezaji mmoja tu ukipata, siyo wawili au watatu, mmoja tu inalipa. Kwa hiyo, Wabunge hilo pia mnaweza kulichangamkia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sikubaliani na msemaji aliyepita hapa kwamba tuwalete wachezaji wengi wa nje wacheze ligi yetu ya ndani. Uingereza wana tatizo hivi sasa hawana timu ya Taifa nzuri kwa sababu wageni ni wengi. Cha kufanya sasa hivi TFF itengeneze kanuni kwamba klabu yoyote kwanza iwe na timu ndogo lakini ilazimike kama vile ambavyo kuna limit ya wachezaji wa nje kucheza watano basi lazima iwe na mchezaji under 20 katika kila mechi yake ya ligi, mmoja, wawili au watatu, hiyo itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine naogopa time yangu isiishe nataka nizungumzie juu ya mchezo wa chess. Mheshimiwa Waziri nisikilize vizuri. Chess ni mchezo ambao unaweza kututoa Tanzania kwa haraka sana, kwanza hauna gharama. Mimi ni mshabiki wa chess na nafundisha chess. Ni mchezo ambao ukishapata bao lako la kuchezea, mnakaa watu wawili, ukivaa bukta, kanga, seluni (msuli) unacheza tu. Ni mchezo ambao unaweza kufundishwa na kukuza vipaji vya watoto wetu. Kuna uwezekano pia wa kusaidia kupata masters wa chess wakacheza dunia nzima na tukajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nafikiri tusing’ang’anie tu michezo iliyopo na ndiyo maana hapa nataka kusema Mheshimiwa Waziri lazima hivi sasa tuamue tuwe na priority, iko michezo tumecheza miaka haijatupeleka popote, lakini iko michezo inayoweza kututoa. Kwa hiyo, hata kama utatangaza waziwazi kwamba priority itakuwa ni riadha, soka na kitu fulani na kitu fulani kwa sababu hatuwezi kucheza michezo yote kwa sababu hatuna fedha za kuhudumia michezo yote, lakini lazima tuangalie na hii michezo mingine. Mheshimiwa Waziri tunaweza kushauriana zaidi ukinihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.