Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Wizara hii ni nzuri na Waziri na Naibu Waziri wanafanyakazi vizuri kabisa. Tunawatia moyo muendelee kuwa wabunifu na kusimamia maadili ya wafanyakazi walio chini yenu. Pamoja na kuunga mkono hoja nina mambo yafuatayo kuishauri na kuiomba Wizara kwanza Nkasi tuna uhaba wa watumishi wa afya yaani madaktari, wauguzi na wataalam wa maabara. Kwa vile tuko pembezoni hali siyo nzuri, tusaidieni watumishi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nkasi huduma hutolewa kwenye zahanati chache kabisa, wananchi wamejenga maboma zaidi ya 30 Wilaya nzima hayajamaliziwa yanahitaji kuezekwa, tunaomba bati ili wananchi waielewe Serikali iliyowahimiza wajenge na majengo yao yataezekwa.

Mheshimia Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya iliyopo inamilikiwa na Wamisionari na usimamizi wa huduma siyo mzuri kabisa. Naomba mtusaidie tujenge hospitali yetu, huduma hazitolewi kwa msingi ya maadili hata mchango wa Serikali hauwanufaishi wananchi wa Nkasi ipasavyo.

Mheshimia Mwenyekiti, Nkasi bado kuna ukoma hasa maeneo ya mwambao mwa Ziwa Tanganyika. Naomba Wizara itambue jambo hilo na kuongeza huduma katika eneo hili. Pia dawa bado hazitoshelezi, nashauri fedha za dawa ziongezwe zaidi. Aidha, walemavu wawekewe utaratibu wa kutibiwa bure, hii ikiwa ni pamoja na walemavu wa ngozi (albino), walemavu wa ngozi wanashida sana huko vijijini na hapajawa na ufuatiliaji toka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya nchini kote. Naomba ufuatiliaji uwe unafanyika, watambuliwe na wasimamiwe huduma za ushauri na matibabu yao.

Mheshimia Mwenyekiti, Nkasi kuwa pembezoni kuna vifo vingi vya akina mama na watoto. Hatuna vituo vingi vya afya hasa Jimbo la Nkasi Kusini. Naomba Serikali iweke miundombinu kwenye kituo cha afya cha kata ambacho kilijengwa na Benjamin Mkapa Foundation ili huduma ziweze kuanza kutolewa kama ilivyokusudiwa.

Mheshimia Mwenyekiti, nina maombi maalum, naomba gari ya wagonjwa katika kata ya Kala lipatikane ili kupunguza vifo vingi vinavyotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni watumishi wa afya walioonekana wana vyeti visivyokuwa halali wachunguzwe vizuri ili wale wenye weledi wasaidie kupunguza upungufu kwa masharti mapya, wale wasiofaa waachishwe kazi kabla ya kufukuzwa, haya ni maoni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kitengo cha MOI kinachotoa matibabu ya mifupa, kiangaliwe hakina huduma nzuri na wauguzi na hata madaktari hawana maadili kabisa. Watu wanapoteza maisha wakati mwingine bila sababu za kutosha, nina shaka huenda kuna shida ya kuhitaji visenti ingawa sina ushahidi, hii ni kutokana na urasimu uliopitiliza wa kupata kitanda hata kwa mgonjwa ambaye hajiwezi kabisa.