Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa na Serikali. Nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa utumishi uliotukuka katika kuwasaidia Watanzania, katika kuwa na afya na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii zilizopo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya wagonjwa (ambulance); magari haya ni muhimu sana kama ilivyo muhimu kuwa na dawa za kutosha, vifaa tiba vya kutosha. Pia ni muhimu kila hospitali na baadhi ya vituo vya afya vilivyopo maeneo ya vijijini ndiyo vinavyohudumia watu wengi sana ambao wanategemea kupata matibabu katika vituo hivi pekee tofauti na maeneo ya mjini ambako kuna hospitali na vituo vya afya visivyo vya Serikali. Mfano, katika Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe eneo hili lina takribani watu zaidi ya 100,000 lakini ina vituo vitatu tu vya afya na hakuna hospitali yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wagonjwa wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata matibabu kwenye kituo cha afya kilichopo Lupembe umbali wa kilometa 75 toka Hospitali ya Kibena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kituo kipya cha Kichiwa kipo umbali wa kilometa 50 toka Hospitali ya Kibena na kituo cha Sovi ambacho kipo umbali wa kilometa 45 toka Hospitali ya Kibena. Katika Halmashauri yetu tumekuwa tukipoteza akina mama wengi kwa kucheleweshwa kupata upasuaji kutokana na kutokupata msaada wa usafiri kwa ajili ya kupelekwa Hospitali ya Kibena kwa ajili ya upasuaji. Hivyo tunaomba tupewe gari angalau moja kwenye vituo hivi vitatu kwa ajili ya kuwasaidia usafiri akina mama wajawazito na wagonjwa mahtuti ili kuwahi matibabu au huduma kwenye Hospitali ya Kibena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Wilaya, Jimbo letu na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe haina hospitali. Tumeanza jitihada za kujenga hospitali ya Wilaya. Wananchi kwa kutambua umuhimu wa kuwa na hospitali ya Wilaya, wamejitolea eneo lao lenye ukubwa wa ekari 52 ili eneo hili litumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali. Tunaomba Serikali itusaidie kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazee ambao ni wazazi wetu ambao sisi watoto wao tuna wajibu wa kuwasaidia kwa malazi, mavazi, chakula na kuwahudumia pale wanapokuwa na matatizo ya kiafya. Wazee wengi wanafariki kabla ya muda wao kutokana na ugumu wa maisha na msongamano wa mawazo unaotokana na watoto wengi hawatunzi wazazi wao, hata kama watakuwa na uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea wazee wanatunzwa vizuri na Serikali kwa kushirikiana na watoto wao. Hii inawafanya waishi miaka mingi tofauti na Tanzania na nchi nyigine za Afrika. Hivyo basi, napendekeza Serikali ije na sheria itakayotutaka Watanzania kuhakikisha kwamba wanawatunza wazazi wao hasa wanapokuwa wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mara nyingi watoto wakipata kipato huwa wanawasahau wazazi waliowalea, wazazi wanataabika vijijini bila chakula na makazi duni wakati wao wakiwa na maisha mazuri. Hivyo sheria ikitungwa itawabana watoto wao kuwa na wajibu wa kuwalea wazazi wao, angalau kwa kuwapa huduma za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi hasa maeneo ya vijijini.Mara nyingi watumishi wa afya wakianzia kazi mjini huwa hawapo tayari kuhamia vijijini pale wanapopata uhamisho wa kwenda vijijini. Hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuwafanya watumishi wawe flexible kwenda popote atakapopangiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ipeleke watumishi wa afya katika maeneo ya vijijini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Pia pale penye upungufu wa watumishi au watumishi kutakiwa kufanyakazi masaa ya ziada tunaomba Halmashauri na Wizara kuwalipa malipo yao ya kazi za ziada au on call allowances wapewe na ikiwezekana Serikali iwaongezee, shilingi 25,000 ni ndogo sana. Serikali ione uwezekano wa kuongeza kiwango hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mimba za utotoni na ukatili wa watoto; pamoja na tatizo hili kuchangiwa na mila na desturi pamoja na imani za kishirikina, pia wazazi kutotimiza wajibu wao wa malezi inachangia watoto wengi kupata mimba wakiwa na umri mdogo. Kila mzazi anatakiwa na ana wajibu wa kumlea mtoto wake katika maadili mema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi wanaacha watoto wao walelewe na house girls na television, vitu hivi ndivyo vinavyochangia watoto wengi kukosa malezi bora. House girls na television ndio wamekuwa walimu wa watoto hususani kwenye upande wa ngono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalosababisha mimba za utotoni na ukatili kwa watoto ni umbali wanaotembea watoto wetu kwenda shuleni. Mtoto anayetembea zaidi ya kilometa tano kwenda shule ya msingi au sekondari, ana hatari kubwa ya kukumbana na vishawishi vya ngono kuliko mtoto anayetembea chini ya kilometa tano. Shule nyingi zilizopo maeneo ya vijijini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wapo hatarini kujiingiza kwenye vitendo hivyo na hatimaye kupatikana na ukatili wa kijinsia au mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kutatua matatizo ya mimba za utotoni ambazo kwa sasa zinasababishwa na vijana wanaotoa msaada wa usafiri (lift) bodaboda na magari na kuwafanyia ukatili watoto wetu, ni vizuri Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI, tuje na mpango wa kujenga hostels kwenye shule zetu za msingi na sekondari ili kuwaepusha watoto wetu kuingia kwenye vishawishi vitakavyopelekea kwenye matatizo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za damu salama, bado kuna changamoto ya watu kujitolea kuchangia damu na maeneo mengine hasa vijijini wananchi wengi hawapo tayari kuchangia damu mpaka walipwe. Hivyo Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi waishio vijijini juu ya umuhimu wa kuchangia damu. Hii itaongeza mwamko wa wananchi waishio vijijini kuchangia damu bila malipo pale wanapoombwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.