Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ambayo iko mbele yetu. Kwa sababu ya muda niende haraka; pamoja na juhudi ambazo zinafanywa na Serikali na kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri tumeiona ametusomea tumeona mengi yaliyofanyika, lakini kiukweli bado tatizo la afya katika nchi yetu halijafikia katika standard ambayo tunaweza tukajisifia, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika nchi yetu maeneo mengi sana wataalam, watumishi wa afya, maeneo yote kuanzia hospitali kwenda kwenye zahanati, vituo vya afya, bado ni wachache sana. Kwenye maeneo yetu, mfano tu ukienda Wilaya ya Kaliua vituo vya afya, kwanza tunavyo vichache, viko viwili tu, lakini kuna wahudumu watatu mpaka wanne; hebu niambie kwa eneo ambalo lina watu karibu laki tatu, wanahudumiwaje? Vile vile zahanati zina Mganga mmoja au Nesi mmoja akiugua mmoja wapo au wote wakiugua, zahanati imefungwa na watu hawapati huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wajawazito wanakaa zahanati kuanzia saa kumi na mbili asubuhi mpaka jioni hospitali imefungwa, hakuna huduma. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na juhudi zote lakini lazima kuhakikisha kuna watumishi wa kutosha kwenye maeneo yetu ya vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vingi vya afya kwanza havina Madaktari, lakini pia havina vifaa tiba vya kupimia malaria na magonjwa mengine. Leo Kaliua mtu akiwa na malaria, mpaka aende Urambo, vituo vya afya havina hata vipimo vya kupima magonjwa madogo tu mpaka aende Wilaya ya Urambo. Kwa hiyo naomba, kwa kuwa lengo ni kupunguza vifo vya Watanzania vituo vya afya vyote viwe na vipimo vile vya kawaida kama vile vya kupima malaria na BP viwepo; vinginevyo hatuwezi kupigana na suala la vifo vinavyotokea ambavyo ni vingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Wilaya ya Kaliua hatuna Hospitali. Kwa nguvu za wananchi na fedha za ndani tumeanza kujenga jengo la OPD, lile ni jengo la ghorofa moja na lina vyumba vyote vya muhimu, tumejibana kwelikweli kwenye mapato ya ndani. Naiomba Serikali, sasa hivi tupo kwenye hatua za mwisho, tumeshapaua, bado kupiga rangi, kuweka milango na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Serikali iweke mkono wake pale, itusaidie pale tulipofikia tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na Hospitali ya Wilaya. Kutoka Kaliua kwenda Urambo ni zaidi ya kilomita 35, lakini pale hakuna huduma ya operesheni hakuna chochote kinachofanyika. Mtu ambaye hali yake ni mbaya na barabara hakuna kutoka Kaliua mpaka Urambo, wengi wanajifungulia njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, hospitali ile ambayo tumeshaanza OPD iongezewe fedha za kutosha ili iweze angalau ndani ya muda mfupi tuweze kuhakikisha kwamba ndani ya Wilaya yetu ya Kaliua tunakuwa na Hospitali ya Wilaya tuweze kuokoa maisha ya akinamama na watoto ambayo yanapotea kila kukicha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kuwepo na vituo vichache. Sera inasema na ni Sera ambayo tunatamani itekelezwe; kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati, lakini mbona mpango huo hauzungumziwi? Kila kata iwe na kituo cha afya, mbona mpango huo hauzungumziwi? Leo tunasema tunaokoa akinamama wajawazito na watoto, tunawaokoaje wakati unakuta vijiji kati ya 100 labda zahanati ziko tano au kumi? Leo Kaliua ina vijiji 101, zahanati hazizidi 20. Si kila kitu wananchi wanaweza kukifanya; ni kweli wanafanya na tunawahamasisha wanafanya, lakini ni ngumu kwa wananchi kujenga kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunawaomba ile Sera ya Serikali itekelezwe ili tuweze kuwa na zahanati kila kijiji, tukaweza kuwa na kituo cha afya kila kata. Naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, mwaka jana tumepata mwongozo kwenye vikao vyetu vya Halmashauri, Mheshimiwa Waziri alituma barua kwamba kila kata mbili ziandae maeneo kwa ajili ya kujenga vituo vya afya, tumeshaandaa yale maeneo, tukashauriana kila kata mbili zikaandaa eneo la kujenga Hospitali. Hebu atuambie, ni lini ujenzi au maandalizi ya kuanza kujenga vituo vya afya utaanza?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: …Kwa sababu maeneo yametengwa yako pale na yako kwenye Wizara.