Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa fursa hii ya kuweza kuchangia kwa maandishi. Natumia fursa hii ya kufanya wajibu wangu wa Kibunge kwa kuishauri Serikali katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa jana katika michango yangu Bungeni kwa Wizara hii nilitoa ushauri kwa Serikali kwamba Serikali iliangalie suala la hedhi na upatikanaji wa sanitary pads. Natumia fursa hii kuikumbusha Serikali haja ya kulishughulikia suala la hedhi ili kusaidia kupunguza mimba za utotoni na school drop-outs kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iunde chombo ndani ya TFDA kitakachofanya kazi ya kusimamia bei ya bidhaa ambazo zimeondolewa VAT kama vile dawa na sanitary pads ili lengo la kuondoa VAT liweze kutimia kwa kuwasaidia wananchi kupata bidhaa hizo kwa bei rafiki tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyabiashara hujipatia faida kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa sanitary pads kunamfanya mtoto wa kike kukosa siku nne mpaka saba suala ambalo linajenga utoro shuleni. Watoto wakike hukosa ujasiri kwenda darasani kwa kuwa hawana vifaa bora vya kujihifadhia kipindi cha hedhi. Utoro huo wa siku nne hadi saba humfanya mtoto wa kike kupoteza muendelezo wa kimasomo na hivyo mtoto wa kike anakuwa katika hatari ya kufanya vibaya katika masomo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoro pia unachangia katika ongezeko la school drop-outs, yaani kuacha shule kwa watoto wa kike ambapo baadaye huleteleza (husababisha) mimba za utotoni. Ni vyema Serikali ikalitazama suala hili kama suala muhimu na kuweza kulifanyia kazi ili kuwaokoa watoto wetu. Serikali ikisaidia kupatikana kwa sanitary pads kwa bei rafiki au bure itasaidia kuongeza kiasi cha ufaulu cha watoto wa kike kwa kuwa utoro utakoma na upatikanaji wa sanitary pads utapunguza idadi ya watoto wa kike wanaoacha shule na hivyo kupunguza mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu iratibu suala la upatikanaji wa pesa ili kugharamia sanitary towels. Serikali iongeze pesa kwenye capitation funds ili watoto wa kike wapate sanitary pads/ towels mashuleni. Katika kusimamia hilo, Serikali ihakikishe anapatikana mwalimu wa kike (matron) atakayeshirikiana na Mwalimu Mkuu wa Shule katika kusimamia pesa za capitation ambazo zitakuwa zimepangwa kwa ajili ya upatikanaji wa sanitary pads. Matron atawajibika kuunda girls club mashuleni ili kujua namna ya kutumia na kupata sanitary pads lakini pia girls clubs hizi zitasaidia kutoa elimu ya afya ya uzazi. Wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wapatiwe ongezeko kwenye mkopo ili waweze kugharamia sanitary pads.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeandaa hoja binafsi ingawa kutokana na ufinyu wa nafasi sijaweza kuiwasilisha; pamoja na kwamba imewasilishwa kwa Mheshimiwa Spika na Katibu wa Bunge. Hoja hiyo niliijenga katika kuliomba Bunge liazimie kuitaka Serikali katika kubadilisha kifungu cha dawa kuwa katika fungu la matumizi ya kawaida ya Wizara. Kwa sasa kifungu cha dawa kiko kwenye fungu la bajeti ya maendeleo ya Wizara ambapo pesa hizo hazipatikani au kutolewa kwa kila mwezi na hivyo kuathiri upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fungu la bajeti ya maendeleo la Wizara katika magonjwa kama UKIMWI na TB hutegemea wahisani ambao huchelewa kutoa pesa hivyo huathiri upatikanaji wa dawa. Ni vyema sasa Serikali ikaweka pesa za dawa na vifaa tiba katika fungu la matumizi ya kawaida na ifuate vipaumbele kama ifuatavyo; kwanza, mshahara; pili, dawa za binadamu na vifaa tiba na tatu matumizi mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia dawa za binadamu kuwa na pesa za uhakika ambazo ni pesa za ndani na hivyo kuondoa tatizo la upatikanaji wa dawa. Kwa kusema pesa za dawa za binadamu na vifaa tiba namaanisha dawa pamoja na vifaa tiba wezeshi kama vile pamba, sindano, gloves na si vifaa kama x-ray machines ambazo zibaki kwenye fungu la maendeleo ya bajeti, ahsante.